Serikali zote mbili
zinatambua umuhimu na mchango mkubwa unaotolewa na wanawake hapa nchini na
zimekuwa zikichukua hatua mbali mbali za kumlinda na kuwawezesha katika hatua
za kimaendeleo.
Hayo yamesemwa na Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi
katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar. HEMED SULEIMAN ABDULLA katika Kongamano la Uwezeshaji wanawake Kiuchumi
Zanzibar linaloenda sambamba Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani
lililofanyika katika Ukumbi wa Hotel ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar leo.
Amesema kuwa kwa kutambua mchango wa wanawake nchini
serikali imeongeza nafasi za wanawake katika vyombo vya maamuzi kutokana na
marekebisho ya katiba ya mwaka 2010 kwa kuongeza asilimia ya viti maalum vya
wanawake katika Baraza la Wawakilishi kutoka asilimia 30 hadi asilimia 40.
Rais Dkt. Mwinyi amesema
kuwa Serikali kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi imetoa mafunzo
mbali mbali kwa wajasiriamali wapatao 5,231 ambao kati ya hao 3,581 ni wanawake
sambamba na kutoa mikopo zaidi ya Bilioni 29 kwa wajasiriamali wakiwemo
wanawake kwa lengo la kuwaendeleza kuichumi.
Sambamba na hayo Dkt.
Mwinyi amesema Serikali inakamilisha kwa hatua za mwisho katika ujenzi wa
masoko ya kisasa ambayo fursa kwa wajasiriamali kufanya biashara zao bila ya
usumbufu na kukuza kipato kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Hata hivyo Rais wa
Zanzibar amesema Serikali itaendelea kushirikiana na mashirika na Taasisi
binafsi katika kutoa fursa mbali mbali kwa wanawake na wajasiriamali kwa lengo
la kuhakikisha mwanamke anasimama na kuweza kujitegemea katika maisha yake
sambamba na kutoa wito kwa wadau wa maendeleo kushirikiana na Chemba ya
wanawake wafanya biashara wa Tanzania (TWCC) ili kuipa nguvu na kuwawezesha
wanawake wengi zaidi nchini.
Mapema Waziri wa
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Riziki Pembe Juma amezishukuru
Serikali zote mbili ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzaia inayoongozwa na Dkt
Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na
Dkt Hussein Ali Mwinyi, kwa juhudi kubwa wanazozichukua katika kuwainua
wanawake kiuchumi hapa nchini sambamba na kuwaunganisha katika majukwaa ya
wanawake.
Amesema kongamano hilo la uwezeshaji wanawake kiuchumi, linakwenda sambamba na maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani yakiwa na kauli mbiu ya mwaka huu isemayo, “Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi kwa Maendeleo ya Taifa.” Ikiwa lengo ni lile la kumuendeleza mwanamke.
Aidha amesema Wizara ya
Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto itaendelea kushirikiana na wadau
mbali mbali katika kuhakikisha wanamuinua mwanamke kiuchumi pamoja na kupiga
vita vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na
wanawake na watoto,
Naye Mwenyekiti wa
Taasisi ya Tanzania Women Chember of Commerce (TWCC) kwa upande wa Zanzibar, Bi
Tatu Suleiman Tandu katika risala yao wameishukuru Serikali kwa kazi nzuri
inayoendelea kufanyika katika kuukuza Uchumi wa Buluu sekta ambayo inachangia
maendeleo ya haraka na jumuishi kwa wanawake ambayo itasaidia kupunguza
umasikini, kuboresha maisha ya wananchi na kuimarisha uchumi wa Zanzibar kwa
ujumla.
Hata hivyo amesema kuwa
Serikali ya awamu ya nane imewafanyia mambo mengi yakiwemo kuwapatia huduma
wajasiiramali kwa kupata nembo ya ubora kwa gharama nafuu kutoka laki saba hadi
elfu 50 ambayo inasaidia kupata masoko ndani na nje ya Zanzibar.
Aidha wameiomba Serikali
kuangalia upya gharama za Tozo, Ada, pamoja na kodi za uingizaji wa malighafi za
uzalishaji wa bidhaa na vifungashio sambamba na kuwaunganiasha na wajasiriamali
wa nje ya Tanzania kwa lengo la kujifunza kwa vitendo.
Comments
Post a Comment