NA MOZA SHAABAN, ZU
WAKULIMA katika Shehia ya Kojani
Wilaya ndogo ya Kojani mkoa wa Kaskazini Pemba, wamewalalamikia wafugaji kutodhibiti
mifugo yao, jambo ambalo hupelekea uharibifu wa mazao yao.
Akizungumza na Zanzibar leo, mkulima wa Viazi
vitamu Saada Ali Faki kijijini hapo, alisema wamekua wakijishughulisha na
kilimo ili kujikwamua kiuchumi, ingawa wafugaji hurejesha nyuma jitihada zao.
Alisema wamekuwa wakitumia nguvu na gharama
kubwa, kupanda mazao ili yawasaidie kiuchumi, ingawa malengo yao hayafikiwi
kwani wafugaji hushindwa kudhibiti mifugo yao na kufanya uharibifu mkubwa.
"Sisi
tunatumia nguvu kupanda mazao, ili yatusaidie na familia zetu, ingawa wafugaji
wanaturejesha nyuma kwa kuachia huru mifugo yao na kutuharibia mazao yetu,”alisema.
Nae
mkulima wa zao la Mtama Bikombo Said Hamad alisema, wamekua wakichukua hatua
kadhaa, ili kudhibiti suala hilo ikiwemo kuripoti matukio hayo kwa uongozi wa
shehia na hatua stahiki kuchukuliwa, ingawa bado suala hilo linaendelea kijijini
kwao.
Akizungumzia
kadhia hiyo, mfugaji wa Ng'ombe na Mbuzi, Hassan Hussein Makame alisema, kuna
haja kubwa kwao kudhibiti mifugo yao ili kuzuia uharibifu unaotokezea.
Alisema,
iwapo watadhibiti mifugo yao, watatoa fursa kwa wakulima, kuendeleza kilimo
chao, ili wapate tija kama wanavyo tarajia wenyewe.
Katika
hatua nyingine amewaaasa wakulima, kutolinyamazia suala hilo, na ni muhimu
kuliripoti katika vyombo vya sheria, ili wafugaji wasiodhiti mifugo yao
kuchukuliwa hatua.
Nae
mfugaji wa Mbuzi Issa Mohamed Yakoub, alisema wamekuwa wakiidhibiti, ingawa
uharibifu mwengine unatokea, pale wanapokata kamba.
‘’Wakati
mwengine mifugo hukata na kupelekea uharibifu wa mazao, lakini sio kama
tunawaharibia kwa maksudi wakulima, kwani hao ni ndugu zetu,’’alifafanua.
Naibu
Sheha wa shehia hiyo Ali Hamad Ali, alisema amekua akipokea malalamiko mara kwa
mara kutoka kwa wakulima, juu ya wafugaji kutodhibiti mifugo yao, na tayari
wameshachukua hatua kadhaa, kama kuzungumza na wafugaji.
“Hatua
nyingine tunazozichukuwa ni kulipisha faini kwa mfugaji, ingawa bado suala hilo
ni sugu kijijini hapa, na naendelea kutoa wito kwa wafugaji, kudhibiti mifugo
yao ili, kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima,”alifafanua.
Hata
hivyo amewataka wakulima kufanya mazungumzo ya utatuzi wa migogoro baina yao na
wafugaji na wajiepushe na kujichukulia sheria mikononi.
Mkuu
wa wilaya ya Wete Dk. Hamad Omar Bakari, alieleza kuwa wilaya itaendelea kuwatuma
wataalamu na kutoa elimu ya kukinga na migogoro inayoepukia.
Mwisho
Comments
Post a Comment