NA ZUHURA
JUMA, PEMBA::::
UZAZI ni
sehemu ya maisha ya mwanadamu.
Ambapo mwanaume hutoa mbegu na mwanamke hupokea, ndipo hapo
anapopatikana mtoto, awe wa kiume ama wa kike.
Kila mmoja anapokuwa na mweza wake, mwisho wa siku
wanatumainia watoto na hapo furaha huzidi kutawala ndani ya nyumba na familia
kwa ujumla.
Pamoja na kwamba kila mmoja anahitaji watoto katika maisha
yake, lakini ni muhumu sana kufuata utaratibu mzuri kwa lengo la kuimarisha afya
ya mtoto na mama.
Hii humfanya kuweka hali bora ya kiafya, katika mwili na
kuimarisha fuko lake la uzazi kwa kujitayarisha kubeba tena mimba nyengine.
Wapo baadhi ya akinamama hufurahia sana kuzaa papo kwa papo,
kwa kile wanachodai kuwa, wamalize haraka na baadae wapumzike bila kujali
usalama wa afya zao.
Wafahamu kuwa, kutumia uzazi wa mpango kwa akinamama ni muhimu
sana katika kuimarisha afya zao, kwani dini ya kiislamu, imehimiza mtoto kunyonyeshwa
miaka miwili.
Qur-an tukufu katika Suratul-Baqarah aya ya 233 imeeleza kuwa
‘Wazazi wa kike wanyonyeshe watoto wao miaka miwili, kwa mwenye kutaka kutimiza
kunyonyesha…’
Hiyo inaonesha wazi kwamba, kuachisha mtoto kwa miaka miwili
ni muhimu sana kwa akinamama kutokana na faida inayopatikana ndani yake.
HALI
IKOJE KWA AKINAMAMA WENYE VVU?
Akinamama wanaoishi na Virusi vya Ukimwi, wanahitaji mapumziko
baada ya kujifungua, ili apate kuimarika kiafya pamoja na mtoto wake.
Huku akifuata maelekezo ya daktari wakati gani kwake anaweza
kubeba mimba.
Dk, Rahila Salim Omar ambae ni msimamizi wa vituo vya kutoa
huduma kwa watu wenye ‘VVU’ anasema, mwili unapotoa kiumbe, unahitaji
kujirejesha tena katika hali ya kawaida na ndipo uweze kubeba mimba nyengine.
Wakati wa ujauzito, kinga ya mwili inashuka, kwa hiyo
uwezekano wa kupata maambukizi mengine unakuwa ni mkubwa zaidi yeye ama mtoto.
Anafahamisha, afya inakuwa bado haijarudi katika hali yake ya
kawaida, hivyo virusi vinaweza kupanda kwa vile kinga yake imeshuka na hatimae kumuambukiza
mtoto.
“Hata kama mama mwenye ‘VVU’ tumempima jana, basi akija leo
ikiwa tumemgundua na ujauzito, tunampima tena wingi wa virusi, je idadi
haijaongezeka?”, anaelezea.
Na ikiwa virusi vimeongezeka, wanampa huduma ya ziada kuweza
kumkinga mtoto na maambukizi hayo, ambapo wanampima kila baada ya miezi mitatu,
mpaka pale atakapoachisha.
“Kile ndio kipindi ambacho anaweza kumuambukiza mtoto, ama
wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua au wakati wa kunyonyesha, ikiwa
atakuwa na maradhi au vidonda mdomoni”, anafahamisha.
Wanapendekeza kwamba, baada ya mama kujifungua, akae miaka
miwili, ili mwili ujirudi na afya iwe nzuri, ndipo abebe mimba nyengine.
Dk, Rahila anawashauri akinamama hao kabla ya kubeba ujauzito,
wafike hospitali, ili wafanyiwe uchunguzi kwamba je, anaweza kubeba mimba
nyengine au kinyume chake.
“Wengine wanatwambia na wengine tunakuja kugundua tayari
wameshabeba mimba, lakini tunatakiwa tuwapime wingi wa virusi, ikiwa ni kidogo
ndipo tuwaruhusu kubeba mimba”, anaeleza.
Pamoja na ushauri wanaoutoa kwa akinamama hao, bado kuna
baadhi yao wana usiri mkubwa, jambo ambalo linaweza kusababisha maambukizi kwa
mtoto, anaezaliwa na yule wa nyuma yake ambae hakuachishwa.
