NA ABDI SULEIMAN, PEMBA@@@@
MKURUGENZI wa Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu Zanzibar Ali Suleiman Mussa amesema, kutokana na kuongezeka kwa utapeli katika jamii ni vyema wakulima wa karafuu kuendelea kutumiwa fedha zao kwenye akaunti ya TigoPesa, ili zibaki kuwa salama.
Alisema, njia hiyo itaweza kuwasaidia wakulima wa zao la karafuu, fedha zao kuendelea kuwa katika hali ya usalama muda wote na sio kuchukua mkononi, kwani inahatarisha maisha yao.
Mkurugenzi huyo aliyaeleza hayo wakati akifungua mkutano wa wakulima wa karafuu Mkoa wa Kaskazini Pemba, juu ya kuhamasisha kutumia mtandao wa simu ya Tigo Pesa katika kutumiwa malipo yao baada ya kuiuzia Serikali karafuu zao.
Aliwataka wakulima hao katika msimu wa karafuu ulioanza Agosti 3 mwaka huu, kuhakikisha wanatumia mitandao ya simu kuweka fedha zao, huku Shirika la ZSTC likiendelea na mchakato wa kuwasajili wakulima wote.
“Kutumia mitandao katika kuhifadhi fedha ni sehemu salama, kuliko kuondoka na fedha mkononi, wengi wanakumbana na changamoto za kuungua, kuliwa na mchwa au panya ikiwa fedha hizo zimehifadhiwa majumbani na hata kutapeliwa”, alisema.
Alieleza kuwa, mkulima aliyesajiliwa anapopatwa na tatizo wanampa kipaombele cha kumshughulikia kuliko asiesajiliwa, kwa sababu aliesajiliwa anatambuliwa kwake na Shirika hilo.
Nae Mdhamini wa Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) Pemba Abdalla Ali Ussi, aliwataka wakulima kukubali kulipwa fedha zao kupitia huduma ya TigoPesa na kama kuna matatizo wasisite kutoa taarifa kwa wahusika.
Alisema, ulipaji wa fedha kwa kutumia mitandao ya simu ni rahisi, kwani mtu anapata fedha zake kwa wakati na kiwango kikubwa, hivyo ni vyema kuliunga mkono Shirika kwa mfumo huo waliouweka, kwani lengo lao ni kuhakikisha fedha zote za wakulima wao zinakuwa salma.
Aidha aliwafahamisha wakulima hao kuwa, ZSTC tayari imeshafungua vituo vyake vya ununuzi wa karafuu kwa Unguja na Pemba tokea Agosti 3 na tayari tani mbili za karafuu zimeshanunuliwa.
Kwa upande wake Meneja wa TigoPesa Zanzibar Salum Nassor Mohamed alisema, tangu kuanza kwa malipo ya wakulima wa karafuu Unguja na Pemba mwaka 2021 hadi 2023, zaidi ya wakulima 10,000 wameshapokea malipo kupitia tigoPesa na zaidi ya bilioni 40 zimepelekwa kwa wakulima hao kupitia mitandao ya simu.
Alisema, faida ya kutumia tigopesa ni njia salama ya kuweka fedha kuliko kuchukua mkononi na ikitokea bahati mbaya ya kupoteza simu, bado fedha zao zitaendelea kuwa na usalama.
Nae Meneja wa TigoZantel kanda ya Pemba Farouk Ahmed alisema, mawakala wa kampuni hiyo watahakikisha wanakuwepo katika vituo vyote vinavyohusika na mauzo ya zao la karafuu.
Aidha aliahidi kwamba, hakutokuwepo na changamoto yeyote ya kukosekana kwa mawasiliano ya mtandao, kwani wamejipanga kuendelea kuboresha huduma hizo.
Kamanda wa ZAECA Mkoa wa Kaskazini Pemba Nassor Hassan Nassir, aliwapongeza wakulima wa karafuu kwa mashirikiano makubwa walioyatoa katika msimu uliopita na akuwataka kuendelea na msimu huu.
Mkulima wa karafuu kutoka Kisiwani kwa Binti Abeid Mohamed Salum Ali, aliwapongeza Tigo Zantel kwa mikakati yao mizuri mwaka jana, kwani aliweza kupokea fedha kwa wakati muwafaka bila ya usumbufu wowote.
Aidha alisema, changamoto kubwa ilikuwa kwenye viwango vya mikato kwani ilikuwa mikubwa sana kiasi ambacho kiliwakwaza, hivyo aliwaomba kuweka wazi suala la makato kwa wakulima.
Nae mkulima Mohamed Ali Mmaka kutoka Mtambwe, aliitka TigoZantel kuhakikisha wanawafutilia matepeli wanaotumia mitandao ya simu, ili kujuwa wanaovujisha siri za wateja wao.
MWISHO
Comments
Post a Comment