NA HAJI
NASSOR, PEMBA@@@@
USHIRIKA
wa ‘tudumishe maendeleo’ uliopo Misooni shehia ya Shungi wilaya ya Chake chake,
umesema kama migomba yao 50 walioipanda mwaka jana, itazaa kwa pamoja, watajipatia
faida ya shilingi 195,000.
Kwani ushirika
huo umetumia shilingi 25,000 kwa ununuzi wa miche 50 ya migomba aina ya mkono
wa tembo, mtwike, kipukusa kwa wastani wa shilingi 500 kila mche mmoja na shilingi
30,000 kwa kulimishia shamba loa kwa hatua ya awali.
Mwenyekiti wa
ushirika huo Mbarouk Idrissa Omar, wakati akizungumza na mwandishi wa habari
hizi kijijini hapo alisema, waliamua kujikusanya pamoja na kuendesha kilimo
hico, ikiwa ni njia moja yapo ya kujikwamua na umaskini.
Alisema, walichagua
kilimo cha migomba, kutokana na eneo walilo linakukubali vyema hasa kwa aina ya
ardhi yao ilivyo, kilimo hicho ndio kilichoonekana kunawiri vyema,
ilikinganishwa na mazao mingine.
Alieleza kuwa,
matumiani yao ni kuwa, kama migomba hiyo 50 walioipanda mwezi Januari mwaka
jana, na kuzaa kwa pamoja na wanaweza kuvuna ndizi 50 na baada ya kuuza kila
moja kwa wastani wa shilingi 5,000 kwa bei ya jumla, watajipatia shilingi
250,000.
‘’Kima hicho
sio kidogo, maana hata tukishatoa gharama zetu za miche, mbolea, usafishaji tunaweza
kupata faida ya shilingi 195,000 jambo ambalo kwetu sio dogo, maana na shughuli
zetu nyingine za binafsi hazijasimama,’’alieleza.
Katibu wa
ushirika huo Ame Suleiman Juma, alisema walichokifanya ndani shamba hilo la migomba,
wamepanda na mihogo wastani wa mashina 50, ambayo nayo baadae wanampango wa
kuuziana wenyewe.
‘’Huu muhogo
umepandwa hivi karibuni, lakini nao kama utazaa vyema, tunaweza kujipatia
wastani wa shilingi 100,000, kwani shina moja ni kati ya shilingi 1,500 hadi shilingi
2,000 hutegemea na mzao ulivyo,’’alifafanua.
Hata hivyo Katib
huyo, alieleza kuwa, mbali na kilimo cha migomba na mihogo, ushirika wao unajishughulisha
na kilimo cha mchicha na bilingani, ingawa changamoto katika eneo, hilo ni
maji.
‘’Inatubidi tubebe
maji kwa kichwa, kutoka kilipo chanzo hadi kwenye kilimo chetu, jambo ambalo
wakati mwingine huongezeka gharama, kwa kule kuwalipa watu wa nje,’’alifafanua.
Mshikafedha wa
ushirika huo Moza Salim Mohamed, alieleza kuwa kwenye kilimo cha mboga
wameshavuna misimu saba, ambayo yote baada ya kutoa gharama, wamejipatia
shilingi 100,000.
Alisema mavuno
huwa mabaya, kutokana na changamoto kadhaa ikiwemo, ukosefu wa maji ya uhakika,
utaalamu mdogo, ukosefu wa mbole hasa ya kuulia wadudu, ambao hupendelea kushambulia
micheo yao.
‘’Tulianzia
na mtaji wa shilingi 90,000 kwa mara ya kwanza, zilizotumika kwa ununuzi wa mbegu
za mchicha, bilingani, mbolea, upigishaji matuta, na kwa mara ya kwanza
tulipata faidi shilingi 20,000 pekee,’’alifafanua.
Akizungumzia
kuhusu soko, alisema wateja wa kwanza ni wanachama wenyewe, familia zao,
majirani na kisha bidhaa inayobakia huirandisha kijijini kwao, na hubahatika
kununuliwa yote.
Mwanachama wa
ushirika huo Asha Suleiman Hamad na mwenzake Fatma Mohamed Kassim, walisema kwa
sasa maisha yao yamebadilika kiasi, kwa kule kuwa na uhakika fedha japo ndogo.
‘’Maana
pamoja na changamoto zote hizo, lakini tunazo fedha kiasi kama akiba, na ushirika
unaendelea kubuni miradi mingine, sasa unapopata changamoto ya kimaisha, kwa
sasa tunajua wapi tuelekee tofauti na zamani,’’walisema.
Ushirika huo
wa ‘tudumishe maendeleo’ uliopo kijiji cha Misooni shehia ya Shungi, wilaya ya
Chake chake, ambao una wanachama saba, wakiwa wanawake watano na wanaume wawili,
ulianza mwaka 2022, unajishughulisha na kilimo cha mchicha, bilingani, migomba
na mihogo.
Mwisho
Comments
Post a Comment