IMEANDIKWA NA
ZUHURA JUMA, PEMBA
WALIMU
na wanafunzi wa vyuo vikuu kisiwani Pemba wametakiwa kuyatumia matokeo ya sensa
katika kufanya shughuli za utafiti, ili kuwarahisishia katika kazi zao
za kimasomo na kufundishia.
Akifungua kikao cha usambazaji wa
matumizi ya matokeo ya viashiria vya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa wanafunzi
na walimu wa vyuo vikuu kisiwani hapa, Kamisaa wa Sensa Zanzibar Balozi Mohamed
Haji Hamza alisema, takwimu za matokeo ya sensa zitawarahisishia kufanya
utafiti wa haraka.
Alisema kuwa, ni vyema sensa ikatumika
kwa ajili ya kufanya utafiti wa baadae kutokana na matokeo yaliyopatikana,
hivyo ipo haja kila wanapofanya utafiti kutumia takwimu hizo kwa maendeleo yao
na taifa kwa ujumla.
‘’Sensa ina vitu vingi sana tunavyoweza
kuvitumia katika mambo yetu mbali mbali, ikiwemo ya kiutafiti, hivyo tuzitumie
takwimu hizi za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa ajili ya kazi zetu,’’
alisema Balozi huyo.
Aidha aliwahamasisha walimu na wanafunzi
hao kuelimisha jamii ili ihamasike kuyatumia matokeo ya sensa kufanya utafiti
na vitu vyengine vya kimaendeleo, kwani bila ya takwimu utafiti hauwezi kuwa wa
kiwango kizuri.
Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali Salum Kassim Ali alisema kuwa, kawaida wanafunzi wanatumia tafiti kwa ajili ya mazoezi (field) katika vyuo vyao, hivyo aliwashauri walimu kuwahamasisha wanafunzi wao kutumia sekondari data kwani ni rahisi.
‘’Tumewaita hapa kuwafahamisha kwamba
mnapopewa kazi za utafiti kule vyuoni basi mjitahidi kutumia takwimu ambazo
zimepatikana kutokana na matokeo ya sensa, hivyo zitakuwa na thamani na wengine
pia watatumia,’’ alieleza.
Akiwasilisha mada katika kikao hicho,
Meneja Viwango na Utafiti Zanzibar Hamisa Suleiman alifahamisha kuwa, data zote
za hatua ya sekondari zitapatikana kwa kufuata utaratibu unaotakiwa, hivyo ni
vyema kwanza kupata kibali ambacho kinahitaji kulipiwa.
‘’Tufuate utaratibu mzuri wakati wa
kufanya tafiti zetu na sisi tunaangalia data hizo unazitaka kwa lengo gani, ikiwa
utafiti huo una maslahi na nchi yetu kwa maendeleo basi tunakupatia,’’,
alisema Meneja huyo.
Nae Mwenyekiti wa sensa Balozi Amina Salim Ali alisema, matokeo ya sensa ni muhimu kwa kufanya tafiti mbali mbali, kwani kuna takwimu ambazo zitawasaidia katika masomo yao.
Kwa upande wao washiriki wa mkutano huo
walisema, baada ya kuwasilishwa matokeo hayo ya sensa walibaini kwamba, viashiria
vingi vya hatari vinatoka Mkoa wa Kaskazini Pemba, hali ambayo imewapa
wasiwasi, hivyo kunahitajika utafiti wa hali ya juu kuweza kujua tatizo.
Mkutano huo wa siku moja umefanyika
katika ukumbi wa ZRA Gombani Chake Chake ambao umeandaliwa na Ofisi ya Mtakwimu
Mkuu wa Serikali Zanzibar kwa lengo la kuihamasisha jamii kutumia matokeo ya
sensa kufanya mambo yao ya kimaendeleo.
MWISHO.
Comments
Post a Comment