NA FATMA HAMAD, PEMBA
……………..SIRI
ya mtungi aijuaye ni kata………
……Wahenga wengine wakasema hasira hasara…...
Misemo yote hii inasadifu mno pale ndoa inapovunjika
baada ya wana ndoa kuamua lipasuke tugawane mbao.
Ingawa misumari ya hizo mbao, huwachoma na kuwaumiza
wengi, wakiwemo wana familia na hasa watoto wao.
Mara nyingi pale wazazi wakiwa wametengana, baada ya
ndoa kuvunjika watoto hukosa huduma muhimu za maisha na kuathirika kimwili na
kiakili.
Mwana harakati maarufu wa kulinda na kutetea
haki za watoto kisiwani Pemba,Tatu Abdala Msellem, mara kwa mara amekuwa akitoa
tanbihi kuwa, kuvunjika kwa ndoa isiwe sababu ya kila mzazi kufumbia macho
wajibu wake wa malezi ya watoto.
Hii ni kwa sababu, mtoto anapokosa
huduma za lazima sio tu huwa mnyonge na kujiona kama yatima, bali huwa hana
furaha anapocheza, na akili yake huwa haifuatilii vizuri masomo.
‘’Kama ndoa imevunjika, kwanini watoto
waingizwe katika shida wakati wao sio walioingia kwenye mkataba wa ndoa, wala
kupelekea wazazi watenngane,’’anahoji.
Sheihk Said Ahmad Mohmed kutoka Ofisi ya Mufti
kisiwani Pemba, aliwataka wanaume wasimame kwenye nafsi zao, watulize akili zao
na inapobidi ndoa kuparaganyika, basi waelewe bado wanayo dhima ya kuhakikisha
watoto wanapata huduma zote muhimu.
’Ndoa ikifikia mwisho wake kwa kuvunjika ,sio
kuvunjika kwa wajibu wa kulea na kuhudumia watoto, kwa mke huduma zinapaswa
kuendelea mpaka inapomalizika eda, lakini kwa watoto lazima ziendelee kwa
ukamilifu,’’ anafafanua.
Rashid Said Nassor, Afisa Hifadhi ya Watoto Wilaya
ya Chake chake anashangaa kuona inapovunjika ndoa, wathirika wakubwa wawe
watoto wakati wao hawakuhusika na kutengana kwa hao wana ndoa?
WATOTO WANASEMAJEE
Mwanafunzi mmoja wa
darasa la kwanza wa Skuli ya Kangagani, nilimkuta akiwa kwao nyumbani kwa
takriban wiki mbili akiwa amepiga kambi kwenye eneo la
uvunjaji wa kokoto bila ya kuhudhuria masomoni.
Akinieleza kilichomsibu
kuwa, amelazimika kufanya kazi hio ya sulubu, ili ajipatie mahitaji ya
shuleni na nyumbani kwao, baada ya baba yao kutowajali kimaisha na
kisha kuingizwa kwenye dimbwi la utelekezaji.
‘’Kwa sasa nabanja
kokoto, ili kujipatia vifaa vya skuli, kama viatu na sare, kwani mama yangu
hapatiwi huduma na baba yangu’’, anasema.
Mtoto huyu anaeleza
kuwa, sasa ni mwaka wa saba hajaitia machoni
sura ya baba yake, na amekuwa akisikia tu habari zake kutoka kwa mama yake,
lakin hamjui kwa sura.
‘’Nasikia baba yangu anaishi Unguja, lakini
sijawahi kumuona wala kupata huduma yake yoyote, tena kwa wadogo zake, (baba
mdogo na mkuu),’’anasimulilia.
Kwa hivyo ikifika
karibu na kipindi cha sikukuu za kiimani, huenda kubanja kokoto kwa ajili ya
kujinunulia nguo n ahata kumsaidia mama yake chakula,’’analeza.
Mtoto Juma mwenye umri
wa miaka [15] mkaazi wa Mjini Wingwi (hilo sio jina lake halisi), anaefanya
kazi ya uvuvi wa samaki, amesema baba yao amewatelekeza takriban kwa miaka
minane sasa na hawaulizi cha asubuhi wala cha jioni.
