Na Salma Lusangi, New York@@@@
Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imesema imewawezesha wanawake
kupata fursa za manunuzi ya umma kwa kutoa mafunzo ya kiufundi ili kuongeza
uwezo wa zabuni na matumizi bora ya mifumo ya ununuzi wa kielektroniki.
Taarifa hiyo imetolewa na
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma
mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akifunga kikao cha pembeni (side Event) huko
New York, Nchini Marekani katika ukumbi wa Umoja wa Mataifa.
Mhe Riziki amesema Serikali
imefanya juhudi hiyo ili kuwezesha kila raia wa
Tanzania kumudu faida sawa kutokana na fursa za manunuzi, hasa zile
zinazohusiana na biashara ndogo ndogo zinazoendeshwa na kumilikiwa na wanawake.
Amefahamisha kwamba jitihada hiyo inafanywa na Baraza la Taifa la
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma
(PPRA) na Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGAs).
Alieleza Serikali
yaTanzania inasisitiza matumizi ya mfumo wa kitaifa wa ununuzi wa kielektroniki
ili kuweka mazingira mazuri ambayo pia yanaiwezesha Serikali kufuatilia idadi
ya mikataba ya manunuzi inayotolewa kwa wanawake.
Pia alisema
ili kuhakikisha wanawake wanawezeshwa na ujuzi mdogo wa lugha ya Kiingereza, Serikali
inatayarisha na kuhakikisha nyaraka za zabuni zimeandikwa katika Lugha yetu ya
Taifa (Kiswahili) ili ziweze kueleweka kwa urahisi na kunufaisha makundi maalum
fursa za manunuzi.
Mhe Riziki alifahamisha
kwamba, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanza safari ya ubunifu wa kuendeleza Dira yake mpya ya
Maendeleo 2050 itakayoendesha Ajenda ya Maendeleo ya Taifa kwa miaka 25 ijayo
ili kuhakikisha maono yanafafanuliwa vyema na mienendo ya kijamii na kiuchumi pamoja
na mitazamo ya kijinsia, itazingatiwa.
“Safari ya ubunifu wa
kuendeleza Dira yake mpya ya Maendeleo 2050 itakayoendesha Ajenda ya Maendeleo
ya Taifa kwa miaka 25 itasaidia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na
wasichana katika mipango ya maendeleo ya kitaifa “ Alisema Pembe.
Aidha waziri
huyo ametoa shukrani za pekee kwa Wizara, Idara na Wakala za Serikali, maafisa
wa Umoja wa Mataifa, Taasisi za Utafiti na wadau wa elimu juu, sekta binafsi na
vyombo vya habari kwa kufanikisha mkutano huo.
Mapema
akifungua kikao hicho Mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt
Samia Suluhu Hassan katika masuala ya Wanawake na Makundi Maalum Bi Sophia
Mjema alisema Tanzania Bara na Zanzibar, imeandaa sera, mikakati, mipango, na
programu kadhaa za kuwawezesha wanawake na wasichana na kuhakikisha usawa wa kijinsia katika shughuli
mbali mbali.
Alielezea Sera
ya Taifa ya Biashara ya mwaka 2003 imetaja
haja ya "kuunga mkono ushirikishwaji wa wanawake katika michakato ya
maendeleo ya biashara kupitia upatikanaji wa usawa zaidi wa mali za uzalishaji,
hasa ardhi yenye hati miliki, miundombinu, fedha, elimu na ujuzi".
Pia,
kuongeza mafunzo na kurekebisha taratibu za uendeshaji ili kuruhusu na kukuza
matumizi ya mfumo wa manunuzi ya umma; kushughulikia vikwazo vya kifedha na
upatikanaji wa taarifa za manunuzi ya umma.
Mkutano wa Hadhi ya Wanawake (CSW68) ulianza tarehe 11 hadi 22 Machi 2024, New York nchini Marekani ambapo ya kikao cha pembeni kilikuwa na mada isemayo Kufadhili Usawa wa kijinsia: Kuwawezesha Wanawake na Wasichana Kupata Huduma za Umma na Kuendeleza Ahadi za Kizazi chenye Usawa nchini Tanzania.
Mwisho
Comments
Post a Comment