Anasema, wanawafuatilia kwa umakini na wapo vizuri kwenye
huduma za mama wajawazito, wanaoishi na VVU, hivyo wanashukuru kwani ni
asilimia ndogo sana ya watoto wanaozaliwa na VVU.
Na hiyo ni kwa sababu baadhi ya akinamama hao hawafuati
maelekezo ya daktari na kutotumia dawa za ARV kwa usahihi.
Dk. Rahila anasema, ikiwa mama ana VVU anaweza kumuambukiza
mtoto wake hasa, ikiwa hakutumia vizuri dawa za ‘ARV’ ambazo zinapunguza idadi
ya virusi mwilini.
Kuanzia mwaka 2020 hadi Machi mwaka huu ni watoto wawili tu
ambao wameambukizwa VVU na mama zao baada ya kuzaliwa, kati ya vipimo 102 vilivyopimwa
kisiwani Pemba.
‘’Vipimo vyetu tunafanya pale mtoto anapofikisha wiki sita
baada ya kuzaliwa, miezi tisa na mwaka mmoja na nusu, hivyo tuligundua watoto
wawili tu wameambukizwa’’, anasema.
Anaeleza, sababu ya kuambukizwa watoto hao ni kutokana na mama
zao kutohudhuria vizuri kliniki na kutofuata hatua zinazotakiwa, ikiwa ni
pamoja na kutotumia dawa vizuri.
Dk, Khamis Hamad ambae Msaidizi Meneja Kitengo Shirikishi cha
Ukimwi, Kifua kikuu, Homa ya ini na Ukoma, anaeleza, kuwa mama mjamzito ambae
anaishi VVU anahitaji zaidi kuzaa kwa mpango.
“Ingawa wajawazito wote kinga yao hupungua, lakini hawa
wanaoishi na VVU inapungua zaidi, hivyo anatakiwa apangiwe muda wa kuzaa
kulingana na idadi ya virusi alivyonavyo”, anasema.
Kutokana na mimba za papo kwa papo, mwili unakuwa hauwezi
kujirudi na unakuwa dhaifu, hivyo mama atakuwa hana mda wa kumshughulikia mtoto
alienae, kwa malezi na hata mfumo wa kula.
Mtoto anatakiwa anyonye maziwa ya mama kwa miezi sita bila
kumchanganyia chochote, lakini ikiwa mama atabeba mimba nyengine kabla ya
wakati unaotakiwa, atamkosema mawanwe haki zinazostahiki.
“Ikiwa ndani ya miezi sita unabeba mimba, unaanza kumkosesha
haki ya kumnyonyesha huyu mtoto ulienae, unakosa mda wa kujiandaa kiuchumi na
kimwili”, anaeleza.
Hivyo anaanza kuchanganya vyakula huku anaendelea kumnyonyesha,
hatima yake ikiwa ziwa la mama lina vidonda na mtoto akiwa ana michubuko mdomboni
anamuambukiza.
MAMA
WENYE VVU
Maryam Salum mkaazi wa Mabaoni Chake chake, anaeishi na VVU alishawahi
kupata elimu kupitia wataalamu wa afya, na sasa amekuwa akifika kliniki, kila
anapotaka kubeba ujauzito.
“Najitahidi kufuata ushauri wa daktari, ili kumkinga mtoto
wangu dhidi ya maambukizi, kwa sababu unapotaka kubeba mimba unapewa maelekezo
na ni vizuri uyafuate”, anafahamisha.
Maryam, baada ya kubeba mimba anatakiwa kutumia dawa vizuri na
chakula kizuri kwa lengo la kujenga afya yake na mtoto.
Lengo ni kumkinga mtoto asipate maambukizi ya VVU, na kuongeza
idadi ya watu wanaoishi na maambukizi mapya.
Maryam ameolea na mume ambae hana maambukizi, ambapo amezaa
mtoto, ambae hana maambukizi na kwa sasa ana miezi tisa anaendelea kumnyonyesha.
‘’Kuna faida kubwa kwa mama mwenye ‘VVU’ kuachisha, kwa sababu
afya yake sio nzuri, ukilinganisha ya akinamama wasio na VVU’’, anaeleza.
Anatakiwa kulinda afya yake na hatakiwi kuzaa mtoto mwengine
hadi pale afya yake, itakapoimarika, kwani ikiwa afya yake sio nzuri kuna
uwezekano mkubwa wa kumuambukiza mtoto.
