NA FAKI MJAKA, AMM -ZANZIBAR@@@@
Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora
Mh. Haroun Ali Suleiman amesema kuanzishwa kwa Sheria ya Usuluhishi na Kituo
cha Utatuzi wa Migogoro Zanzibar kutaongeza imani ya wawekezaji kuja nchini
kuwekeza miradi yao ya kimaendeleo.
Amesema kituo hicho kitakapoanzishwa kitawahudumia wenyeji na wageni na
hivyo kupunguza kasi ya watu kuepelekana mahkamani hasa pale migogoro ya
kibiashara na uwekezaji inapotokea.
Waziri Haroun aliyasema hayo huko katika ukumbi wa Golden Tulip Uwanja
wa Ndege alipofungua Mkutano wa Wadau uliojadili Rasimu za Miswada ya Sheria ya
Usuluhishi na Sheria ya kuanzisha Kituo cha Usuluhishi wa Migogoro Zanzibar
uliohudhuriwa na wadau kutoka sekta mbali mbali nchini.
Alisema hali ya Zanzibar kiuchumi inaimarika sana kutokana na juhudi
zinazochukuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.
Hussein Ali Mwinyi za kuwavutia Wawekezaji kuwekeza miradi yao ya kiuchumi
Zanzibar.
Alisema suala la uwekezaji linahitaji pia kuwa na sheria nzuri ili
kuwavutia wengi zaidi kuja kuwekeza nchini na kuleta tija kwa wananchi na taifa
kwa ujumla.
Alifahamisha kuwa, waligundua kwama, Sheria iliyopo kwa sasa ya utatuzi
wa migogoro imepitwa na wakati na hupelekea migogoro mingi ambayo huchukua muda
mrefu na gharama kubwa mahkamani.
Alisema Serikali kwa makusudi imeamua kuanzisha Kituo maalum cha
usuluhishi wa migogoro ambacho kitakuwa na jukumu la kuipatia ufumbuzi migogoro
itakayojitokeza.
“Badala watu kupelekana Mahkamani panapotokea mgogoro sasa watu watakuwa
wanaenda katika kituo hicho kwa ajili ya kutafuta suluhu, na imani yetu
watakaokwenda kituoni watatoka hapo kila upande ukiwa umeridhika” Alifafanua
Waziri Haroun.
Aliongeza kuwa, Kituo hicho kitakuwa chini ya Mwenyekiti wake
(atakayeteuliwa na Rais), ambaye pia atakuwa na jukumu la kutumia busara kwa
kushirikiana na Wajumbe wake kuitatua migogoro itakayofikishwa katika kituo
hicho.
“Ukweli ni kwamba Wawekezaji hupenda mazingira salama ya uwekejazi wao.
Wanapopelekwa mahkamani, huvunjika moyo na kutafuta nchi nyingine zenye
mazingira rafiki ya uwekezaji wao, ili yasifikie hayo Kituo hiki kitakuwa
kichocheo cha kuwaongezea Imani na usalama wao” Aliongeza Waziri Haroun.
Akitoa historia ya chimbuko la uwamuzi huo, Waziri Haroun alisema, Rais
Dkt. Mwinyi baada ya kuingia madarakani aliagiza sheria zote zilizopitwa na
wakati zifanyiwe marekisho au kufutwa na kutungwa upya. Miongoni mwa Sheria
hizo ni sheria ya usuluhishi ambayo ilitungwa toka zama za wakoloni mwaka 1926
hivyo ni wajibu kufutwa ili kuendana na hali halisi ya sasa.
Akizungumza katika Mkutano huo, Mwanasheria Mkuu Zanzibar Dkt. Mwinyi
Talib Haji alisema ni muda muafaka wa Zanzibar kuwa na kituo chake cha
usuluhishi wa migogoro hasa kutokana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Nane ya
kushajihisha Uchumi wa Buluu na uwekezaji wake.
Alisema Rasimu mbili zilizokuwa zinajadiliwa zitatoa Dira muhimu na
mustakabi mwema wa Zanzibar ambapo shughuli za uwekezaji zitakapoongezeka,
zitawanufaisha wananchi kwa ujumla wake.
Alifahamisha kuwa, kiutaratibu Rasimu hiyo itapelekwa katika kamati ya
uongozi ya Wizara na baadaye kikao cha Makatibu wakuu kabla ya kupelekwa Baraza
la Wawakilishi kwa hatua za kujadiliwa zaidi.
Amesema kukamilika kwa Sheria na Kituo hicho cha usuluhishi kutachochea
imani zaidi kwa wawekezaji kwamba Zanzibar ni sehemu nzuri ya uwekezaji na
hivyo kupelekea kutekeleza dhamira ya Dkt. Hussein Ali Mwinyi ya kuifungua
Zanzibar kiuwekezaji hasa katika uchumi wa Buluu.
Akichangia katika mkutano huo, Mwenyekiti mstaafu wa tume ya kurekebisha
sheria Zanzibar ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka
ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Jaji Mshibe Ali Bakari amesema moja ya faida ya
Kituo hicho ni kuipunguzia mzigo mkubwa Mahkama kwani migogoro mingi itapatiwa
ufumbuzi katika kituo hicho badala ya mahkamani.
Kwa upande wake Rais mtaafu wa Jumuiya ya Mawakili Zanzibar na Wakili wa
kujitegemea Slim said Abdala amesema uzoefu unaoenesha kuwa migogoro ya
kibiashara na uwekezaji haitakiwi kwenda katika Mahkama za kawaida, bali
hupelekwa katika Vituo vya usuluhishi.
Amesema Kituo cha usuluhishi ni sehemu muafaka zaidi kwa vile ni maamuzi
hutolewa kwa haraka zaidi na kwa ufanisi bila kuvutana katika mahkama
kunakochukua muda mrefu na gharama kubwa.
Wakili Slim aliahidi kuwa wapo tayari kuunga mkono kituo hicho ambacho
ana Imani kitazidi kuchochea kasi ya uwekezaji na maendeleo nchi.
mwisho
Comments
Post a Comment