NA MARYAM NASSOR, ZANZIBAR@@@@
MTUHUMIWA wa
kesi ya kuua kwa makusudi, inayosikilizwa mahakama kuu Tunguu Zanzibar,
inayomkabili Omar Mahmoud
Abdallah (36) mkaazi wa Jang’ombe
Unguja, ameendelea kusota rumande, baada ya upande wa mashtaka, kushindwa
kukamilisha upelelezi wa shauri
hilo kwa wakati.
Mara baada ya kufika mahakamani hapo, mtuhumiwa huyo akitokea rumande, Mwendesha mashtaka kutoka ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka Zanzibar Said Ali Said, alimueleza Jaji wa mahakama kuu Zanzibar kuwa, kesi iyo ipo kwa ajili ya kuanza kusikilizwa maelezo ya awali, lakini bado upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.
“Mheshimiwa Jaji leo, kesi hii ipo kwa ajili ya kusikilizwa, lakini bado
hatujakamilisha upelelezi wa kesi na
mashahidi, hivyo tunaomba utupangie tarehe nyingine, kwa ajili ya kusikilizwa,’’
alidai.
Baada ya maelezo hayo, Jaji wa mahakama kuu
Zanzibar Ali Mohamed Ali, aliwauliza mawakili wa upande wa utetezi
uliokuwa ukiongozwa na Ali Rashid Ali na
Elia Elisha kuwa, wanakubaliana na ombi la upande wa mashtaka.
Wakili hao walidai kuwa, hawana
pingamizi yoyote juu ya ombi hilo, ila
wanataka upande wa mashtaka kujihimu
kukamilisha maelezo ya kesi, na mashahidi illi kesi hiyo ianze kusikilizwa.
“Hatuna
pingamizi na upande wa mashtaka ila tunataka, wajihimu kukamilisha maelezo ya kesi, ili mteja wetu ajuwe hatma
yake mapema,” walidai mawakili hao.
Jaji wa
mahakama hiyo, aliuliza upande wa
mashtaka kuwa ni lini, watakuwa
wameshakamilisha maelezo ya kesi na mashahidi na kujibu hivi karibuni.
Jaji huyo,
aliutaka upande wa mashtaka kuwa wanatakiwa kukamilisha maelezo ya kesi na mashahidi kwa wakati, ili
kesi hiyo ianze kusikilizwa.
Kwa mara ya
kwanza shauri hilo, lilisomwa mahakamani hapo
August 29 mwaka 2023 na
kuhairishwa miezi mitatu mfululizo, kutokana
na kutokamilika kwa upelelezi wa kesi hiyo.
Awali
ilidaiwa mahakamani hapo na mwendesha
mashtaka kutoka afisi ya mkurugenzi wa mashtka Zanzibar, kuwa mstakiwa
huyo anadaiwa kumuua kwa makusudi kijana
Seif Omar Salum.
Mshtakiwa
huyo, alitenda kosa hilo, Jang’ombe wilaya ya Mjini, mkoa wa mjini Magharibi Unguja, majira ya saa 1:00 usiku.
Ilidaiwa
mahakamani hapo kuwa, kutenda hivyo ni
kosa kinyume na kifungu cha 179 na 180
chini ya kifungu namba 6 cha mwaka 2018 sheria za Zanzibar.
Jaji huyo,
aliutaka upande wa mashtaka kukamilisha
upelelezi wa shauri hilo,
ili kesi hiyo ianze kusikilizwa
mahakamani hapo na kuihairisha kesi hiyo hadi Machi 20 mwaka huu, kwa ajili ya
kusikilizwa maelezo ya awali na mtuhumiwa kurejesha rumande.
MWISHO
Comments
Post a Comment