UTAFITI: WATANZANIA WAUNGA MKONO KUPUNGUZA UZALISHAJI GESI METHANE KUSHUGHULIKIA MABADILIKO HALI YA HEWA
NA MWANDISHI WETU,
Watanzania wameonekana kuunga mkono kwa kiasi kikubwa mipango inayolenga kupunguza uzalishaji wa gesi ya methane na kushughulikia mabadiliko ya hali ya hewa. Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Global Methane Hub, shirika la kibinadamu linalojitolea kupunguza uzalishaji wa methane duniani.
Utafiti huo, ambao ulijumuisha nchi 17
katika mabara sita, umetoa ufahamu wa jinsi jamii inavyoiona hali ya mazingira
na njia za kisheria za kurekebisha hali hiyo. Matokeo ya utafiti huo yanaonesha
kwamba asilimia 83 ya washiriki kutoka Tanzania wanapendelea sera zinazolenga
kupunguza uzalishaji hatari wa methane, na kati yao, asilimia 49 wanatoa
uungaji mkono mkubwa, kiwango ambacho ni cha juu zaidi kuliko nchi nyingine
zilizofanyiwa utafiti.
Zaidi ya hayo, asilimia 87 ya Watanzania
wanaamini kwamba shughuli za binadamu ndio sababu kuu ya mabadiliko ya hali ya
hewa, ikionesha ufahamu mkubwa wa umuhimu wa kuchukua hatua za kupunguza athari
hizo. Utafiti huo pia unaonesha kwamba asilimia 88 ya washiriki kutoka Tanzania
wanapendelea sheria zinazolenga kupunguza upotevu wa chakula na utupaji sahihi
wa taka za kikaboni, ambazo ni moja ya vyanzo vikuu vya uzalishaji wa methane.
Kwa mujibu wa Marcelo Mena, Mkurugenzi
Mtendaji wa Global Methane Hub, “kupunguza uzalishaji wa methane ni njia ya
haraka zaidi ya kupunguza ongezeko la joto duniani na kudhibiti athari za
mabadiliko ya hali ya hewa.”
Utafiti pia unaonesha kwamba wale
wanaoathiriwa zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa ndio wanaotoa uungaji mkono
mkubwa kwa jitihada za kupunguza methane.
Utafiti huo unathibitisha pia kwamba
uungaji mkono wa mikakati ya kupunguza gesi ya methane umebaki imara licha ya
tofauti katika ufahamu wa awali wa gesi hiyo katika nchi zilizofanyiwa utafiti.
Hata hivyo, wasiwasi mkubwa pia umeelekezwa kwa suala la ubora wa maji, ambapo
asilimia 76 ya washiriki kutoka Tanzania wameripoti wasiwasi mkubwa kuhusu hilo.
Natalie Lupiani, ambaye ni Makamu wa Rais
wa kampuni ya BSG, anasisitiza kwamba data hizi ni ishara nzuri kwamba watu
wanaunga mkono serikali zao katika kuchukua hatua za kuwalinda dhidi ya
ongezeko la joto duniani. Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi tatu
zilizoathiriwa zaidi, pamoja na Brazil na Kenya, huku karibu nusu ya washiriki
wakiripoti athari kali katika maisha yao ya kila siku.
Mwenyekiti wa Jopo la Kitaalam la Sayansi
la Hali ya Hewa na Hewa Safi (The Climate
and Clean Air Coalition Scientific Advisory Panel), Drew Shindell, amesisitiza
umuhimu wa kupunguza uzalishaji wa methane mara moja ili kuzuia jamii dhidi ya
athari mbaya za uchafuzi wa hewa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Ripoti inaonesha kuwa kupungua kwa kiasi
kikubwa katika ongezeko la joto kunaweza kutokea kupitia juhudi za kupunguza
methane kwa asilimia 45, ambayo itasaidia kuleta mustakabali bora na kufikia
malengo ya kimataifa ya hali ya hewa.
Utafiti huo pia unaonesha kwamba watu
duniani kote wanaona serikali za kitaifa, biashara, na watu binafsi kuwa wajibu
wa uharibifu wa mazingira, lakini kuna imani kubwa kwamba biashara kubwa na
serikali zinaweza kuleta mabadiliko muhimu katika kukabiliana na athari za
mabadiliko ya hali ya hewa.
Utafiti huu uliwafikia watu katika nchi 17
kote ulimwenguni kwenye mabara sita, ukikusanya data kutoka kwa watu wazima
12,976, takriban 750 kutoka kila nchi.
Comments
Post a Comment