IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
MWENYEKITI wa Bodi ya Takwimu Zanzibar balozi Amina Salim Ali amewataka viongozi wa dini kuisaidia Serikali katika kuwahamasisha wanandoa kusajili ndoa, zao.
Akizungumza katika mkutano wa usambazaji wa matumizi ya matokeo ya viashiria vya sensa ya watu na makaazi 2022 kwa viongozi wa dini alisema, wanandoa wengi hawana elimu ya kusajili ndoa, hivyo ipo haja kwa viongozi hao kuhakikisha wapofungisha ndoa, kuwahamasisha wanandoa kusajili ndoa zao katika mamlaka husika.
Alisema kuwa, watu wengi katika jamii hawajui kwamba wanatakiwa kupata cheti cha ndoa kwa maslahi yao na Serikali kwa ajili ya kuweka takwimu sawa, hivyo viongozi wa dini wana jukumu la kuisaidia Serikali katika kutoa elimu ili wanandoa wasajili na kupata cheti.
"Kwa kweli hatuna elimu hiyo kwa sababu tukipewa karatasi ya sheha au ya kutoka kwa sheikh tu basi tunatosheka na hilo, lakini kwa elimu tulioipata leo juu ya umuhimu wa cheti cha ndoa, tutakwenda kutengeneza, akinamama wenzangu tujitahidi kulifanya hili," alisema Balozi huyo.
Kwa upande wake Afisa Fat-twa kutoka Ofisi ya Mufti Pemba sheikh Said Ahmad alisema kuwa, kuna migogoro mengi inayotokana kwa kukosa cheti cha ndoa na talaka, hivyo imefika wakati wa kuondosha changamoto hiyo kwa kuwaelimisha wanajamii ili watafute.
"Hivi vyeti ni muhimu sana kwetu kwa sababu ikiwa huna kinaweza kukukosesha fursa kubwa na ukajutia kwa nini hukutafuta hapo mwanzo, ninazo kesi hizo kuna watu wapo nje ya nchi na amepata fursa lakini ili afanikiwe awe na cheti cha ndoa, kwa hiyo wanakosa fursa kwa hasa hapati kuja huku kutia saini," alifahamisha.
Aliishukuru ofisi ya takwimu kwa kuwapelekea mrejesho wa matokeo ya sensa, ambayo yamewasaidia kubaini changamoto kwenye jamii na pia kujua namna ya kupanga mambo yao ya kidini.
Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali Salum Kassim Ali alieleza kuwa, kupitia zoezi la sensa lililofanyika mwaka 2022 matokeo yalionesha kuwa takwimu za ndoa, talaka, vizazi na vifo zimekuwa na changamoto kutokana na baadhi ya wananchi kukosa vyeti, hivyo ndoa na talaka zisajiliwe ili takwimu ziende sawa.
Mapema washiriki hao walisema, Serikali iandae mpango wa upatikanaji wa vyeti vya ndoa na talaka kwa haraka, ili wananchi wasione shida kutafuta haki yao hiyo.
"Upatikana wa hivi vyeti ni shida hasa cha talaka na kuwafanya wanajamii wasione umuhimu wa kwenda kutafuta, hivyo Serikali iandae mpango utakasaidia upatikanaji wa vyeti haraka," alisema sheikh Yussuf Khamis Ali.
Nae mwalimu wa madrasa Ahmed Yahya aliishauri Serikali ihamasishe watu watafute vyeti vya talaka, ili ofisi ya takwimu ipate taarifa sahihi zinazoendana na vyeti vya ndoa.
Akifingua mkutano huo Kamisaa wa Sensa Zanzibar Balozi Mohamed Haji Hamza alisema, viongozi wa dini walitoa mchango mkubwa katika kufanikisha zoezi la sensa hivyo ni vyema wakaendelea kuwapatia elimu ili wananchi wapate vyeti vya ndoa, talaka, vizazi na vifo.
Mkutano huo umeandaliwa na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ambao umewashirikisha viongozi wa dini pamoja na walimu wa madrasa ukiwa na lengo la kurudisha shukrani kwao kufuatia zoezi la sensa ambalo walilifanikisha kwa kiasi kikubwa.
MWISHO
Comments
Post a Comment