NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
MKAGUZI wa shehia ya Mlindo Wilaya ya Wete, Inspekta wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Khalfan Ali Ussi amewataka wanajamii kushirikiana pamoja katika kuhakikisha wanapambana na wizi wa mifugo pamoja na mazao.
Aliyasema hayo wakati wa kampeni ya nyumba kwa nyumba kutoa elimu ya kupambana na matendo ya kihalifu katika jamii, kupitia mradi wa 'familia yangu haina uhalifu' ambao husikiliza changamoto za wananchi na kutafuta mbinu mbadala ya kuzitatua.
Alisema kuwa, iwapo wanajamii watashirikiana katika kukomesha vitendo vya kihalifu, watafanikiwa kudhibiti wizi wa mazao na mifugo ambao kwa sasa umeshamiri katika shehia hiyo, hali ambayo inarudisha nyuma juhudi za wananchi ambao wanapambana na hali duni ya maisha.
"Lengo la ziara yetu hii ni kuendeleza kufanyia kazi miradi ya Polisi jamii, kusikiliza kero za wananchi na kizitafutia ufumbuzi," alisema Mkaguzi huyo.
Alifahamisha kuwa, anaamini kwamba kampeni hiyo ya nyumba kwa nyumba italeta tija katika shehia hiyo kwani mara nyingi wanapoitisha mkutano baadhi ya wananchi hawahudhurii, jambo ambalo linasababisha kutofikiwa kwa lengo walilolikusudia.
Aidha alieleza kuwa, ili kufanikiwa katika kudhibiti wizi kwenye vijiji vyao, kuna haja ya kuacha muhali ili kuweza kuzalisha zaidi na kujipatia kipato kitakachowakwamua na umasikini.
"Kilimo na mifugo ni miradi ambayo ina tija kubwa sana iwapo utazalisha zaidi na ikiwa hutoibiwa, hivyo nakuombeni mifugo muijengee mazizi karibu na munapoishi na atakapotokea mwizi mfikisheni kwenye vyombo vya Sheria," alieleza.
Alisema kuwa, pia watakapoimarisha ulinzi katika mazao na mifugo yao itawasaidia kupata mkopo utakaowawezesha kuzalisha zaidi na kupata bidhaa bora zitakazoingia kwenye soko, kwani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewekeza fedha nyingi kwa ajili ya kuwakomboa wananchi kiuchumi.
Kwa upande wa familia hizo walishukuru juhudi anazozichukua Mkaguzi huyo kuhakikisha anawapa elimu mara kwa mara, kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi unaofaa.
Mwananchi Juma Hamad Seif alieleza kuwa, pamoja na kuwepo kwa ulinzi shirikishi katika shehia yao lakini bado suala la wizi hawajaweza kulidhibiti, kiasi ambacho kinawakwaza sana.
"Kila siku tunalima na tunafuga lakini hatufaidikia na chochote kwa sababu wizi wanatumaliza na umasikini unazidi," alisema mwananchi huyo.
Kwa upande wake mzee Hamad Seif alisema watakaposhirikiana na kuacha muhali, watafanikiwa kudhibiti vitendo vyote vya uhalifu ikiwemo wizi, udhalilishaji na madawa ya kulevya.
MWISHO.
Comments
Post a Comment