IMEANDIKWA NA
ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
WAZAZI
na walezi wametakiwa kushirikiana pamoja na walimu, kamati ya skuli na kamati
ya shehia katika kuhakikisha wanadhibiti utoro kwa wanafunzi, jambo ambalo litasaidia
kunyanyua viwango vya ufaulu.
Wakizungumza na mwandishi wa habari
hizi, wananchi wa shehia ya Mjiniole Wilaya ya Chajke Chake walisema, kuna
baadhi ya wazazi huchangia watoto wao kuwa watoro kutokana na kuwa anapokaa
nyumbani hamuulizi jambo lolote.
Walisema kuwa, ushirikiano wa dhati
unahitajika katika kudhibiti utoro maskulini kwa lengo la kustawisha maendeleo
ya mtoto kielimu, jambo ambalo litasaidia kusoma na kufaulu vizuri kwenye mitihani
yake.
Mwananchi Fatma Ali Hamad mkaazi wa
kijiji cha Simaongwe alisema kuwa, ni vyema kwa wazazi kuwa tayari
kuwashughulikia watoto ili wapate elimu ambayo itawasaidia katika maisha yao
yote.
Kwa upande wake mwananchi Hamad Khatib
Hamad alieleza kuwa, ingekuwa wazazi wana mashirikiano kama ilivyokuwa zamani
basi suala la utoro lisingekuwepo na watoto wangekwenda skuli kupata elimu.
‘’Zamani nilikuwa nikimkuta mtoto
anazurura nampeleka skuli na bakora mbili nampiga, siku ya pili hasubiri
kuambiwa, lakini mtoto wa leo ukimuuliza tu hujaenda skuli au madrasa kwa nini,
mzazi wake anakujia juu na kukuambia kwani unampa kula yako huyu? Kwa kweli
hatuendelei,’’ alieleza baba huyo.
Nae Hadia Ali Hamad alieleza kuwa, ipo
haja ya kuwa na mikakati maalumu pamoja na sheria ndogo ndogo katika shehia
yao, ili mtoto akionekana anazurura wakati wa skuli au madrasa apelekwe kwa
lazima na endapo mzazi wake atakaidi basi achukuliwe hatua.
‘’Tutakapofanya hivi itasaidia sana
watoto kupata elimu na kuziondoa familia katika dimbwi la umasikini, kwa sababu
ikiwa huna elimu unakuwa na umasikini wa mawazo, kifikra na umasikini wa
kipato, hivyo unakosa fursa za kujiendeleza kimaisha,’’ alifafanua mama huyo.
Mratibu wa wanawake na watoto shehia
hiyo Khadija Henock Maziku alisema, utoro katika shehia yao upo kwa kiasi
kikubwa kutokana na kuwa wazazi kutokuwashughulikia watoto wao na wanapoambiwa
wanakuwa wakali.
Alifahamisha kuwa, iwapo watoto
wataendelea kutoroka skuli na madrasa, shehia yao itakuwa haina maendeleo kwa
sababu watajiingiza katika makundi ya wizi, utumiaji wa madawa ya kulevya na
kujiingiza kwenye ajira za kukata matofali na kuchimba mawe.
Sheha wa shehia hiyo Hamad Said Mgau alisema
kuwa, wameunda kamati wa skuli na wamekuwa wakilizungumzia kwa kila suala la
utoro na namna ya kulidhibiti, ambapo kwa hatua ya mwanzo wamewaomba walimu
wakuu kuwapa majina ya wanafunzi wote watoro ili kuwafuata majumbani mwao.
Mwalimu Mkuu wa skuli ya Sekondari Kangagani
Omar Kombo Hamad alisema, skuli hiyo inachukua wanafunzi wa shehia ya Mjiniole
na Kangagani ambapo baadhi yao wamekuwa watoro sana licha ya kuwapa adhabu ya
bakora na adhabu mbadala.
‘’Tunawapiga bakora mbili au tunawapa
adhabu mbadala lakini bado hali ni mbaya, ila utoro zaidi unachangiwa na wazazi
kwa sababu anamuona mtoto wake amekaa nyumbani hamuulizi na wala sisi hapewi
taarifa kwamba ana dharura au la,’’ alieleza mwalimu huyo.
Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Amali Pemba Mohamed Nassor Salim alisema, Wizara ina mikakati mbali
mbali kuhakikisha wanadhibiti utoro kwa wanafunzi ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa
kampeni maalumu ya kuwarudisha wanafunzi watoro skuli, ambapo kwa sasa
wameshawarudisha wanafunzi elfu 31,000 kati ya 35,000 waliokuwa nao kwa Unguja
na Pemba.
Aidha alisema kuwa, mkakati mwengine ni
kuongeza madarasa na matundu ya vyoo kwa sababu wakati mwengine watoto
wanapokwenda vichakani kujisaidia hawarudi tena skuli, ambapo kwa sasa
wanatarajia kuongeza matundu 60 katika skuli mbali mbali kisiwani Pemba.
‘’Pia tunaajiri walimu ili waweze
kuwazibiti wanafunzi, kwa sababu wanapokuwa wachache wanashindwa kuwadhibiti watoto
na hatimae wanakuwa watoro, mwaka jana tumeajiri walimu 1,444 na mwaka huu
tunataraji kuajiri walimu wasiopungua 400, pia tunashirikiana na OCD
kuhakikisha tunadhibiti hali hii,’’ alifafanua.
Afisa Mdhamini huyo aliwataka wazazi
kushirikiana pamoja na Serikali katika suala la kumpatia mtoto elimu, kwani
ndio urithi pekee utakaodumu na kumletea maendeleo katika maisha yake ya baadae.
MWISHO.
Comments
Post a Comment