NA ZUHURA JUMA, PEMBA
LICHA
ya elimu ya uzazi wa mpango inayotolewa kwenye vituo vya afya lakini bado kuna
baadhi ya akinababa huwazuia wake zao, jambo ambalo linaweza kusababisha athari
kwa mama mwenye matatizo katika mfumo wake wa uzazi.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wananchi wa
shehia ya Shungi Wilaya ya Chake Chake walisema, madaktari wanajitahidi kutoa
elimu kuhusiana na uzazi wa mpango, ingawa kuna baadhi ya wanawake wanaendelea
kupata athari kutokana na kutofuata huduma za uzazi wa mpango.
Walisema kuwa, uzazi wa mpango ni muhimu kwa
wanawake kwani wanapata kupumzika, kuimarika kiafya na kumfanya mtoto akue
vizuri, hivyo ipo haja kwa akina baba kuangalia hali ya afya kwanza, ndipo
wakatae uzazi wa mpango.
‘’Elimu ipo kwa sababu tunapokwenda vituo vya afya
madaktari wanajitahidi kutuelimisha, lakini baadhi ya wanaume wanahisi kama
tunataka kufungwa uzazi, jambo ambalo sio sahihi,’’ walisema wananchi hao.
Mwananchi Fatma Said Khalfan alisema kuwa, kuna
baadhi ya wanawake wanapokuwa wajawazito wanateseka sana kiasi ambacho wanakaribia
kupoteza maisha, ingawa ukimwambia apumzike angalau miaka miwili anakwambia
mume wake hataki.
‘’Mimi naona kabla ya kuwasikiliza waume zetu,
kwanza tujiangalie na sisi afya zetu, je zinaruhusu kuzaa papo kwa papo? kwa
sababu ile adhabu ya maumivu anaeipata ni mwanamke,’’ alisema mama huyo.
Kwa upande wake Massoud Juma Abdalla alieleza kuwa,
uzazi wa mpango ni muhimu, lakini ikiwa mwanamke afya yake inamruhusu kuzaa
papo kwa papo, anatakiwa kuzaa.
‘’Ikiwa mwanamke ana matatizo katika mfumo wake wa
uzazi basi ni vyema kila baada ya kujifungua akapumzika miaka miwili ndipo azae
mwengine ili kuimarisha afya yake,’’ alieleza.
Nae Mohamed Juma Mohamed alisema kuwa, uzazi ya
mpango una faida kwa kulinda afya ya mwanamke, kwani uzazi wa papo kwa papo
unaumiza mama na mtoto kutokana na kuwa hapati kupumzika.
Asha Said alisema, wengine hawatumii uzazi wa
mpango kwa kuhofia kukimbia uzazi wake, kwani wengine wana uzazi mdogo, hivyo
wanapopunzika wanaweza kujikuta wanakosa watoto.
Daktari kutoka kituo cha Afya shehia hiyo Habiba
Omar Mwinyi alisema, wananchi wana elimu ya kutosha kuhusiana na uzazi wa
mpango, kwani mwamko wa kutumia ni mkubwa ukilinganisha na hapo zamani.
‘’Kwa mwezi tunatakiwa tupokee wajawazito 13 lakini
kwa sasa tunapokea idadi ndogo kutokana na wengi wao kutumia uzazi wa mpango,
kitu kinachotuhangaisha ni baadhi ya wanaume kukataa hata kama mke wake ana
matatizo,’’ alifafanua.
Akitaja athari za uzazi wa papo kwa papo Dk. Habiba
alisema, ni mama kutoka damu nyingi wakati wa kujifungua, kukosa muda wa
kumshughulikia mtoto, mtoto kupata utapiamlo au kuzaliwa akiwa njiti.
Shehia ya Shungi Wilaya ya Chake Chake ina wananchi
3,880, wanawake 2,397 na wanaume 1,483 ambapo shughuli zao kubwa ni kilimo,
biashara na uvuvi.
MWISHO.
Comments
Post a Comment