‘’Nimejingiza kwenye
shughuli hizi za uvuvi, ili nipate fedha kwa ajili ya matumizi ya nyumbani
kwetu na mimi binafsi,’’anasema.
Ali Khamis Kombo mwenye umri wa [15] mkazi wa
kijiji cha Mijini Kiuyu aliacha kusoma na kufanya shughuli ndogo ndogo za
kibiashara, kwa ajili ya kumsaidia mama yake, baada ya kubaina baba yake hana mpango
nao.
‘’Nyumbani tuko watoto sita (9), na mama hana
kazi yoyote, hivyo nafanya kazi ili niendeshe familia yangu baada ya baba kutupa
kisogo cha kutuhudumia,’’anafafanua.
WAZAZI WANASEMAJE
Asha Ali, mkaazi wa Mjini Kiuyu Wete Pemba,
mwenye watoto tisa anasema, huduma zote anajitegemea, ingawa bado yuko
kwenye ndoa ya mume alieongeza mke wa pili hivi karibuni.
‘’Sio kama naona raha mwanangu kufanya
biashara, lakini nitafanyaje sasa, sina budi ila kumtaka anisaidie kimaisha na
anafanya hivyo,’’anassimulia.
Bikombo Khamis mkaazi wa mjini Wingwi anaeleza
kuwa, mume wake aliondoka kwenda uvuvini [dago ] Dar es- Saalam karibu miaka
minane sasa iliopita, na hurudi wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani
pekee.
‘’Ameniachia watoto wanane
[8] na huenda pwani na watoto wangu
kupanda mwani, ili tupate pesa za kujinunulia mahitaji, mana baba
yao amenitelekeza,’’anafahamisha.
Mratibu wa wanawake na watoto wa Shehia
ya Kangagani, Awena Salim Kombo, anaesema wanawake wengi walioachiwa mzigo wa
ulezi peke yao, huwauzisha biashara watoto wao, ili wapate chakula.
‘’Ukimuuliza mama kwa nini hawa watoto
hawaendi skuli na madarassa na badala yake wanatembeza biashara, anakwambia
afanye nini na hana uwezo wa kuwahudumia,’’anaeleza.
SHERIA
MBALI MBALI
Sheria
ya Ajira na Mahusiano Kazini nambari 8 ya mwaka 2005 inakataza mtoto mwenye
umri wa chini ya miaka 14, kuajiriwa na kukataza ajira kwa watoto wa chini ya
miaka 18, katika maeneo ya migodi, viwanda, ubaharia katika meli au kazi
nyingine yeyote inayotambulika kuwa hatarishi.
Hata
hivyo, sheria inaruhusu ajira kwa watoto wa miaka 14 katika kazi nyepesi,
ambazo sio hatarishi kwa afya yake, lakini haiathiri mahudhurio ya watoto masomoni.
WANAHARAKATI
WANASEMAJE
Semeni Ali Khamis, mwanaharakati kutoka
Jumuiya ya Wanawake katika wilaya ya Micheweni, anaeleza kuwa watoto wengi
wanaojiajiri ni wale ambao kuwa hawapati matunzo, kutoka kwa wazazi wao.
‘’Katika kijiji cha Konde baadhi ya wanaume
hujiingiza kwenye masuala ya ulevi tu, hawana habari ya kushughulikia familia
zao,’’analeza.
Fat-hiya Mussa Said Mratibu wa Chama cha
Wandishi wa habari wanawake Tanzania [TAMWA] ofisi ya Pemba, anasema anapoachwa
mwanamke anaachwa na watoto wote kihuduma, hivyo shida na
dhiki zinawakumba zaidi watoto.
‘’Utawakuta watoto
muda wa kuwepo masomoni wamebebeshwa mabakuli ya Mchicha, chaza, kwa ajili ya kutembeza
mitaani, jambo ambalo linasababisha kufanyiwa udhalilishaji hapo baadae,’’
anasema.
