NA HABIBA ZARALI, PEMBA@@@@
SHIRIKA la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) limekabidhi vifaa vyenye thamani ya shilingi 53,900,000 kwa ajili ya kusaidia uoteshaji wa miche ya mikarafuu kwa wizara ya kilimo na baadhi ya wakulima kisiwani Pemba.
Vifaa hivyo vilivyokabidhiwa ni pamoja vyandarua vya kivuli 35, roli ya vifuko vya kuatikia miche kilogramu 3100 pamoja na fedha taslimu shilingi milioni mbili kwa ajili ya ununuzi wa matende ya mikarafuu.
Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa makabidhiano hayo, Mkurugenzi wa Mfuko wa Karafuu wa Shirika la ZSTC Ali Suleiman Mussa kwa niaba ya Mkurugenzi Mwezeshaji wa shirika hilo alisema vifaa hivyo vitasaidia upatikanaji wa miche ya mikarafuu kwa wingi na kuondowa usumbufu kwa wakulima.
Alifahamisha kuwa shirika la ZSTC linathamini na kuwajali sana wakulima wa zao la karafuu kutokana na umuhimu wao wa kulikuza zao hilo ambalo ni tegemeo katika kukuza uchumi wa taifa.
Alieleza kuwa shirika hilo litaendelea na jitihada zake zote kuhakikisha linawainuwa wakulima hao ili waweze kupata nguvu zaidi wa kuliendeleza na kuinuwa kipato cha wananchi na nchi yao kwa ujumla.
"Vifaa hivi hatukuvielekeza kwa wizara ya kilimo pekee bali tumewaangalia na wakulima wetu ili nao waweze kuatika miche hii kwa wingi na kuondokana na matatizo yasiyo ya lazima wanapohitaji miche ",alisema.
Mapema akipokea msaada huo Mkuu wa Idara ya Kilimo Pemba Asha Omar Ali kwa niaba ya Ofisa Mdhamini wa wizara ya Kilimo Pemba, alisema vifaa hivyo vitawasaidia sana katika shughuli zao za uoteshaji wa miche kwani baadhi ya vifaa vyao ikiwemo vyandarua vilikuwa vimeshachakaa
Aidha Mkuu huyo alibainisha kuwa, changamoto kubwa waliyonayo ni uhaba wa mabwana shamba, hivyo aliwataka wakulima kuendelea kuwatumia mabwana shamba waliopo mpaka pale tatizo hilo litakapotatuliwa.
Akizungumzia suala la ugawaji wa miche ya mikarafuu kwa wakulima, Afisa huyo alieleza kuwa hivi sasa wamekuwa na mpango mzuri kuhakikisha wakulima wa zao hilo wanapata miche hiyo.
"Kwa sasa mpango tulionao wakuwapatia wakulima miche ya mikarafuu ni kupata orodha ya idadi ya wakulima kutoka kwa masheha, ndipo tuanze kugawa miche hiyo," alisema.
Alieleza kuwa, matarajio yeo ni kuona uzalishaji wa miche ya mikarafuu inaongezeka kwa wingi, ili na wananchi wapate miche mingi itakayosaidia kupata zao la karafuu kwa winging hapo baadae.
Nae mkulima aliyepata vifaa hivyo Abdalla Mohamed Salim wa Kijiji cha Kuungoni Wilaya ya Micheweni alisema ni matarajio yake kufanya kazi ya uoteshaji miche ya mikarafuu ili kufikisha malengo yaliyokusudiwa na shirika ikiwemo kuliimarisha zao la karafuu na kuleta maendeleo ya nchi.
" Hapo nyuma nilikuwa na changamoto ya vifaa kwani havikuwepo Pemba ilibidi nivifuata Bara lakini sasa nitazalisha miche zaidi ya ile niliyokubaliana na shirika kwani sina sababu vifaa nnavo"alisema.
Nae Mwenyekiti wa kikundi cha ushirika cha umoja wa Tangaani Wilaya ya Mkoani Abdalla Ali Salim baada ya kupokea vifaa hivyo aliahidi kuvifanyia kazi kwa malengo yaliyokusudiwa na kuliomba shirika la ZSTC kuendelea na ushirikiano wa kuwatembelea mara kwa mara ili kujuwa matatizo yanayowakabili katika kilimo cha karafuu.
Hivyo aliiomba Serikali kuwapekekea mabwana shamba mara Kwa mara ili waweze kuwatatulia changamoto zinapotokezea katika kilimo hicho.
MWISHO.
Comments
Post a Comment