NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANANCHI wa kijiji cha Mleteni, shehia
ya Kisiwani wilaya ya Wete Pemba, katika kukabiliana na dawa za kulevy na wizi,
wameendelea kupiga marufuku kwa mgeni yeyote, kuingia kijijini hapo, pasi na
taarifa kwa uongozi wa kijiji.
Walisema, hawatomvumilia
mgeni wala mwenyeji aliyefuatana naye, ikiwa watabainika ameingia kinyemela
kijijini hapo na hakuna taarifa rasmi.
Walieleza
kuwa, kwa sasa kijiji chao cha Mleteni, kiko salama kiasi, kwa dawa za kulevya
na hata wizi, ndio maana wanawasisitiza wenyeji wanaotembelewa na jamaa zao,
kutoa taarifa rasmi, kwa uongozi wa kijiji.
Mmoja kati
ya wananchi hao Salim Mussa Ali, alisema ingawa utumiaji wa dawa za kulevya
bado uko chini, lakini wanaendelea kuwataka wenyeji, wanaoingia na wageni wao,
kutoa taarifa rasmi.
‘’Tumeshagundua
kuwa, wapo wageni wengine wanakuja na nia mbaya katika kijiji chetu, sasa
tukigundua na ikawa ana mwenyeji wake wa kijiji cha Mleteni, tutamfikisha mbele
ya vyombo vya sheria,’’alieleza.
Nae Yassir
Said, alisema bado kijiji chao kiko salama na utumiaji mkubwa wa dawa za
kulevya, na ndio maana kila mgeni anayeingia, wamependekeza, kuwepo kwa taarifa
zake kamili.
‘’Inawezekana
ile mikakati yetu ya kila wakati, ikawa inasaidia kupunguza wimbi la vijana
kuzurura ovyo, na baadhi ya wakati ndio wanaojihusisha na utumiaji wa dawa za kulevya,’’alieleza.
Akizungumzia
juu ya wizi wa mazao kijijini hapo, mwananchi Alawi Said Yussuf, alisema wizi
ni mkubwa kiasi, ingawa kwa sasa wanajiandaa kuanzisha kamati maalum.
Alisema,
mifugo kama kuku na mazao kama ndizi, mihogo imekuwa ikiibiwa hasa nyakati za
usiku, ingawa wamebaini ni watoto wao na sio wageni.
Kwa upande
wao Asha Ali Sharif na mwenzake Aisha Nassib Shehe, walisema bado mkakati wa
kweli na endelevu haujakuwepo wa kudhibiti vitendo vya wizi.
‘’Ni kweli
utumiaji, usambaazaji na uuzaji wa dawa za kulevya kwenye kijiji chetu cha
Mleteni haupo, lakini kama tukishindwa kudhibiti wizi, kisha dawa za kulevya
zitafika,’’walisema.
Kaimu sheha
wa shehi ya Kisiwani wilaya ya Wete, Bahati Juma Mtwana, aliwataka wananchi hao
wa kijiji cha Mleteni, kuanzisha haraka ulinzi shirikishi kijijini hapo.
Alisema, kwa
sasa karibu kila kijiji kwa Unguja na Pemba, kimeshaathirika kwa wizi, dawa za
kulevya, vitendo vya udhalilishaji, hivyo kama kijiji chao cha Mleteni kiko
salama na dawa za kulevya, waendelee kudhibiti.
Kaimu sheha
huyo alisema, ingawa kwa sasa wamo katika kuufufua ulinzi shirikishi, lakini
sio vibaya kijijini hapo wanao watakuwa na kamati yao.
Katika hatua
nyingine, Kaimu sheha huyo wa shehia ya Kisiwani, amewakumbusha wananchi
kuendelea kutoa taarifa Polisi, pindi wakibaini kuwepo kwa vitendo vya
kihalifu.
‘’Kwa mfano kuna ubakaji, wizi, dawa za kulevya au jambo jingine lolote linaloashiria uvujivu wa amani, wasijaribu kuchukua hatua mikononi na badala yake, wawasiliane na mamlaka husika,’’alisisitiza.
Hata hivyo,
amewataka wananchi hao kuwashajiisha watoto kuhudhuria masomoni, kwani serikali
imesikia kilio chao cha ujenzi wa skuli ya maandalizi.
Mkuu wa
wilaya ya Wete Dk. Hamad Omar Bakar, alisema wakati umefika sasa wa kuendelezwa
kwa kamati za ulinzi shirikishi katika shehia.
Mwisho
Comments
Post a Comment