OFISI YA MUFTI
Afisa kutoka Ofisi ya
Mufti iliopo Pemba, Abdalla Muhamed Abdalla, anasema utelekezaji wa wanawake
unachangia kwa kiasi kikubwa watoto kujiingiza katika ajira.
Kwa bahati mbaya, siku
hizi kumekuwa na ongezeko la talaka ambapo kwa kipindi cha
Juni hadi Agosti mwaka 2023, kupitia ofisi ya Mufti wamepokea
maombi 18 ya talaka, na malalamiko tisa (9) ya utelekezaji wa familia.
Alisisitiza ni vyema
watoto, wakapatiwa huduma muhimu na malezi ya familia ili wakuwe vizuri kwa
faida ya taifa kwa ujumla.
Naibu Waziri, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu wa Jamuhuri ya Mungano
wa Tanzania, Patrobas Katambi, amesema serikali haitavumilia
kuona watoto wanakosa haki zao za msingi .
‘’Ni kosa kuajiri watoto kinyume na sheria inavyosema
na adhabu inatolewa chini ya kifungu cha 102 (2) ambacho kinampa Hakimu kutoa
adhabu sawa na faini isiyozidi shilingi milioni 5 au kifungo cha mwaka mmoja au
vyote,’’ anafafanua.
Kwa mujibu wa
takwimu kuna watoto milioni 152 wanatumikishwa duniani hivi sasa na
kati yao 25,803 ( asilimia 5.6) wapo katika ajira Zanzibar.
Hali hii imebainishwa katika
taarifa ya Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik
Ramadhan Soraga, katika maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Ajira za watoto
mjini Zanzibar.
Siku hii huadhimishwa rasmi kila
ifikapo Juni 12 ya kila mwaka.
KITENGO
CHA HIFADHI YA MTOTO
Kwa mujibu wa takwimu za kitengo cha hifadhi ya
mtoto Pemba katika wilaya ya Micheweni kwa mwaka 2022, malalamiko yalioripotiwa
ya utelekezwaji wa wanawake ni 71, ambapo yamehusisha watoto 185, wanawake 92
na wanaume 93.
Kuanzia mwezi Januari hadi Agosti
mwaka 2023 malalamiko yaliyopokelwa ni 28,watoto walioripotiwa kutelekezwa ni
84 ( wanaume ni 49 na wanawake 35).
Shirika la Kazi Duniani (ILO)
linakadiria kuwepo watoto 152 milioni katika ajira
duniani na kati yao 73 milioni wamo katika
kazi ambazo ni hatari.
Karibu asilimia 70 ya
ajira hizi za watoto ni katika kilimo na sababu kubwa ni
kutokana na umasikini na ugumu wa wazazi kupata ajira zenye hadhi.
Sheria ya Elimu Zanzibar ya 1982,
kifungu cha 20, cha sheria hiyo kinamtaka kila mzazi kuhakikisha anampatia
mtoto wake elimu ya lazima, pale anapofikia umri wa miaka saba.
Katiba ya Zanzibar ya
1984, inaeleza wazi katika kifungu cha 15[1] kuwa kila mtu ana stahili
kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafasi yake, maisha yake binafsi naya
nyumbani kwake, na pia heshima na hifadhi ya maskani yake na mawasiliano yake.
Nacho kifungu cha
12[1] kikasisitiza kuwa, watu wote ni sawa mbele ya sharia, na wanayo haki, bila
ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.
MIKATABA
Kwa mujibu wa Mkataba
wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto wa mwaka 1999, Ibara ya15, kinafafanua
kuwa, mtoto ana haki ya kulindwa dhidi ya kazi au ajira zitakazoathiri afya,
elimu na maendeleo yake.
Serikali inatakiwa
kuweka sheria za kima cha chini cha mshahara, muda wa kufanya kazi,
mazingira ya kazi na adhabu kwa wasio tekeleza haki hii.
Mkataba wa Umoja wa
Mataifa wa Haki za Mtoto wa mwaka 1989 ibara ya 32, kinaeleza mtoto ana haki ya
kulindwa dhidi ya kazi au ajira zitakazoathiri afya au elimu yake.
Mwisho
Comments
Post a Comment