IMEANDIKWA NA
ZUHURA JUMA, PEMBA
WAJASIRIAMALI
wa kikundi cha mboga na matunda cha ‘Hufedheheki’ kilichopo Kwale Mpona Finya wamesema,
wanafurahia uongozi wa Katibu wao Subira Mkubwa Mohamed namna anavyopigania
katika kuhakikisha kikundi hicho kinapata maendeleo.
Walisema kuwa, amekuwa akiwashirikisha hatua
kwa hatua katika masuala yote ya kikundi, jambo ambalo linawapa faraja kwani
wanakuwa na uhuru wa kutoa maoni yao na baadae kuyafanyi kazi kadiri anavyoweza.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi
wanakikundi hao walisema, Katibu wao huyo anapambania kwa hali na mali
kuhakikisha kikundi kinazalisha zaidi na kujipatia kipato kitakachowakwamua
kimaisha.
Mwanakikundi Khamis Ali Khamis alisema, mama
huyo ni kiongozi mchapa kazi na mchakarikaji kiasi ambacho na wao hupata nguvu
ya kuzalisha zaidi bidhaa zao kwa lengo la kujipatia mafanikio.
Alisema, wamepata manufaa mengi kupitia kiongozi
huyo mwanamke kutokana na kuwa anawahamasisha kufanya kazi kwa bidi, ili
kuondokana na hali ngumu ya maisha, ambapo wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa
katika uzalishaji.
"Tumejifunza vitu vingi kupitia Katibu
wetu huyu kwa sababu anapambana kuhakikisha tunazalisha bidhaa nyingi na zenye
ubora ili kukuza soko,” alifafanua.
Nae mwanakikundi Salma Said Salim alieleza
kuwa, mama huyo anaweza kugombea nafasi yoyote ya uongozi na akaitumikia vizuri
jamii yake, kutokana na utendaji kazi wake ulio bora.
"Jinsi anavyosimama imara kutatua
changamoto zetu za kikundi, naamini atakapoingia jimboni na kushinda, basi
ataibua matatizo yaliyomo ndani ya jamii na kuyatafutia njia mbadala ya kuyatatua,”
alisema.
Alisema kuwa, kikundi chao kinajishughulisha
na mazao ya mapesheni, mananasi, ndimu, maparachichi, mchicha, pilipili boga,
nyanya chungu, ndizi na malimau, ambacho kilianzishwa mwaka 2000.
Katibu wa kikundi hicho Subira Mkubwa Mohamed
alisema, walihama mjini Wete na kwenda kuhamia kijiji cha Kwale Mpona Finya kwa
ajili ya kufanya shughuli za kilimo.
Alisema kuwa, kwa sasa wamepiga hatua nzuri
kwani walianza na robo ekari na sasa wana ekari sita na nusu, ambapo ekari nne
na nusu zimejaa mazao mbali mbali.
Alisema malengo yao, ni kuhakikisha
wanazalisha zaidi ili kujinufaisha wao na kuongeza ajira kwa vijana katika
kijiji na familia zao.
Akizungumzia soko kiongozi huyo alisema ni zuri,
isipokuwa kama ilivyo kawaida bei ya mazao siku za mvua hushuka kwa vile idadi
ya wateja wao ambao huwafuata shambani nayo hupungua.
Alisema kuwa, changamoto inayowakabili ni
kukosa mtaji kwani wanataka wazalishe zaidi, lakini wanashindwa kutokana na kukosa
fedha za kujiendeleza.
‘’Tumeshaomba mkopo lakini bado hatujapewa,
ingawa tunatumai kwamba tutapata, huu utatusaidia kutatua changamoto
zinazotukabili,’’ alisema mama huyo.
Aliwaomba viongozi wa Serikali wafike kwenye
shamba lao kukagua shughuli zao na kuona jinsi walivyoimarisha, ili wapatiwe
mkopo utaowasaidia kujiendeleza.
Kaimu Mratibu Wakala wa Uwezeshaji Wananchi
Kiuchumi Pemba Haji Mohamed Haji alisema, ombi la mkopo la wakulima wa mboga na
matunda Kwale Mpona lipo katika utaratibu na baada ya kumaliza watapatiwa.
"Mkopo watapewa, lakini maombi ni mengi
na wao wakati wanapeleka waliwakuta wenzao, hivyo mpaka wapewe aliowakuta ndipo
na yeya apewe,’’ alieleza.
Aliwataka wanakikundi hao kuwa wavumilivu
kwani itakapofika zamu yao watapewa, kwa sababu wao ni walipaji wazuri na wala
hawana matatizo yeyote katika urejeshaji wa fedha.
MWISHO.
Comments
Post a Comment