NA MWANDISHI WETU, PEMBA
JAMII kisiwani Pemba, imetakiwa kufahamu changamoto
na viashiria vya udhalilishaji kwa watoto, ili kuwalinda na vitendo hivyo.
Hayo yameelezwa
na Mwenyekiti wa Mtandao wa Asasi za Kiraia Pemba ‘PACSO’ Mohamed Ali Khamis,
mara baada ya kuutambulisha mradi wa kujadili changamoto zinazowakabili watoto,
katika ukumbi wa kiwanda cha Makonyo Wawi Chake chake Pemba.
Alisema,
jamii inapaswa kuwa karibu mno na watoto wao, ili kujua haraka viashiria vya
kudhalilishwa, na sio kusubiri hadi janga liwakumbe.
Mwenyekiti
huyo alieleza kuwa, hilo litakuwa rahisi ikiwa wazazi na walezi watatenga muda
wa kuwa karibu na watoto wao.
‘’Kama
tunajiona tuko na harakati nyingi za maisha na kusahau kukaa na watoto wetu,
wanaweza kukumbwa na janga kama la udhalilishaji na tukachelewa
kufahamu,’’alieleza.
Akielezea
lengo la mradi huo Mwenyekiti huyo wa PACSO, alisema ni kuwazindua wazazi,
kufahamu viashiria na changamoto na namna ya kuwasaidia watoto wasifanyiwe
matendo hayo.
Akifungua
mafunzo hayo, Mratibu katika ofisi ya usajili wa asasi za kiraia Pemba, Ashrak
Hamad Ali, alisema baadhi ya wazazi wanakosa muda wa kukaa na watoto wao, ili kusikiliza
changamoto zinazowakabili.
Aidha aliwataka
wazazi kujenga utamaduni wa kukaa na watoto wao ili kuwapa fursa ya kuwasikiliza
sambamba na kufuatilia nyenendo zao za kila siku.
Katika
hatua nyingine, Mratibu huyo, aliwataka waandishi wa habari kushirikiana na
viongozi wa dini, kutoa elimu kwa wanandoa, ili kupunguza talaka za kiholela.
‘’Wakati
mwengine wapo watoto wetu wanakumbana na changamoto za kimaisha na kisha
kudhalilishwa ama kutelekezwa, moja ya sababu ikiwa ni wazazi
kutengana,’’alifafanua.
Akiwasilisha
mada kwenye mkutano huo kuhusu changamoto zinazowakabili watoto, Mratibu kutoka
Chama cha waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA– Pemba Fat- hyia Mussa
Said, alisema watoto wana haki ya kushiriki na kushirikishwa kwenye ngazi za
kijamii.
Akizitaja
baadhi ya haki hizo kupitia mkataba wa kimatifa wa mwaka 1988 ni pamoja na ya
kuishi, kuendelezwa kwa mujibu wa sera ya maendeleo ya mtoto Tanzania, kulindwa
na vitendo viovu pamoja na haki ya kushirikishwa.
Nao
washiriki wa mkutano huo, Aisha Abdallah Juma na mwenzake Abdurr-azak Imam Juma,
walisema ni hatari kwa wazazi kupuuzi taarifa wanazopewa na watoto wao.
Sheha wa
shehia ya Pembeni wilaya ya Wete Saumu Ali Hamad na mjumbe wa sheha shehia ya
Wambaa Amini Haji Makame, walisema kukosekana kwa uthubutu wa wazazi, kuwakemea
watoto kuiga mitindo ya kigeni ni moja ya chanzo cha kutokea kwa changamoto
hizo.
Awali, Mratibu
wa miradi kutoka PACSO Mohamed Najim Omar, alisema kama jamii haikuungana kama
ilivyokuwa zamani kwenye malezi, watoto wataendelea kukumbwa na changamoto.
Aidha
aliwataka washiriki wa mkutano huo, kuisambaaza elimu walioipata, ili kuona
wazazi na walezi wanakuwa na mamko wa malezi kwa watoto wao.
Mradi huo wa miezi sita unatekelezwa kwa ufadhili wa Shirika la Irish
Aid, unaendeshwa na Mtandao wa Asasi za Kiraia Pemba ‘PACSO’.
Mwisho
Comments
Post a Comment