|
KUANZIA mwaka 1983 hadi 1992, hatua zilichukuliwa, ikiwani pamoja na
maamuzi ya mwisho ya Umoja wa Mataifa, kuitangaza Disemba 3 ya kila mwaka, kuwa
siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu.
Siku hiyo, pamoja na mambo mengine, kundi la watu
wenye ulemavu hujadili, mafanikio na changamoto zao, zikiwemo za huduma za
afya.
Kisha serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, iliunda Mkakati wa Kitaifa wa Ujumuishi wa mwaka 2010 hadi 2015, na sera
ya taifa ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2004, ukitaja ulazima wa huduma za afya
kwa watu wenye ulemavu.
Ipo sera ya kitaifa ya watu wenye ulemavu
ya mwaka 2018 kwa upande wa Zanzibar, ambayo Ibara ya 20, inasisitiza uimarishwaji
wa upatikanaji huduma bora na endelevu kwa kundi hilo.
Serikali ilitunga sheria ya Watu wenye
Ulemavu ya mwaka 2010, ambapo ilikuja kuharakisha huduma bora na endelevu za
afya kwao.
Kwa Zanzibar, ilikuwa na sheria ya watu
wenye ulemavu, nambari 9 ya mwaka 2006, ambayo imefutwa na sasa kuwa na sheria
mpya nambari 8 ya mwaka 2022.
Kifungu cha 28 (1) (c) cha sheria hiyo, kimeainisha
haki ya kupata huduma na elimu ya afya, kwa watu wenye ulemavu, ikiwemo
matibabu, matengenezo au marekebisho yanayohusiana na aina ya ulemavu wao.
Kulikuwa na Mpango Mkakati wa sekta ya afya
wa miaka tisa, ambao uliishia mwaka 2019, nao ulitaja hatua za kuchukuliwa, ili
kuwakinga na utapiamlo wanawake, watoto na watu wenye ulemavu.
Kimataifa, upo Mkataba wa haki za watu
wenye ulemavu, ambao Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliusaini mwaka
2007, na kuthibithisha mwaka 2009, ambao unalazimisha huduma za afya, kwa watu
wenye ulemavu.
Ibara ya 25, inasisitiza nchi wanawachama, zitumbue kuwa, watu wenye ulemavu, wanayo haki ya kunufaika kwa
kiwango cha juu, cha huduma na elimu ya afya.
‘’Nchi wanachama zitatoa huduma za afya,
zinazohitajika kwa watu wenye ulemavu, hasa kutokana na aina ya ulemavu wao, yakiwemo
maeneo ya vijijini,’’umefafanua.
Ukaongeza kuwa,
nchi hizo zitawataka wataalamu wa afya, kutoa huduma za kiwango sawa, kwa watu
wenye ulemavu, kama wengine.
HALI IKOJE KWA VIZIWI NA ELIMU YA AFYA YA UZAZI?
Omar Haji Omar wa Mtambile wilaya ya Mkoani
mwenye watoto sita, akizungumza na wandishi wa makala hii, chini ya mkalimani
wake, anasema hajapata elimu ya afya ya uzazi kwa aina ya miundombinu yake.
‘’Mimi nishahudhuria kliniki mara tatu,
lakini sijawahi kupata elimu ya afya uzazi, hasa kwa aina yangu ya ulemavu,’’anasema.
Khamis
Massoud Khamis mwenye watoto wawili, mkaazi wa Kilamatinde anasema, hata yeye
na mke wake wameshahudhuria klikini mara mbili, lakini hawapati elimu ya afya
ya uzazi.
‘’Mara ya kwanza, nilipokwenda tunawasiliana
na daktari kwa njia ya maandishi, mpaka nikifahamu, lakini kwa kutumia
mkalimani sijawahi,’’anasema.
Mkewake Khamisi, Aisha Muhidin Kombo,
anasema njia anayotumia kupata elimu ya afya ya uzazi ni kujisomea vipeperushi,
lakini sio kupitia madaktari.
‘’Ni kweli mimi nimezaa mtoto kila baada ya
miaka mitatu, lakini elimu hii ni ya mazoea tu, sio kama nimefundishwa na
madaktari,’’anasema.
