NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
VIJANA wa shehia ya Pandani Wilaya ya Wete Pemba, wametakiwa kuendelea kushikamana pamoja na kuwasimamia vijana wadogo, ili wakue katika maadili mema, hali itakayosaidia kujenga jamii yenye heshima.
Akizungumza Machi 12, 2024 mara baada ya kukabidhi mipira ya kufanyia mazoezi kwa vijana wa vijiji vya Masipa, Kijuki na Kidutani, Inspekta wa Jeshi la Polisi na Mkaguzi wa shehia ya Pandani Khalfan Ali Ussi alisema, ili kujenga jamii iliyobora ni lazima vijana wafuate maadili mema na kuacha kufanya mambo yasiyofaa.
Alisema kuwa, ushirikiano na mshikamano ni muhimu katika kuelekezana kufuata maadili mema, hivyo ni vyema kuendeleza ili kujenga jamii iliyobora na yenye heshima.
"Nawapongeza sana kwa juhudi mnayoichukua kuhakikisha vijiji hivi vinakuwa salama na kuwataka waendelee, kwani jukumu la ulinzi wa mali zao ni la kila mwanajamii," alisema Inspekta huyo.
Inspekta huyo aliwaasa vijana hao kuacha muhali kwa vijana wanaojihusisha na matendo maovu, badala yake wawafikishe kwenye vyombo vya Sheria ili kukomesha vitendo hivyo ambavyo vimekuwa vikitokea siku hadi siku kwenye jamii.
"Tusiwe woga na wala tusiwafumbie macho watu waovu, wanapofanya makosa tuwafikishe vituo vya Polisi au kwa askari wa shehia, kwani Sheria inaruhusu na uwezo wa kumkamata munao, tusikae kulalamika tu," alieleza.
Akizungumzia suala la mazoezi alisema, ni muhimu sana kwa kuimarisha afya ya mwili na akili sambamba na kuwaepusha kufikiria kutenda vitendo viovu, kwa sababu muda mwingi wanakuwa kwenye mazoezi.
Kwa upande wake Mratibu wa Dawati la Wanawake na Watoto Mkoa wa Kaskazini Pemba A/INSP Amina Sipe aliwataka vijana hao kuwaheshimu wazazi wao na kujiepusha na vitendo vya udhalilishaji kwani vina madhara makubwa kwao na kwa jamii.
"Hakikisheni munadhibiti matamanio yenu ili yasiwapeleke pabaya, hivyo mujiweke (busy) kwenye mazoezi zaidi ili kuepuka vitendo hivyo," alisema.
Nao vijana hao ambao pia wanajishughulisha na ulinzi shirikishi, walimshukuru Mkaguzi huyo wa shehia kwa imani, upendo pamoja na ufuatiliaji wa mara kwa mara katika kikundi chao, ili kujua changamoto zinazowakabili na kuweza kuwasaidia," walieleza.
Comments
Post a Comment