Skip to main content

MANENO 'SHINANI, SHIMONI' YAWAWEKA HURU WALIODAIWA KUKUTWA NA BANGI PEMBA

 



NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

MAHAKAMA kuu Zanzibar kanda ya Pemba, imewaachia huru Akida Mbega Bakari (33) na Rashid Rajab Ngoji (32), waliyokuwa wakikabiliwa na tuhma za kupatikana na misokoto 340 ya iliyodhaniwa kua ni bhangi, baada ya ushahidi uliotolewa, kutowaunganisha na makosa yao.

Aliyeaachia huru watuhumiwa hao ni Jaji Ibrahim Mzee Ibrahim wa Mahakama hiyo, ambapo alitoa uamuzi huo, baada ya kusema ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, kwenda kinyume na hati ya mashitaka.

 Alisema, pamoja na upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi saba mahakamani hapo, lakini ushahidi wao umeshindwa kuthibitisha kwamba, kosa hilo lilifanyika sehemu ambayo hati ya mashitaka ya washitakiwa imeitaja.

Alisema ushahidi uliotolewa na mashahidi wote saba, kutoka upande wa mashitaka, unaonyesha kwamba washitakiwa walitenda kosa hilo eneo la Machomane Shimoni, ambapo hati ya mashitaka inaonyesha kwamba, walitenda kosa hilo Machomane Shinani.

Jaji Ibrahim alisema kuwa, hivyo sehemu iliyotajwa katika hati ya mashtaka ‘charge sheet’ ni tofauti na sehemu ilioainishwa na mashahidi wa kesi hiyo, wakati walipofika mbele ya mahakama hiyo kutoa ushahidi wao.

Awali Mwendesha mashitaka na Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Asya Ibrahim Mohamed, aliiambia mahakama kuu kua, kesi hiyo ipo kwa ajili ya kutolewa hukumu.

Aliieleza mahakama hiyo, baada ya wao kufunga ushahidi mwezi uliopita na kumalizika kwa mashahidi kwa upande wa utetezi, sasa kwa leo (jana), ni zamu ya mahakama kutoa ushahidi.

‘’Mheshimiwa Jaji, leo (jana), kesi iliyoko mbele yako, ni kwa ajili ya kutolewa hukumu, na tayari watuhumiwa hao wameshafika mahakamani hapa,’’alidai Wakili huyo.

Washtakiwa hao awali, walikua wakikabiliwa na shitaka la kupatikana na dawa za kulevya aina ya bhangi, kinyume na kifungu cha 21(1) (d) ya sheria ya Mamlaka ya Kudhibiti na kupambana na dawa za kulevywa Zanzibar, sheria namba 8 ya mwaka 2021 sheria za Zanzibar.

Walidaiwa kua Novemba 25, mwaka 2022, majira ya saa 5:00 asubuhi, eneo la Machomane Shinani, walipatikana na misokoto 340 ya bhangi yenye uzito wa gramu 961.91, ambapo kufanya hivyo ni kosa kisheria.

                 Mwisho

 

Comments