IMEANDIKWA NA
ZUHURA JUMA, PEMBA
WANAFUNZI 274 wa skuli ya msingi Minungwini wilaya ya Wete Pemba, wanaendelea kusoma chini ya miti baada ya vyumba vinne vya madarasa walivyokuwa wakitumia kuchimbuka na kuvuja kwa muda wa zaidi ya miezi sita sasa.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wazazi na walezi wenye watoto skulini hapo walisema, wanafunzi hao wanaendelea kukosa mtiririko mzuri wa masomo kutokana na kutumia eneo hilo kwa siku za kiangazi pekee huku siku za mvua zikiwa ni changamoto.
Wazazi hao walisema kuwa, kutokana na kuharibika kwa madarasa hayo wana hofu ya kuporomoka kwa elimu skulini hapo kutokana na changamoto ya wanafunzi hao kusoma chini ya miti.
Mmoja kati ya wazazi hao Fatma Jaffar Faki alisema kuwa hali hiyo haimpi usingizi kutokana na watoto wao kutokuwa na mazingira rafiki ya kusomea.
"Tunapenda watoto wetu wapate elimu bora lakini kwa hali hii ya kuwekwa chini ya miti ni mtihani kwa sababu wakati wa upepo ni hatari, kwani hata tawi linaweza kukatika na kuwaangukia," alisema.
Mzazi Asha Omar Rashid ameiomba Wizara ya elimu kuchukua hatua za haraka kujenga ili kuwarejesha wanafunzi madarasani.
Akizungumzia kuwepo kwa vyumba hivyo chakavu alisema, vinaweza kuhatarisha maisha ya wanafunzi, walimu na wapita njia.
"Banda hili lina hatari mbili, moja ya wanafunzi kukosa kulitumia na nyengine linaweza kuwaangukia kwa sababu kuta zimeinama na zimepasuka, ikinyesha mvua viambaza huroana na watoto kama tunavyowajua pale kwenye hatari ndipo wanapokimbilia kucheza,’’ walisema.
‘’Tunaamini kwamba Serikali italijenga banda hili lakini
hofu yetu kwa sasa ni kuja kuanguka ghafla na watoto muda wote wapo karibu,
hivyo hata kama bado kujengwa basi tunaomba livunjwe,’’ walisema.
Mwalimu Mkuu skuli hiyo Ahmada Ali Omar alisema, ubovu wa banda hilo umesababisha wanafunzi 274 kukosa sehemu ya kukaa na badala yake wanawaweka chini ya miti, ili kuhakikisha na wao wanapata elimu kama kawaida.
Alieleza kuwa wameshalifikisha wizarani suala hilo na tayari viongozi wameshakwenda kulikagua, hivyo wanatarajia litajengwa na wataendelea kulitumia baada ya kumalizika.
‘’Chini ya miti ni hatari kwa sababu siku za upepo
kuna vumbi na pia tunahofia kukatika kwa matawi na kuwaangukia, vile vile siku
za mvua hatuna pakuwaweka, hivyo ni hatari kwa kweli,’’ alieleza mwalimu huyo.
Mwalimu huyo anawashukuru sana viongozi wao wa Serikali,
majimbo na shehia kwa ushirikiano wanaouonesha katika kuhakikisha wanapeleka
maendeleo ya elimu mbele.
Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
Pemba Mohamed Nassor Salim alisema kuwa, changamoto hiyo wameiona ambapo wana
mpango wa kujenga skuli ya ghorofa pamoja na kuyafanyia ukarabati madarasa
chakavu, ili kuondosha tatizo hilo.
‘’Kujenga skuli na madarasa ni maelekezo ya Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwamba
wanafunzi waende skuli mkondo mmoja tu, ili wapate kwenda madrasa na pia kila
darasa liwe na wanafunzi 45 tu ili kupunguza msongomano wa wanafunzi ambao
husababisha wanafunzi kutofahamu vizuri,’’ alisema.
Aidha aliipongeza skuli hiyo kwa kutoa ufaulu mzuri
kwa wanafunzi wao, ambapo umetokana na ushirikiano mzuri kati ya wazazi, kamati
ya skuli, walimu na Serikali kupitia Wizara na kuwataka kuendeleza
mashirikiano, ili kuongeza kiwango cha ufaulu.
‘’Hivi karibuni Waziri wetu wa elimu alinipa fedha
shilingi laki tatu ili niwapatie zawadi wanafunzi watatu waliofaulu kwa kupata
alama ‘A’, hii ni motisha kwa wanafunzi wengine kufanya vizuri,’’ alifafanua.
Skuli ya msingi Minungwini ina wanafunzi 2,277 na
walimu 42, ambapo wanakwenda mikondo miwili asubuhi na mchana.
MWISHO.
Comments
Post a Comment