NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
MWENGE wa uhuru wa kitaifa, umewasilileo Mei 13, 2024 katika
mkoa wa kusini Pemba, kwa ajili ya kutembezwa katika wilaya za Mkoani na Chake
chake, ukitokea mkoa wa Dar-es Salaam Tanzania bara.
Mwenge huo, umepokelewa katika uwanja wa ndege
wa Pemba, na kupokelewa na wakuu wa mikoa ya kusini na kaskazini Pemba, wakuu
wa wilaya nne za Pemba, maafisa wadhamini, viongozi wa Chama cha Mapinduzi, ‘CCM’
wa mikoa ya Pemba, wafanyakazi wa serikali na wananchi wengine.
Kabla ya Mkuu wa mkoa wa Dar-es Salaam Albert
Chalamila kumkabidhi Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba, Mattar Zahor Massoud mwenge
huo, alisema aliupokea ukitokea mkoa wa Pwani ukiwa salama.
Mkuu huyo wa mkoa alisema, mwenge huo ukiwa
ndani ya mkoa wake ulitembezwa urefu wa kilomita 427.7 kwa siku tano, na ulizindua
miradi 39 yenye thamani ya shilingi bilioni 479.6.
Alieleza kuwa, pamoja na uzinduzi huo wa
miradi, mwenge huo ulisababisha wananchi 994, kujitokeza kuchunguuza afya zao,
wakiwemo wanawake 456 na wanaume 538, na wananchi sita kati yao, waligundulika
na virusi vya ukimwi, wakiwemo wanawake wanne na wanume wawili.
Aidha alieleza kuwa, wananchi wa mkoa wa
Dar-es Salaam, kutoka wilaya zote, wapatao 272 walijitokeza kuchunguuza afya zao,
kuangalia homa ya malaria, wakiwa wanaume wakiwa 88 na wanawake 184, waliogundulika
walikuwa watatu, wote wakiwa ni wanaume.
‘’Mwenge wa uhuru kwa mwaka huu, umesaidia
sana wananchi wa mkoa wangu wa Dar-es Salaam, maana wamepata ushauri, kuchunguuza
magonjwa bila ya malipo na kisha kupewa ushauri nasihi,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar-
es Salaam, alisema wakimbizwa mwenge wa uhuru kitaifa, wamefanyakazi kubwa wakiwa
mkoani humo, kwa kutoa ujumbe wa mwenge kwa upana.
Mapema kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa
Godfrey Eliakimu Mnzava, alisema wamejifunza mambo kadhaa, walipokuwa mkoa wa
Dar-es Salaam, ikiwa ni pamoja na umoja na mshikamano kwa watendaji wote.
Katika hatua nyingine, aliutaka uongozi wa
mkoa wa kusini Pemba, kuhakikisha wanapata taarifa za miradi mapema, kabla ya
kuanza ukaguzi na uzinduzi, ili kujiridhisha.
Alieleza kuwa, jingine ni kuhakikisha kila
mradi wanawekewa wataalamu husika, ambao wanataarifa za ndani na za uhakika,
juu ya mradi husika, ili kazi ya uzinduzi iwe rahisi.
‘’Ile miradi ambayo imepangwa mwenge wa uhuru
uyapitie, ni vyema kwa wakuu wa wilaya na watendaji wingine, kujipanga na
taarifa zipatikane mapema, samba mba na kuwekwa kwa wataalamu husika,’’alisisitiza.
Mara baada ya mkuu wa mkoa wa kusini Pemba,
Mattar Zahor Massoud kuupokea mwenge huo, na watembeza mwenge sita, alisema
utatembezwa katika wilaya za Mkoani na Chake chake, kabla ya kuukabidhi mkoa wa
kaskazini Pemba.
Alisema, miradi kwa upande wa wilaya ya
Mkoani, ipo tisa ikiwa ni pamoja na kilimo cha umwagiliaji maji bonde la
Mlemele, mradi wa mazingira Pujini, barabara eneo la Mauwani Kiwani.
Mradi mwingine ni ushirika wa wajasiriamali shehia
ya Kukuu, kisima cha maji shehia ya Stahabu, ujenzi wa dakhalia skuli ya
Michenzani, ujenzi wa nyumba za daktari hospitali ya Abdalla Mzee, pamoja na ugawaji
wa vyandarua kwa watoto waliochini ya umri wa miaka mitano na utoaji matone ya
vitamin ‘A’.
Mkuu wa wilaya ya Mkoani Khatib Juma Mjaja, alisema
atahakikisha mwenge huo pamoja na watembeza mwenge wake, watakuwa na amani wakati
wote wakiwa wilayani humo.
Mwenge wa uhuru wa kitaifa kwa mwaka 2024, ulizinduliwa
na waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa Aprili 2, 2024 uwanja wa chuo
kikuu cha Ushirikia Moshi Tanzania bara.
Mwisho
Comments
Post a Comment