Fatma Juma Mohamed (50) mwenye watoto 10,
mkaazi wa Mchanga mdogo Wete, anasema mimba moja baada ya kuonekana na tatizo,
alikwenda hospitali na mkalimani.
Maimuna Issa Haji na mwenzake Husna Kombo
Omar wa Micheweni wanasema, wanapokwenda kliniki, hakuna mkalimani wa lugha ya
alama na kukosa taarifa sahihi za afya ya uzazi.
‘’Natamani hasa nipate elimu ya afya ya
uzazi kwa kina, ili nijue mambo kadhaa, lakini inakuwa vigumu maana, wale ni
wataalamu wa afya tu, sio wa lugha ya alama,’’anasema.
Mkalimani wa lugha ya alama Pemba Asha
Suleiman, anasema hajawahi kualikwa na wizara ya Afya, ili kuwa makalimani
wakati elimu ya afya uzazi ikisomeshwa.
Mwenyeikiti wa Chama cha Viziwi wilaya ya
Chake chake Mohamed Khamis Shehe, anasema hakuna hata mkutano mmoja wao peke
yao, waliowahi kualikwa wa utoaji elimu ya afya ya uzazi.
Mjumbe wa Umoja wa Watu wenye Ulemavu
Zanzibar, Hidaya Mjaka Ali, anakiri kuwa, elimu ya afya ya uzazi bado ni
changamoto kwao.
‘’Ni kweli wizara ya Afya, imeyafikia
makundi yote, lakini kwa wenzetu wenye uziwi kwa mkutano wao peke yao, hilo
halijafanyika,’’anasema.
Mratibu wa Baraza la Taifa la watu wenye
Ulemavu Zanzibar ofisi ya Pemba, Mashavu Juma Mabrouk, anakiri kuwa wizara ya
Afya, haijawahi kuliita kundi la watu wenye uziwi, kuwapa elimu hiyo.
‘’Mbinu tunayoitumia kwa watu wenye uziwi,
ili wafikiwe na elimu ya afya ya uzazi, ni kuwatumia maafisa wa Baraza, ambao
wameshapata elimu na kukutana na viziwi,’’anasema.
Changamoto inayojitokeza kuwa ni uwepo wa
viziwi zaidi ya 400 kisiwani Pemba, ingawa yupo mkalimani mmoja anayetambulika
rasmi.
Muhudumu wa afya shehia ya Kisiwani panza, ‘CHV’
Haroub Makame Bakar, anasema kwao ni changamoto kuwafikishia elimu viziwi,
kutokana na wao, kukosa mafunzo ya lugha ya alama.
‘’Sisi ‘CHV’ tupo watano kwenye shehia hii,
lakini hakuna hata mmoja ambae anaelimu, japo ndogo ya lugha ya alama, inakuwa
vigumu kuwasiliana nao,’’anasema.
WIZARA YA AFYA INASEMAJE?
Afisa Mdhamini wizara ya Afya Pemba Khamis
Bilali Ali, anasema anapotokezea mjamzito mwenye uziwi, huwasiliana na mamlaka
husika, kwa ajili ya kupatiwa mkalimani.
‘’Ni kweli wataalamu wetu wa afya hawana
utaalamu wa ukalimani, lakini akitokezea mjamzito na mwenzawake wanahitaji
ukalimani, tunawasiliana na wenzetu katika hilo,’’anasema.
Eneo jingine, anasema wapo wajawazito ambao
ni viziwi, lakini panapokua na shida ya kupata elimu zaidi, huhudhuria kliniki
na waume zao.
‘’Wakati mwengine hufuatana na ndugu au
jamaa zao wanaoelewa lugha ya alama, ili madaktari wanapowasiliana, iwe rahisi
kupata majibu,’’anaeleza.
Anaona bado ipo fursa kwa wale viongozi wa
jumuia za watu wenye ulemavu, kuwasilisha maombi kwao, ikiwa wanahitaji elimu
ya afya uzazi, chini ya mkalimani wao.
