Na Salma Lusangi, Zanzibar:
KATIBU Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar Joseph Kilangi
ameahidi kusitisha mkataba na Kampuni ya Simba Developa inayojenga mradi
wa tangi la kuhifadhia maji safi na salama eneo la Mgeni Haji Wilaya ya
Maghari ‘A’ Unguja, kwa kutoridhishwa na utendaji kazi wa kampuni hiyo.
Aliyasema hayo wakati alipofanya ziara yake ya
kiutendaji ya kukagua miradi hiyo inayotekelezwa na kampuni mbalimbali
ikiwemo kampuni ya Afcon, Simba developa na Shanjo.
Alisema utekelezaji wa kampuni hiyo, haujafikia hata
asilimia 30 ya ufanyaji kazi, hivyo endapo ujenzi huo utaendelea kudorora,
atashauriana na mwasheria wa wizara yake, ili kuandaa utaratibu wa kusitisha
mkataba pamoja na kuwatoza fidia kampuni hiyo.
“Mradi wa ujenzi la tangi ni mradi wa miezi minane,
lakini hadi sasa miezi minne imepita wamechimba shimo na kufunga nondoo chini
basi, hakuna kazi inayoendelea na hatuwezi kuendelea na kampuni hii,’’alieleza.
Alisema hatua ya kukatisha mkataba itafanyika kwa
kampuni zote ambazo zitashindwa kutimiza ahadi kama walivyokubaliana, na kila kampuni
ina muda waliyokubaliana katika kutekeleza mradi.
Alielezea Mradi wa Maji unayotekelezwa na kampuni ya
Afcon kupitia fedha za Benki ya Exim, ambapo ni mkopo nafuu wa dola milioni
92.18 unajukumu la kuchimba visima, kujenga matangi ya kuhifadhia maji, kufukia
maboba pamoja kujenga nyumba ya kuhifadhi Maji (Maji House) unaendelea vizuri.
Naye Meneja Mradi huo, Rashid Mohamed kutoka Mamlaka ya Maji Zanzibar
‘ZAWA’ alisema mradi wa kisima kupitia fedha za ahuweni za UVIKO-19, unajukumu
la kujenga matangi 10 kwa Unguja na Pemba, kuchimaba visima vipya 38 pamoja
kufanya kazi ya kutandika mabomba.
Kwa upande wake Mhandisi Hassan Khamis Hassan kutoka ‘ZAWA’, alisema kisima
cha Bubwisudi, hakina tatizo kimefungwa mashine kubwa ya kusukumia maji,
ila wanahitaji usalama wa mashine hiyo na wameshafanya utaratibu wa kuwaomba
ZECO wasaidie kifaa hicho cha usalama wa mashine (mota).
Mapema Mhadisi wa kampuni ya Simba Develop Hassan Hamad, alisema
utekelezajwi wa mradi wa tangi la maji kupitia kampuni hiyo unatokana na
mshauri elekezi ambapo alifelisha kokoto zilizoagizwa mwanzo kutona na ardhi ya
hapo ina maji maji isingeweza kukidhi vigezo vilivyohitajika lakini tayari wameshaagiza kokoto zinanostahiki na
kuendelea na kazi.
Ziara ya katibu Mkuu Kilangi ni ziara ya siku mbili,
ambapo siku ya kwanza alitembelea Mradi wa maji shehiya ya Masingini, Dimani, Nyumba
ya kuhifadhia maji eneo la Miembeni ( Madema) ambapo shughuli hizo
zinatekelezwa na fedha za Exim Benki. Pia alitembea mradi wa maji Mbuzini
unaotekelezwa kwa fedha za ahuweni za UVIKO-19 na mradi wa ujenzi wa tangi la
kuhifadhia maji Mgeni haji linalojengwa na kampuni ya Simba Developa.
Mwisho.
Comments
Post a Comment