IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
MKAGUZI wa shehia ya Mjananza Wilaya ya Wete Inspekta wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Khalfan Ali Ussi amewataka wazazi na walezi kushirikiana katika kusimamia malezi ya watoto ili wakue katika maadili mema na kuhakikisha wanapata haki zao za msingi.
Akizungumza katika muendelezo wa ziara zake ya kutoa elimu nyumba kwa nyumba kwa ajili ya kudhibiti uhalifu, Mkaguzi huyo alisema watoto wanapaswa kukua katika maadili mema hivyo ni vyema wakawasimamia ili kuhakikisha hawaharibikiwi kwenye maisha yao.
Alisema kuwa, urithi pekee wa mtoto utakaomsaidia katika maisha yake ni malezi bora, elimu na afya njema, hivyo wazazi na walezi wahakikishe wanasimamia vyema kuhakikisha watoto wanapata haki zao hizo kwa ajili ya maendeleo yao ya baada
Aidha aliwaomba wazazi hao kuwalinda na kuwa karibu na watoto wao ili wasifikwe na janga la udhalilishaji na ikiwa litawakuta basi wawe na moyo wa ujasiri kuwaelezea kile kinachowakuta na kuweza kuchukua hatua za haraka.
"Msiwe wakali kwa watoto wenu kwa sababu wanakuogopeni na mwisho wa siku wakipata matatizo wanashindwa kusema, hivyo muwe na kawaida ya kutenga mda kuwasikiliza," alisema.
Alieleza kuwa, lengo la kufanya ziara hiyo ya nyumba kwa nyumba ni kuona kwamba katika shehia zote anazozisimamia zinaondokana na uhalifu ili wananchi waishi kwa amani.
Alisema kuwa, pia katika shehia hiyo wameanda kanuni ndogo ndogo kwa ajili ya kuwadhibiti wahalifu, hivyo ni vyema waache muhali ili atakapopatikana muhalifu afikishwe kwenye vyombo vya Sheria kuwajibishwa.
Wanafamilia ya Juma Bakar Hamad walimshukuru Mkaguzi huyo kwa hatua zake za kupita nyumba kwa nyumba katika kuhakikisha vitendo vya kihalifu vinaondoka katika jamii.
Walisema kuwa, wataendelea kushirikiana bega kwa bega ili kuona kwamba vitendo hivyo kihalifu havitokei tena kwenye jamii sambamba na kuwashauri wananchi wenzake kuwasimamia watoto wao na kuwapa huduma stahiki.
"Changamoto tuliyonayo kwa sasa katika shehia yetu ni utoro, watoto hawataki kwenda madrasa hali ambayo inatuuma sana kwani ikiwa hawakwenda hawajui mungu wao na wala hawajui katika maadili mema.
MWISHO.
Comments
Post a Comment