Mtaalamu wa afya ya uzazi kutoka hospitali
ya Chake chake Rahila Salim Omar, anasema haki ya afya ya uzazi ndio msingi wa
kuwa na afya njema.
Anaona, bado baadhi ya wanaume, wamekuwa
wazito kuwasindikiza wenza wao, kuhudhuria kliniki, jambo ambalo husababisha
matatizo kadhaa wakati wa kujifungua.
NINI ATHARI YAKE?
Aisha Hussein Khamis, anasema kama wao
wataendelea kutengwa kwenye elimu ya afya uzazi, kunaweza kukalizwa matatizo
kadhaa, ikiwemo kifo kwa mama na mtoto.
Mwanajuma Majid Ibrahim, anasema athari
nyingine ni kukosekana kwa mfumo wa lihse husika kwa mjamzito, kunakotishia kuzaliwa
mtoto mwenye utapiamlo.
Mbarouk Juma Daudi wa Kengeja, anasema
athari nyingine ni kuongezeka kwa uzazi wa papokwa papo, kunachochangiwa na
ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi.
Afisa Mdhamini wizara ya Afya Khamis Bilali
Ali, anasema moja ni kuongezekwa kwa wimbi la wanaojifungulia majumbani.
Afisa wa Chama cha Viziwi wilaya ya Chake
chake Mohamed Khamis Shehe, anasema ni kuwaweka wao katika msingi wa kukumbwa
na magonjwa nyemelezi.
NINI KIFANYIKE?
Mratibu wa Baraza la Taifa la watu wenye ulemavu
Zanzibar ofisi ya Pemba, Mashavu Juma Mabrouk, anasema ni wizara ya Afya, kurudi
kwa kundi la watu wenye ulemavu, ili kuliemisha kwa mujibu wa miundombinu yao.
Mkalimani wa lugha ya alama Asha Suleiman,
anashauri vipindi na taarifa zote za kwenye tv zinapoendeshwa, kuwepo kwa
mkalimani.
Mzazi mweye kijana mwenye uziwi, anasema ni
kutekelezwa kwa sheria kama zilivyo, ili kundi hilo lipate haki zao.
TAMWA
ZANZIBAR INAFANYA NINI?
Chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania TAMWA-
Zanzibar na Tanzania bara wanashirikiana, katika kuendesha mradi wa mwaka mmoja,
wa kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuandika, habari za afya ya uzazi.
Kwenye mafunzo yaliofanyika Pemba, Mratibu wa mradi huo
Zaina Abdalla Mzee, anasema tafiti zilionesha, kuna vipindi na habari kidogo,
katika vyombo vya habari, juu ya haki ya afya ya uzazi.
Mradi huu wa majaribio, ambao unafadhiliwa na Shirika la
Wellspring Philonthropic fund la Marekani, unaendeshwa katika wilaya za Chake
chake, Magharibi ‘B’ na Kati.
Moja ya shabaha kuu, ni kuhakikisha wanawake na wasichana
walioko mjini na vijijini, wanakuwa na elimu sahihi ya afya uzazi, kupitia
vyombo vya habari.
TAKWIMU
Wakati hayo yakifanyika, Wizara ya Afya Zanzibar,
imebainisha kuwa, katika kipindi cha mwezi Julai, 2022 hadi Machi, 2023, kuna vifo
vya mama 46 na vya watoto wachanga chini ya siku saba 1,567 viliripotiwa.
Vifo hivyo ni sawa na kila wilaya moja ya Zanzibar kati ya
11, kuwepo wa vifo vya mama watano, sawa na 142 nao kufariki katika wilaya
hizo, katika kipindi hicho.
Aidha mwaka huo huo, wapo wajawazito 52,891, sawa 4,808
kutoka kila wilaya moja ya Zanzibar, waliohudhuria kliniki ya upimaji mimba,
angalau mara moja.
Kati yao, wajawazito 9,017 walihudhuria kliniki wakiwa na
ujauzito chini ya wiki 12, huku kukiripotiwa wajawazito 38,097, Unguja 26,405
na Pemba 11,692 kujifungulia hospitali.
Mwisho
Comments
Post a Comment