NA
TATU NAHODA, ZU@@@@
WANAKIJIJI
wa kisiwa cha Kojani shehia ya Mpambani wilaya ya Wete Pemba, wameishukuru
polisi jamii yao, kwa kudhibiti na kukabiliana na vitendo vya kihalifu kijijini
hapo.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi
kijijini hapo, wananchi hao walisema, tokea kuanzishwa kwa ulinzi shirikishi
shehiani hapo, vitendo kadhaa vya kihalifu vimepungua.
Walisema kuwa, ulinzi shirikishi umekuwa
muarubaini tosha katika kijiji chao, kwa kupunguza matendo maovu, jambo ambalo
kabla ya hapo halikuwepo.
Wananchi hao walieleza kuwa, umoja na
mshikamano uliopo, umesaidia kudhibiti vitendo viovu, kama vile wizi wa mazao
na mifugo, na kupelekea kuishi kwa amani na utulivu.
Mmoja
kati ya wananchi hao Said Haji Said alisema, kwa sasa mifugo na vipando vyao vinanawiri,
kutokana na kuimarika kwa ulinzi shirikishi, kijijini kwao.
Alisema kwa sasa wafugaji, na wakulima
wanavuna wanachokipanda kwa wakati, kutokana na kuimarika kwa ulinzi shirikishi,
jambo ambalo halikuwepo kwa muda mrefu kijijini kwao.
“Sisi wananchi lazima tutoe shukrani zetu kwa
vijana wetu wa ulinzi shirikishi, maana sasa ndizi inapea, mihogo, kuku na hata
wizi wa kawaida wa majumbani umepungua, alisisitiza mwananchi huyo.
Na mwananchi Fatma Nassor Ali alieleza kuwa,
kuimarika kwa ulinzi shirikishi kijijini kwao, imetoa fursa kwa wanawake na
watoto, kutembea bila ya wasiwasi hasa nyakati za usiku wamapema wanapokuwa na
shughuli zao.
Aidha Mwanakame Kombo Hassan, alisema
kilichobakia kwao, ni kuendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu na kikundi cha
ulinzi shirikishi, katika kuiweka shehia yao salama.
Mapema Mjumbe wa polisi jamii shehiani hapo, Othman
Mwinyi Shezume alisema, polisi jamii
imekuwa ikifanya kazi zake ipasavyo, ili kudhibiti vitendo vyote vya kihalifu,
kijijini hapo, kama vile wizi, ubakaji uporaji na utoro wa watoto masomoni.
Alieleza kuwa, wamefanikisha majukumu yao
hayo, na yameleta mafanikio makubwa, kutokana na kuwepo kwa ushirikiano mzuri,
baina yao na wanakijiji wa shehia hiyo.
"Jukumu la kulinda na kudhibiti vitendo
viovu, ni jukumu la kina wanakijiji pia, hivyo ushirikiano wao na sisi
waliotukabidhi jukumu hili, utaweza kuleta matunda mazuri katika kijiji chetu,’’alifanunua.
Kwa upande wake Naibu Sheha wa shehia hiyo
Hassan Iddi Othman, aliwaomba wanakijiji wa shehia ya Mpambani, kuzidi kuleta ushirikiano
na polisi jamii, ili kuunga mkono juhudu zao kwa lengo la kufanikisha azma yao.
Hata hivyo aliiomba, serikali kuendelea kutoa
ushirikiano wa hali ya juu na polisi jamii hiyo, juu ya changamoto ambazo
wanapitia wakati wa utendaji wa kazi zao, kwa kuwapa mafunzo maalum.
MWISHO
Comments
Post a Comment