Maryam Said Abdalla mkaazi wa Chake Chake mbae anaishi na VVU,
anasema kuna umuhimu mkubwa kwa mama mwenye VVU kutumia uzazi wa mpango hasa
kwa vile kinga zao ni tofauti na akinamama wasio na virusi vya Ukimwi.
“Kinga yetu ikishuka zaidi, lile fuko la uzazi linaweza kubeba
maambukizi na likamsababishia mtoto maambukizi hayo”, anasema Maryam ambae pia
ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya watu wanaoisha na VVU Wilaya ya Chake Chake.
Na ndio maana hata kama mama hana maambukizi anatakiwa kuzaa
kwa kiasi, kwa sababu atakapomnyonyesha mtoto kwa miaka miwili na kupumzika
mwaka mmoja, analifanya fuko la uzazi kurudi pale pale kwenye sehemu yake.
“Hapo kinga yako inakuwa nzuri na damu haipotei, kwani mwenye
maambukizi yuko katika hatari ya kubeba maambukizi mengine kutokana na kinga
yake kushuka”, anasema.
Ni mwaka wa 16 anaishi na virusi vya ukimwi ingawa anazaa kwa
mpango na kufuata ushauri wa daktari kwani ndie anaejua kwamba, virusi
alivyonavyo ana uwezo wa kubeba mimba au apate muda zaidi wa kupumzika.
Anasema, hawajapokea kesi ambayo ilitokea kwa sababu mama
hakutumia uzazi wa mpango, isipokuwa zinazotokea ni zile ambazo hahudhurii
kliniki vizuri na kutotumia dawa.
TUME YA
UKIMWI
Ali Mbarouk Omar ambae ni Kaimu Mratibu Tume ya Ukimwi Pemba
anasema, ikiwa mama mwenye VVU atazaa papo kwa papo, anapata athari kwa sababu
ya kupungua kinga yake ya mwili.
‘’Na kinga ya mwili ikipungua inasababisha kupata magojwa nyemelezi
na mtoto anakuwa katika hatari ya kuambukizwa VVU kwa sababu mama hana kinga ya
kutosha”, anasema.
NINI
KIFANYIKE
Maryam Said Abdalla anawataka akinamama wanaoishi na VVU wafike
kwenye kliniki zao ili wafahamishwe jinsi ya kubeba ujauzito kwa ajili ya
kumkinga mtoto asipate maambukizi.
“Unapangiwa muda ambao ni stahiki kwako kubeba mimba na pia
unapata muda wa kuwashughulikia watoto huku ukiwa na afya bora na nguvu nzuri’’,
anaeleza.
Ali Mbarouk Omar ambae ni Mratibu wa Tume ya Ukimwi Pemba
anawataka akinamama hao kutumia njia za uzazi wa mpango kuhakikisha wanapata
muda wa kupumzika, ili mwili ujirudi katika hali nzuri.
Anasema, ipo haja ya kufuata ushauri wa daktari mara kwa mara,
jambo hilo litasaidia kumkinga mtoto na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
MIKAKATI
ILIYOWEKWA KUHAKIKISHA WATOTO WANAZALIWA NA KUKUA SALAMA
Dk, Khamis anaeleza, mikakati ya kitengo ni kuhakikisha kila
mama mjamzito ambae anaishi na VVU anatumia dawa za ARV kwa usahihi, ambazo
zipo vituo vikubwa vinne vilivyopo kisiwani Pemba.
Wanapewa elimu pamoja na wenza wao, ili ikiwa na yeye ana
virusi aweze kutumia dawa kwa sababu, ikiwa mama anatumia dawa lakini mume
hatumii, anamuongezea virusi na inasababisha mtoto kupata maambukizi.
“Yeye itakuwa anatumia dawa lakini mume wake anamuongezea
mzigo kila siku, hivyo wote ni vyema wakatumia dawa ili kumnusuru mtoto asipate
maambukizi”, anaeleza daktari huyo.
Anafahamisha, wanawafuatilia vya kutosha wanaoishi na virusi
vya ukimwi katika kuhakikisha wanatumia dawa kwa usahihi.
Uzazi wa mpango ni muhimu kwa mama mwenye VVU kwani inampa
nafasi ya kurudisha afya yake katika hali nzuri na kupata nafasi ya kumuhudumia
mtoto wake vizuri, ili asipate maambukizi.
MWISHO.
Comments
Post a Comment