Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe.Riziki Pembe Juma amesema upimaji wa afya ni muhimu sana kwa wanamke na mtoto, kwani uchunguzi husaidia kutathmini hali ya afya na kusaidia kutambua matatizo yoyote yanayoweza kutokea.
Pia amesema hatua hiyo itawasaidia katika kuwakinga watoto na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.
Mhe Riziki ameyasema hayo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Taasisi ya Maisha bora Foundation mama Maryam Mwinyi, katika kampeni ya Afya bora maisha bora iliyofanyika katika viwanja vya Kivunge Wilaya ya Kaskazini A Unguja.
Amesema Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto imefanikiwa kuweka namba ya simu inayotambulika 116 kwa kupiga bure, ikiwa lengo ni kutoa taarifa masuala yote ya udhalilishaji na kuweza kufuatiliwa na kuchukuliwa hatua.
Ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwasaidia watoto wanapowapatia taarifa za vitendo hivyo, huku akiwasihi kurejesha malezi ya pamoja ili kuwakinga watoto juu ya vitendo hivyo.
Aidha kwa upande wake binafsi Mhe.Riziki ameipongeza Taasisi ya Maisha bora Foundation kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa kwa Serikali katika kupiga vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia hapa nchini.
Wakati huo huo, Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na watoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto (SMZ) bi Siti Abass Ali amesema Wanawake nchini wametakiwa kujitathmini na kujitambua katika kupambana katika kujiletea maendeleo wenyewe.
Mkurugenzi Siti ameyasema hayo, wakati alipofungua mafunzo ya wajasiriamali kwa wanawake wa wilaya mbalimbali za Unguja, ikiiwa ni shamrashamra za kuadhimisha siku ya wanawake duniani Machi,08.
Amesema wanapoadhimisha siku ya wanawake duniani kila mwaka nilazima wanawake kujitathmini katika mwaka mzima ni kitu gani wamefanya katika kujiletea maendeleo na endapo kuna tatizo ni vyema kulitatua ili kusonga mbele kimaisha.
Amesema Wizara imeamua kufanya mafunzo kwa wajasiriamali wanawake, ikiwa lengo ni kuwaunganisha pamoja wanawake na kupeana moyo katika maendeleo, pamoja na kupeana nguvu kwa kugombania nafasi mbalimbali za uongozi ili kuweza kuwa mbele kimaendeleo.
Kwa upende wao baadhi ya wajasiriamali hao, wameishukuru Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto kwa kuweza kuwapatia elimu hiyo ambapo wameomba kusaidiwa katika kupunguziwa masharti ya upatikanaji wa mikopo ili nao waweze kunufaika.
Pia wamewaomba wafadhili wanapotoa misaada mbalimbali kwa wajasiriamali kufika vijijini kwani wamedai kuwa fursa hizo wamekuwa wakizikosa ukilinganisha na watu wanaoishi mjini.
Mafunzo hayo ya siku mbili kwa wajasiriamali wanawake yamefanyika katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkoa wa Kaskazini, na Mkoa wa Kusini, ambapo maada mbalimbali ziimewasilishwa ikiwemo matumizi sahihi ya fedha, nafasi za uongozi kwa wanwake na nyenginezo.
Mwisho
Comments
Post a Comment