NA ZUHURA JUMA, PEMBA
“KUTOKANA malezi mazuri niliyolelewa na wazazi wangu, baada ya kumaliza skuli
sikujipweteka… nilianza kazi ya kuisaidia jamii na mpaka sasa naendelea”,
…Si maneno ya mtumwengine, bali ni ya Khadija Henock Maziku mkaazi
wa shehia ya Mjiniole ambae kwa sasa ndio Diwani wa Wadi ya Ole, Jimbo la Ole wilaya
ya Chake chake Pemba.
HARAKARI
ZA UONGOZI
Khadija alianza harakati zake za uongonzi tangu mwaka 2007 akiwa
katika Jumuiya ya Wanawake (JUWAKAP).
Kwa wakati huo, ambayo ilishirikiana na Shirika la Action Aid,
akiwa kama Makamu Mwenyekiti kwa wilaya ya Wete na hatimae kuwa Katibu kwa Mkoa
wa Kaskazini Pemba.
Dira ya Jumuiya hiyo ilikuwa ni kumkomboa mwanamke, katika nyanja
zote za kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Kazi yao ni kuhamasisha wanawake kugombea nafasi za uongozi,
ili waondokane na utegemezi huku wakiwa mstari wa mbele kupiga vita vitendo vya
ukatili na udhalilishaji.
Mwaka 2009 walifikiwa na mradi wa WEZA kutoka TAMWA, ambao uliwahamasisha
wanawake kuanzisha vikundi vya kuweka na kukopa, ambapo walichagua viongozi
mbali mbali akiwemo yeye.
Wakati anatoa elimu hiyo kwa wanajamii, alifikisha idadi ya
vikundi 16, alivyovianzisha na kuwafikia wanawake zaidi ya 300.
Lengo lao ni kuwajengea uwezo akinamama, kuaminiana,
kukopeshana na kuwagomboa kisiasa na kiuchumi, ambapo walifanikiwa kwa kiasi.
“Nilikuwa naelimisha wanawake wote bila kuchagua chama,
niliwaambia kuwa, muhimu ni kwa wanawake kugombea uongozi, tuchangamkie fursa
hii”, anaeleza.
Alianza uongozi kwenye Jumuiya, kisha kwenye jamii na sasa
kwenye siasa, ambapo awamu iliyopita alipata nafasi ya Diwani wa kuchaguliwa na
awamu hii pia amefanikiwa kushika nafasi hiyo.
Alijengewa uwezo ni TAMWA kupitia mradi wa WEZA na Action Aid
na amepata mafanikio, na sasa ameingia jimboni kugombea nafasi za uongozi na
amefanikiwa.
“Tunaziomba zijitokeze taasisi za kuwaandaa viongozi bora
wanawake, na sio bora kiongozi, huku zijipange kumboresha kwani wana umuhimu
mkubwa katika kuongoza”, anasema.
Anafafanua kuwa, kuna tofauti kubwa ya uongozi wa mwanamke na
mwanaume, kutokana na wanawake kufanya kazi kwa uaminifu na kwa kujitolea.
Aliandaliwa na kuamua kujitolea, hakuogopa vikwazo vyovyote,
ambavyo vinawakumba baadhi ya wanawake ambao wanagombea nafasi za uongozi.
“Kwa vile nimeamua, sikuogopa chochote na sikukubwa na kikwazo
chochote, hapakuwa na changamoto ambayo ilinifanya niogope,”anaeleza.
Anawaelimisha wanawake wenzake kuhusu mambo mbali mbali ya
kijamii, ikiwa ni pamoja na kuanzisha vikundi vya kuweka na kukopa, vya
ujasiriamali na kuingia majimboni kusaka uongozi.
HARAKATI
ZA KUGOMBEA UDIWANI
Khadija anasema, mwaka 2015 ndio mwaka alioingia wadini, wa wadi ya Ole na kufanikiwa kuibuka mshindi.
“Baada ya kuona kwamba mwaka huo nilifanikiwa kuishika nafasi
hiyo, ilipofika mwaka 2020, niligombea tena nafasi hiyo na nashukuru
nimefanikiwa”, anaaeleza.
