Na Salma Lusangi ,New York @@@@
Licha ya changamoto za
kiuchumi Duniani, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweza
kutekeleza hatua mbali mbali zilizolengwa ili kupunguza athari kwa wanawake, na
kuimarisha dhamira ya Utekelezaji wa Jukwaa la Beijing
na ahadi ya Kizazi chenye Usawa.
Kauli hiyo imetolewa
katika mkutano wa Hadhi ya Wanawake (CSW68) uliyofanyika wiki iliyopita katika
ukumbi wa Umoja wa Mataifa New York Nchini Marekani na Waziri wa Maendeleo ya
Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma wakati akitoa taarifa ya
utekelezaji masaula ya wanawake na
wasichana nchini Tanzania.
Amesema hivi karibuni
Tanzania ilizindua Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Jinsia na Wanawake (2023)
iliyopitiwa upya, ambayo pia inaangazia Bajeti inayozingatia Jinsia kama nyenzo
muhimu ya kutathmini athari za kijinsia za sera ya uchumi mkuu na sera za
fedha, kwa kutambua athari zake katika ukuaji wa uchumi, maendeleo ya
rasilimali watu na ajira kwa usawa.
Mhe, Riziki ametoa
taarifa hiyo kulingana na mada ya mkutano huo ambayo imesema: kuharikisha
upatikanaji wa usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote
kwa kukabiliana na umaskini na kuimarisha taasisi na fedha kwa mtazamo wa kijinsia.
Hivyo ameeleza Serikali
ya Tanzania imetenga rasilimali zaidi kwaajili ya kushughulikia usawa wa
kijinsia katika sekta zinazoathiri moja kwa moja ustawi wa wanawake na
wasichana. Amesma hasa, bajeti ya Wizara yenye dhamana ya Jinsia, katika Mwaka huu wa Fedha 2023/24 mgao wa
bajeti uliongezeka kwa asilimia 71 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Alifahamisha kwamba Benki
Kuu ya Tanzania imeanzisha Chombo cha ufadhili wa takriban Dola za Kimarekani
Milioni 400 kwa benki na taasisi za fedha kupata riba ya asilimia 3%. Bchombo hicho
kimeongeza fedha katika sekta ya kilimo ambapo asilimia 50.3 ya wanawake
wanaajiriwa katika sekta ya kilimo.
Amefafanua kwa kusema utoaji wa mikopo hiyo umepewa kipaumbele kwa
wanawake wa vijijini ambapo zaidi ya asilimia 35 ya fedha zote zimetengwa kwa
wanawake katika sekta ya kilimo, ufugaji, ufugaji nyuki, kilimo cha mwani n.k.
Aidha alisema Serikali
pia inatekeleza sera ya elimu bila malipo na imeanzisha mpango wa kuwarejesha
skuli/shuleni wasichana waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali. Zoezi
la uandikishaji limeanza tangu mwaka 2020 na linaendelea hadi sasa, ambapo
uwiano wa shule za awali, msingi na sekondari kwa sasa ni 1:1 kati ya wavulana
na wasichana.
Amesema Jumla ya
wasichana Milioni 29.5 wamefaidika na elimu bila malipo, na juhudi kama hizo
zinaendelea ili kuhakikisha kuwa ongezeko la uandikishaji wa elimu linaleta
kazi nzuri kwa wanawake na wasichana katika soko la ajira.
Pia amesema kwa kutambua
umuhimu wa kuziba pengo la usawa wa kijinsia
katika upatikanaji na matumizi ya teknolojia, Serikali pia inatekeleza Mpango
wa Udhamini wa Mama Samia unaotolewa kwa wanafunzi katika Vyuo vya Elimu ya Juu.
Alisema utekelezaji wa
programu shirikishi za hifadhi ya jamii, kama vile Mpango wa kupunguza ukali wa
umasikini Tanzania (TASAF) na Pensheni jamii kwa Wazee wa Zanzibar, inasisitiza
mbinu ya kina ya uwezeshaji wa kiuchumi Tanzania.
Comments
Post a Comment