NA ZUHURA JUMA, PEMBA @@@@
WAANDISHI wa habari kisiwani Pemba wametakiwa kufuata maadili ya kazi zao, ili kuepuka kuingia kwenye makosa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa maadhimisho ya siku ya uhuru wa habari, leo Mei 18, 2024 uliofanyika ukumbi wa Chuo cha Samail Gombani Chake chake Pemba, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, alisema mwandishi wa habari aliesomea fani ya habari hawezi kuvunja miiko na maadili.
Alisema kuwa, tasnia ya habari sasa imevamiwa na watu ambao hawakusomea fani hiyo, jambo ambalo linaweza kusababisha migogoro katika jamii na kushusha hadhi ya tasnia, hivyo ipo haja kwa waandishi wa habari kuzingatia maadili wakati wa kazi zao ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza.
"Siku hii ya uhuru wa habari ni muhimu kujitafakari kwamba tunafanya kazi kwa kiasi gani, tuna uhuru kiasi gani, vikwazo gani tunavyopitia na kupanga mikakati ya kuweza kutatua," alisema Mkuu huyo.
Mkuu huyo aliwataka waandishi hao kuibua changamoto za wananchi na kuzisemea, ili ziweze kupatiwa ufumbuzi, kwani sauti ya mwandishi ndio inayosaidia katika kuleta mabadiliko na maendeleo katika nchi.
Aidha aliwataka waandishi kuelimisha jamii juu ya kuhifadhi mazingira, ili yawe safi na kuweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamekuwa yakiathiri maisha ya wananchi.
Kwa upande wake Afisa Mdhamini Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Pemba Mfamau Lali Mfamau alisema, waandishi wa habari wana wajibu wa kuwatumikia wananchi, hivyo wafike vijijini kuibua kero zinazowakabili.
"Tufanye kazi kwa bidii na kudumisha nidhamu, pia nawaomba waandishi wenye online TV na blogi wajisajili na kutafuta kadi ya uandishi, kwani kuna baadhi ya watu wanatumia mwamvuli wa waandishi kujifanya mwandishi," alisema Mdhamini huyo.
Mapema Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Pemba (PPC) Bakar Mussa Juma alisema, waandishi wa habari katika Klabu hiyo wanafanya kazi vizuri na kuzingatia maadili ya uandishi wa habari, hivyo wanaomba jamii na viongozi mbali mbali kuendelea kuwapa ushirikiano ili wapate habari na kuzisemea.
Alisema kuwa, Klabu ina malengo makubwa ya kuanzisha radio na television ili waajiri waandishi wao, ambapo kwa sasa wameanza na blogi ambayo inawapatia mafanikio makubwa katika tasnia hiyo.
Nae akiwasilisha mada katika maadhimisho hayo mwandishi wa habari na Mjumbe kutoka PPC Gaspar Charles alisema, waandishi wa habari wana jukumu la kulinda na kuelimisha jamii kuhifadhi mazingira ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi.
Maadhimisho hayo ya siku ya uhuru wa habari yamefanyika katika Ukumbi wa Samael Gombani Chake Chake ambayo yameandaliwa Klabu ya Waandishi wa Habari Pemba (PPC) kwa ufadhili wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).
Comments
Post a Comment