Anasema, anajua kwamba wananchi wameendelea kumchagua kutokana
na mambo ya maendeleo aliyoyafanya katika awamu ya kwanza ya uongozi wake wa
udiwani.
MAFANIKIO
Kuna mafanikio makubwa ikiwa wanawake watagombea nafasi za
uongozi kwani ni wasikivu, wenye huruma na kujitolea, hivyo hufanya kazi kwa
bidii.
Kabla hajapata nafasi ya udiwani, jamii ilikuwa haijui kwamba
kuna mfuko wa mwakilishi na mbunge kwenye majimbo, lakini baada ya kupata
nafasi hiyo aliwaeleza wananchi wake.
Anasema, fedha hizo wanaziona kutokana na kazi kubwa
anayoifanya katika wadi yake, kwani anahakikisha changamoto zilizopo wanazitatua
kupitia fedha hizo.
“Zinapoingia fedha za mfuko wa jimbo tunawaita wananchi wetu,
tunawaambia kiasi cha fedha kilichopo, kisha wanaibua changamoto
zinazowakabili”, anaeleza.
Baada ya kuibua changamoto hizo, wanazigawa fedha kwa wadi
mbili na kutatua matatizo hayo, jambo ambalo lilikuwa halifanyiki kwa madiwani
waliopita ambao walikuwa wanaume.
Anafanya maendeleo makubwa katika wadi yake kwa kushirikiana
na Mbunge pamoja na Mwakilishi, ambapo tayari ameshajenga vyoo Mjiniole vyenye
thamani ya shilingi milioni 26.
‘’Tumepeleka maji katika kijiji cha Makaani kupitia mfuko wa Mwakilishi
wenye thamani ya shilingi milioni 12.8 huku akitumia milioni 57 kujenga mabanda
ya skuli, chumba cha walimu na computer, kuezeka, kujaza kifusi barabara ya
Mbuyuni na Shumindu’’, anaeleleza.
Alisambaza nguzo 12 za umeme kwenye vijiji tofauti pamoja na
kupeleka maji katika kijiji cha Markaz Kianga, ambapo huduma ya maji alitumia
kiasi cha shilingi milioni 7.
Anasimamia majukumu yake kuhakikisha haki zinapatikana, kwani
fedha hizo ni kodi za wananchi.
Anafahamisha, yeye hawezi kufanya jambo kwa maslahi yake
binafsi kama wengine waliopita, anajitolea kwa moyo wa imani katika kupeleka
mbele gurudumu la maendeleo.
Khadija anaeleza kuwa, wananchi katika wadi yake wanampa
mashirikiano makubwa kwa sababu tangu zamani alikuwa na sifa kubwa kutokana na
kuwasaidia katika kutatua changamoto mbali mbali.
Mbali na nafasi ya udiwani aliyonayo pia ni mratibu wa
wanawake na watoto wa shehia ya Mjiniole, hivyo alikuwa akiibua changamoto
zinazowakumba wanawake na watoto na kuzisimamia mpaka wanapata haki zao.
“Tangu mwanzo nilijichanganya na wananchi na kuwasaidia katika
kutetea haki zao za msingi na watuhumiwa kupata hatia, hivyo waliniamini na
naendelea kuwasaidia”, anaeleza.
CHAGAMOTO
ZINAZOWAKUMBA WANAWAKE KUGOMBEA
Mfumo dume ndio unaorejesha nyuma juhudi za wanawake wenye nia
ya kugombea nafasi za uongozi ikiwa hawakujikaza, mwaminifu na kusimamia
anachokiamini.
“Wengine wanakosa ujasiri, kutokuaminiwa kwenye vyama vyao na
kuonekana mwanamme ndie anaeweza kuongoza, na hata akipatiwa nafasi na chama
chake, atakuwa ni mtu wa kupangiwa tu na kufuata maelekezo wanayoyataka”,
anafafanua.
Lakini ni tofauti na kiongozi yeye ambae alijiandaa, kujiamini
na kuwa na uthubutu katika kuwasimamia wanawake wenzake na wananchi kwa ujumla.
