NA HAJI
NASSOR, PEMBA@@@@
MWENYEKITI
wa Bodi ya Jumuiya ya Utetezi wa Mazingira na Jinsia Pemba ‘PEGAO’ Alhajji-Amran Massoud Amran, amewashauri wahamasishaji jamii
kudai haki zao za uongozi, demokrasia na siasa ‘Citizen bragged’ kisiwani
Pemba, kuelekeza nguvu zao ngazi ya vyuo, ili kuwaibua wanawake wenye nia ya
kugombea nafasi za uongozi.
Alisema,
wanafunzi wanawake ambao wanajitayarisha kuja kuitumikia jamii, wako katika
skuli za sekondari na vyuo vikuu, hivyo ni vyema kwa wahamasishaji hao, sasa
kuhamia katika eneo hilo kufanya uhamasishaji.
Mwenyekiti
huyo wa bodi, aliyasema hayo leo August 20, 2023 ukumbi wa mikutano wa Jumuiya
ya ‘KUKHAWA’ wilaya ya Chake chake, wakati akizungumza na wahamasishaji hao,
mara baada ya kuwasilisha utekelezaji wa shughuli zao, kwa kipindi cha miezi
mitatu iliyopita.
Alisema,
wanawake walioko ngazi ya elimu ya sekondari na vyuo vikuu, ndio tegemeo kubwa kwa
jamii, hivyo ikiwa watawezeshwa mapema, kuingia katika nafasi za uongozi,
itakuwa rahisi kwao, baada ya kumaliza masomo.
‘’Kwanza
nipongeze kazi yenu kubwa ya kuzipitia shehia mbali mbali hata zile za
visiwani, kwa lengo la kuihamasishaji jamii, kudai haki zao za uongozi, lakini
msisahau kupitia na vyuoni,’’alipendekeza.
Katika
hatua nyingine, Mwenyekiti huyo wa Bodi ya ‘PEGAO’ Alahajji-Amran Massoud
Amran, alisema bado elimu zaidi inahitajika kwa jamii, ili imuamini mwanamke
kwenye safu ya uongozi.
Hata
hivyo alisema, juhudi zinazofanywa kwa pamoja kati ya PEGAO, ZAFELA na TAMWA
zinafaa kuungwa mkono, kwani inakuja kuchapuza ukuaji wa demokrasia na uwazi nchini.
Mapema
Mkurugenzi wa ‘PEGAO’ Hafidh Abdi Said, aliwasisitiza wahamasishaji hao,
wanapoibua changamoto kwa jamii, wahakikishe wanaifuatilia hadi mwisho.
‘’Kwa
mfano, wapo wanawake hata vitambulisho vya mzanzibari mmegundua hawana, au
hawana huduma za kijamii kama maji safi na salama, sasa hapa lazima mzitafutilie
ufumbuzi wake, ili wawaamini,’’alishauri.
Hata
hivyo Mkurugenzi huyo, aliwakumbusha wahamasishaji hao, kuwamakini wanapoandika
ripoti zao, ili zianishe changamoto, suluhisho na mkakati wa baadae.
Kwa
upande wake Mratibu wa mradi wa kuihamasisha jamii kudai haki zao za kisiasa,
uongozi na demokrasia ‘SWIL’ kutoka ‘PEGAO’ Dina Juma, alisema ni vyema kwa taasisi
na mashirika, kuendelea kushirikiana na asasi za kiraia.
‘’Sisi
asasi na zile taasisi za serikali, sote tunatengeneza jamii moja, sasa
tunawapowafikia, kuwasilisha changamoto zao, waone kama tumewasaidia kazi,’’alieleza.
Akichangia
kwenye ripoti hizo, muhamasishaji jamii kutoka Wete Salim Hamad Sharif, aliuomba
uongozi wa ‘PEGAO’ kupanga timu maalum, kwa ajili ya kwenda kwa wananchi wa kisiwa
cha Fundo, kutoa elimu kwa upana.
‘’Wananchi
wa kisiwa cha Fundo baadhi yao hawajaelewa kwa upana, umuhimu wa elimu kwa
watoto wao, ndio maana mtoto anaweza kutolewa darasani aende habarini, bila
mzazi kujali jambo hilo,’’alieleza.
Nae
Mohamed Maalim, alisema kama inakubalika popote mtu anapofanyia kazi kufikisha
elimu, sasa atahakikisha kila eneo anafika, ili kuelezea haki jamii katika
uongozi, siasa na demokrasia.
Wakiwasilisha ripoti zao, viongozi wa wahamasishaji jamii kutoka wilaya nne za Pemba, walisema wamekuwa wakiibua changamoto zinazoikabili jamii, ingawa upatikanaji wa suluhisho ndio kikwazo.
Mradi wa kuihamasisha jamii kudai haki zao za
uongozi, demokrasia na siasa ‘SWIL’ unatekelezwa na Chama cha Waandishi wa
Habari Wanawake Tanzania, ‘TAMWA’ –Zanzibar, Jumuiya ya Wanasheria Wanawake
Zanzibar ‘ZAFELA’ na Jumuiya ya Utetezi wa Mazingira na Jinsia Pemba ‘PEGAO’
kwa ufadhili wa Ubalozi wa Norway.
Mwisho wa utekelezaji wa mradi huo, huo wa ‘SWIL’ unatarajiwa wanawake
wasiopungua 6,000 iwe wamesha wezeshwa kudai haki zao.
Mradi huo uliozinduliwa Novemba, 2020, na ukitarajiwa kutia nanga
mwaka 2024, watu 100 wakiwemo wanawake na wanaume, iwe tayari wameshajengewa
uwezo, ili nao sasa kuwafikia wanawake 400, ambao nao wenyewe wanatarajiwa
kuwafikia wanawake hao 6,000.
Idadi hiyo wanawake 6,000 watakaofikiwa, ni sawa na PEGAO, TAMWA
na ZAFELA kuwafikia wanawake 1,200 kwa kila mkoa mmoja, kati ya mitano ya
Unguja na Pemba.
Ambapo hapo ni sawa na wanawake 546 kutoka kila wilaya moja, kati
ya wilaya 11, ambapo Pemba zipo nne na Unguja saba.
Zanzibar yenye majimbo 50 ya uchaguzi, mradi huu wa ‘SWIL’
utawafikia wastani wa wanawake 120, kutoka kila jimbo moja la uchaguzi, sawa na
kufikiwa wanawake 55 kwa kila wadi moja, kati wadi 110 za Unguja na Pemba.
Mwisho
Comments
Post a Comment