WANANCHI wa shehia ya Mwambe wilaya ya
Mkoani Pemba, wameiomba serikali, kufanya utafiti wa kina kubaini sababu za
kuongezeka matukio ya ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto, ili
kundi hilo nalo liishi kwa amani.
Walisema licha ya mikakati, mipango na
maazimio ya muda mfupi na mrefu ya kutokomeza vitendo hivyo, bado vimekuwa vikishamiri
siku hadi siku, jambo linalowapa wasiwasi wa kutokupungua.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi shehiani
hapo, walisema hawaoni kuwa, iko siku wanawake na watoto watakuwa huru na vitendo
vya ukatili na udhalilishaji, kutokana na kuongezeka siku hadi siku.
Walisema, kumekuwa na juhudi kubwa
zinazofanywa na serikali kuu, kwa kushirkiana na washirika wake wa ndani na
nje, jambo ambalo walitarajia kuona mabadiliko.
Maua Mwitani Ussi wa Jombwe, alisema
kumekuwa na mikakati kuanzia ngazi ya familia, shehia, wilaya, mkoa, taifa na
kimatifa ingawa kila siku vyombo vya habari, vinaripoti matukio hayo.
‘’Kumekuwa na juhudi ni kubwa mno za kuyashinda
matukio ya ukatili na udhalilishaji, lakini kama haukujafanyika utafiti wa kina
wa kubaina sababu, watoto na wanawake tutaendelea kukukosa amani,’’alieleza.
Nae Mwajuma Haji Makame wa Bwegeza
alisema, utafiti ndio pekee utakaokuja na jibu sahihi, juu ya sababu za
kuongezeka kwa matendo hayo ndani ya jamii.
Kwa upande wake Kombo Othman Mossi wa
Mchakwe, alisema kila jambo unapotaka kulindoa, lazima kutanguliwe na kujua
sababu za ndani, unaotokana na kufanyika kwa utafiti kwa kina.
‘’Serikali kwa sasa ishirikiane na wadau
wake wa ndani na nje, kufanya utafiti mkubwa kwa kila eneo, ili kubaini nini
chanzo cha kuongezeka kwa matendo hayo,’’alifafanua.
Sheha wa shehia ya Shamiani Mwambe Safia Khamis Ngwali ,
alisema ni kweli kumekuwa kukiripotiwa matukio hayo kila siku, kama vile hakuna
juhudi zozote zinazofanywa na serikali.
‘’Hata sisi masheha, kila siku tumekuwa tukisisitizwa
kufikisha elimu ya kupinga matukio hayo, kila tunapokutana na wananchi, ingawa
cha kushangaaza, bado matukio yanaibuka siku hadi siku,’’alieleza.
Afisa Mawasiliano Chama cha waandishi wa habari
wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba Gaspary Charles alisema, moja
ya sababu ya kuripotiwa kwa wingi matukio hayo, katika taasisi husika,
inatokana na jamii sasa kupata uwelewa.
‘’Inawezekana hapo zamani, tuliyaona matukio
hayo ni kidogo, kwa sababu watendewa walidhani ni jambo la kawaida, ingawa
baada ya kupata elimu sasa wanaripoti kila wanapofanyiwa,’’alifafanua.
Mwenyekiti wa Jumuiaya ya Tumaini jipya
Pemba ‘TUJIPE’ Tatu Abdalla Msellem, alisema suala la kufanyika kwa utafiti wa
nchi nzima, ni jambo la msingi, ili kujua panapohitajika kutibiwa.
‘’Lakini sasa wanawake na watoto
wameshapata elimu ya kutosha, na ndio maana wamekuwa wakiripoti hata
wanapokamatwa makalio, baada ya kuelewa kuwa ni aina ya udhalilishaji,’’alifafanua.
Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba Salama Mbarouk
Khatib, alisema utafiti wa kubaini chanzo ni jambo moja, lakini la pili ili
kutokomeza matendo hayo, ni kushirikiana na vyombo vya sheria.
‘’Zipo kesi hufutwa mahakamani, kwa kule
mashahidi kutofika mahakamani kutoa ushahidi, sasa je na hili linahitaji
kufanyiwa utafiti, maana lipo wazi,’’alihoji.
Afisa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto wilaya ya Chake
chake Salma Khamis Haji, alisema njia ya kutokemeza matendo hayo, ni kwa watendewa,
kutoa taarifa, pindi wanakapoona viashiria vya ukatili na udalilishaji dhidi
yao.
Sheikh Abdalla Nassor Mauli, alisema kama jamii itaamua
kukifuata kitabu cha Allah kwa vitendo, matendo hayo yatapungua hata kabla ya
kufanyika kwa utafiti wowote.
Matukio ya ubakaji, ulawiti ambayo
huwakumba wanawake na watoto hapa Zanzibar, yameripotiwa kupungua kiduchu kwa
mwezi Machi, na kufikia 125, upungufu wa matukio 50 kwa mwezi Febuari mwaka
huu.
Taarifa kutoka kwa ofisi ya Mtakwimu mkuu
wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inaonesha kuwa mwezi Febuari pekee kuliripotiwa
matukio 175, sawa na matukio sita kwa siku.
Ingawa kwa mwezi Machi, kumeripotiwa
wastani wa matukio manne kwa siku, ambapo ikaelezwa kuwa, kwa miezi hiyo mwili,
kuliripotiwa matukio 300, ambayo ni wastani wa matukio 28, kwa kila wilaya,
kati ya zote 11 za Zanzibar.
Kati ya matukio hayo, mwezi Machi pekee
katika wilaya hizo 11, imeonesha kila wilaya, kuliripotiwa wastani wa matukio
11, ingawa kwa mwezi Febuari kumeonesha kuwepo matukio 16, kwa kila wilaya moja
kwa Unguja na Pemba.
Mwisho
Comments
Post a Comment