Diwani huyo anasema, ikiwa wanawake wataendelea kubaki nyuma
katika kugombea nafasi za uongozi, watashindwa kusimamia maamuzi yao huku
wakiendelea kuwa tegemezi.
“Umasikini utatutawala na wanaume watazidi kutumiliki na kutufanyia
mambo yasiyostahiki, tuungane mkono pamoja, tusaidiane na lazima tusimamie
hili”, anaeleza.
NINI
KIFANYIKE
Khadija anawataka wanawake wenzake kufanya kazi kwa bidii,
kujitambua na kuwaunga mkono wale ambao wamebahatika kuingia katika nafasi za
uongozi.
HISTORIA
YA KHADIJA
Ameolewa mwaka 1984 na amefanikiwa kupata watoto nane (8),
wanawake watatu (3) na wanaume watano (5) na kupata elimu yake ya msingi katika
skuli ya Kizimbani Wete hadi kidato cha pili.
Alipata elimu yake ya kidato cha tatu katika skuli ya Sekondari
Utaani Wete na baada ya kumaliza hakuendelea na masomo ya elimu ya juu na
hatimae kuolewa.
“Kwa vile nilipata mafunzo mazuri kwetu sikujipweteka,
nilipoolewa tu nilianza harakati za huku na kule na nilijiunga katika Jumuiya
ya Wanawake Mkoa wa Kaskazini Pemba”, anafafanua.
Khadija pia alikuwa kiongozi kwa kada mbali mbali katika jamii
ikiwa ni pamoja na katika vikundi vya ushirika na mratibu wa wanawake na watoto
shehia ya Mjiniole.
Mume wa Khadija, Mustafa Khamis Bakar anasema mke wake amekuwa
mpambanaji kwa wanawake wenzake na watoto kuhakikisha wanapata haki zao.
‘’Nampa mashirikiano makubwa mke wangu kwa sababu
anachokifanya ni kizuri sana kwa maslahi ya jamii na Taifa, amekuwa maarufu na
ndipo akafanikiwa kupata nafasi ya udiwani’’, anaeleza.
Anaeleza kwa, mke wake anajiamini na hakuwahi kukatishwa tamaa
na maneno ya watu na aliendelea kupambana kila hatua kuhakikisha jamii yake
inakuwa salama.
Awena Salim Kombo ambae ni mratibu wa Wanawake na watoto
shehia ya Kangagani anamfahamu Khadija kwamba ni mwanamke mpambanaji ambae
anafanya kazi ya kujitolea kwa jamii yake.
Khadija anafanya kazi ambazo madiwani waliotangulia hawakuzifanya,
kwani amekuwa akiwaita wananchi na kuibua changamoto zinazowakabili katika
jamii yao na zinapoingizwa fedha za mfuko wa jimbo huzitumia kutatulia changamoto
hizo.
“Madiwani waliopita kwa kweli ilikuwa hawafanyi mambo ya
kimaendeleo, lakini Khadija kama ameizindua jamii yake, kwa sababu anafanya
kazi kubwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki”, anaeleza.
Fatma Ali mkaazi wa shehia hiyo anamkumbuka diwani huyo kuwa
ni mwanamke ambae anaisaidia jamii yake kwa hali na mali na ndio maana wananchi
wapo karibu na yeye.
“Namkumbuka tangu alipokuwa akielimisha wananchi kuhusiana na
mambo ya ujasiriamali, kuelimilisha mambo ya udhalilishaji na ukatili wa
kijinsia, hivyo juhudi zake anazitumia na saivi alipopata nafasi ya udiwani”,
anasema.
Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa Said anasema, juhudi zao
za kuelimisha wanawake kugombea nafasi za uongozi zimeanza kuzaa matunda kwani,
mwaka 2020 walijitokeza wengi majimboni mwao kuchukua fomu.
Anawataka wanawake kufuata mfumo wa Khadija katika kuiletea
maendeleo jamii yake, ili wazidi kuaminika na kupewa uongozi, jambo ambalo
litawafanya wawepo wengi kwenye vyombo vya kutoa maamuzi.
MWISHO.
Comments
Post a Comment