NA HAJI
NASSOR, PEMBA
WADAU wa ujenzi
wa amani kisiwani Pemba, wamesema kama haki itatendeka katika sekta kadhaa
zilizopo Zanzibar, suala la uvunjifu wa amani, litabaki kwenye vitabu vya kumbu
kumbu pekee.
Walisema, bado kuna tasisi ndani ya serikali zimekuwa
zikisababisha uvujifu wa amani, kwa kule kutotenda haki ipasavyo, wakati
wanapowahudumia wananchi.
Wakizungumza kwenye kongamano la amani na mashirikiano
lililoandaliwa na tasisi ya Search for Common Ground ikiwa ni
sehemu ya utekelezaji wa mradi wa ‘dumisha
amani Zanzibar’ na kufanyika ukumbi Greef Foullege Chake chake Pemba,
walisema msingi wa amani ni haki.
Walieleza kuwa, kazi inayofanywa na ‘SCG’ kwa kushirikiana na ‘the foundation for Civil Society’
kwa ufadhili wa Umoja wa nchi za Ulaya ‘EU’
ni nzuri, ingawa sasa kazi iliyobakia kwa watendaji ni kutekeleza haki.
Mmoja kati ya wadau hao, kutoka Jumuiya ya Maimamu Zanzibar ‘JUMAZA’
Yussuf Ramadhan Abdalla, alisema uvunjifu wa amani hujitokeza baada ya mwenye
haki kukoseshwa na kupewa mtu mwengine.
‘’Wenzetu wa Search, wamekuja na mradi mzruri mno wa kutuamsha
juu ya kuidumisha amani iliyopo, sasa ni kazi kwa wasimamizi wa haki, kuitekeleza,’’alisema.
Nae mdau Tatu Abdalla Msellem, alisema sio kweli kuwa uvunjifu
wa amani Zanzibar, husababishwa na uchaguzi pekee, bali zipo changamoto
nyingine kama migogoro ya ardhi, ndoa na udhalilishaji, hupelekea kukosekana kwa
amani.
Kwa upande wake mjumbe kutoka chama cha Ualbino Pemba
Mudathiri Khamis Sharif, alisema suala la amani linafaa kuchungwa na kila
mmoja, kwani athari yake, huwakumba zaidi wanawake, wazee, watoto na wenye
ulemavu.
Nae Suleiman Juma Suleiman na Salim Hamad Simba, walisema
vyombo vya habari, visipotumika vyema, vinaweza kuwa chanzo cha uvujifu wa
amani.
Akizungumza kwenye kongamano hilo, Afisa Mawasiliano kutoka Search
for Common Ground Zanzibar, Khelef Nassor Rashid , alisema ujio wa mradi
huo, ni kuona Zanzibar kuna kuwa na amani endelevu.
‘’Mradi huu ambao tuliuzindua tokea mwaka jana, na kutarajia
kuutia nanga mwishoni wa mwaka huu, ni kuhakikisha wanasiasa, viongozi wa dini,
waandishi wa habari na jamii inaendelea kuelimisha faida za ujenzi wa amani,’’alieleza.
Akifungua kongamano hilo, Afisa Mdhamini wizara ya Nchi, Afisi
ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Pemba,
Thabit Othman Abdalla, alisema mradi huo, umekuwa msaada mkubwa kwa serikali
kuu.
Alisema, viongozi wote wamekuwa wakisisitiza kudumisha amani,
na ndio vivyo hivyo tasisi ya search kwa kushirikiana na the foundation, wameibua
mradi huo kwa wakati mwafaka.
‘’Zanzibar kwa sasa inaendeshwa kwa mfumo wa serikali ya Umoja
wa Kitaifa, ambapo suala la amani ni jambo la mwanzo, na huku tasisi hizi
zinakuja na mradi huu, ni jambo jema kwetu,’’alieleza.
Mapema akiwasilisha mada ya vyombo vya habari na ujenzi wa
amani, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya waandishi wa habari Pemba, ‘PPC’ Ali Mbarou Omar,
alisema mradi huo umesaidia kuifikia jamii, katika nyanja mbali mbali.
‘’Tulitengeneza vipindi, uandishi wa habari za kawaida, makala
na hata kuwatumia wasanii kufikisha ujumbe wa amani kwa jamii, hili tunaona
tumefanikiwa,’’alifafanua.
Wakati huo huo Afisa program kutoka ‘the foundation for Civil
Society’ ya Tanzania bara Eveline Mchau, alisema kila mmoja anayonafasi ya
kuchagiza na kufanya uchechemuzi wa ujenzi wa amani.
‘’Tunatarajia hata mradi huu ukimalizika mwishoni mwa mwaka
2022, basi wadau nyinyi na wengine, tuone mnaendeleza wajibu wenu wa kudumisha
amani, katika maeneo yenu,’’alifafanua.
Mwisho
Comments
Post a Comment