NA ABUU BAKAR, ZU@@@@
WANAFUNZI wa skuli za Micheweni kisiwani
Pemba, wametakiwa kuacha utoro na kuhudhuria masomoni kikamilifu, na hali ngumu
ya maisha inowakabili, isiwe chanzo cha katitisha masomo.
Kauli imetolewa
na Afisa Elimu Sekondari wa Wilayani humo, Rishad Kombo
Faki, wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii, ofisini kwake Micheweni,
juu ya utoro kwa baadhi ya wanafunzi, kwa kisingizio cha hali ngumu ya maisha.
Alisema
hali ya kimazingira iliyopo Micheweni, isiwe chanzo kwa wanafunzi hao kukatisha
masomo yao, kwani elimu ni haki yao ya msingi.
Alieleza kuwa,
wazazi wamekuwa wakipambana, ili kuhakikisha wanawapatia watoto wao huduma za
kila siku na za lazima, hivyo ni wajibu kwa wanafunzi hao kuthamini jambo hilo.
“Ni kweli
mazingira yaliyopo Micheweni yana vivutizi vingi vinavyo sababisha wanafunzi
kuwa watoro, na hii inatokana na wanafunzi kupata
marafiki wasio kuwa wazuri kitabia,”alifafanua.
Akizungumzia
athari ya wanafunzi kuwa watoro masomoni, alisema mojawapo ni kudumaa
kiakili, kuongengezeka kwawasiojua kusoma na kuandika na kujirahisishia kuingia
katika vitendo viovu.
Kwa upande
wake Mwalimu mkuu wa skuli ya sekondari ya Tumbe Nassor Rashid Said alisema, muamko
mdogo kwa baadhi ya wazazi na walezi juu ya elimu, unasababisha kwa wanafunzi
kua watoro masomoni.
Mwalimu mkuu
huyo aliwataka wazazi na walezi, kuwa na ushirikiano katika kuwalea vijana wao
na asiachiwe mzazi wa wakike pekee, kwani kufanya hivyo, kutaporomosha
maendeleo ya elimu ya mtoto.
"Ulezi ameachiwa
mzazi wa kike tu, na ndio maana hata tukiwaita kwenye vikao vya skuli, inakuwa
vigumu kuwapa wazazi wanaume, jambo ambalo wakati mwengine, huzorotesha
maendeleo ya elimu kwa mtoto,”alifafanua.
Mzazi Bimzungu
Ali Rashid alisema kuwa,
changamoto za kimaisha za majumbani, wakati
mwengine ni tatizo linalowapelekea wanafunzi kuwa watoro masomoni.
"Ugumu wa
maisha unaotukabili sisi wazazi huko majumbani kwetu na wanaume kutuachia
majukumu peke yetu, nikichocheo kikubwa kwa watoto wetu kutohudhuria masomoni,
kikamilifu,”alieleza.
Naye, mzazi Sabrina
Haroun Hamad, alieleza
kuwa ni vyema kwa wazazi na walezi wenzake, kuwasaidia vijana wao, ili
kukamilisha ndoto zao za kielimu.
Wanafunzi Sada
Ali Hamad na Kombo Mohamed Said wa kidato cha pili skuli ya Tumbe, wamewawataka
wanafunzi wenzao, kutojihusisha na utoro, kwa kisingizio cha hali ngumu ya
maisha, kwani kufanya hivyo kutapoteza ndoto zao za maisha.
Afisa Mdhamini
wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Mohamed Nassor Salim, alizitaka
kamati za wazazi za skuli, kusimamia utoro kwa wanafunzi ili kuhudhuria
masomoni.
MWISHO.
Comments
Post a Comment