HABIBA ZARALI, PEMBA@@@@
WANAFUNZI 771 wakiwemo wanawake 354 na
wanaume 417 pamoja na walimu skuli ya sekondari ya Uweleni wameondokana na
huduma ya maji isiyokuwa ya uhakika, baada ya kukamilishiwa ndoto yao ya
kuchimbiwa kisima.
Kisima hicho
chenye urefu wa mita 70 ambacho kitakuwa na uwezo wa kujaza 22,000 kwa saa mbili
kimechimbwa na shirika la usaidizi wa moja kwa moja Afrika
‘Direct Aid Association’.
Kisima hicho
pamoja na kuwanufaisha wanafunzi, tayari huduma hiyo imeshawanufaisha wanafunzi
768 wakiwemo 205 wa skuli ya maandalizi ya Uweleni na 563 wa madarasatul
Nurudhalami pamoja na wanajamii wa shehia ya Uweleni.
Akizungumza
katika hafla ya kukabidhiwa kisima hicho Msaidizi Mwalimu mkuu wa skuli hiyo
Khamis Mohamed Ussi alisema, kuwepo kwa huduma hiyo ya kudumu skulini hapo, ni
tunu haikuwepo kwa zaidi ya miaka 90 tokea kuanzishwa kwa skuli hiyo.
Alisema
skuli hiyo, tokea kuanzishwa kwake mwaka 1931 haikuwa na huduma ya uhakika ya
maji, kutokana na kutegemea huduma inayozalishwa na Mamlaka ya maji ZAWA,
ambayo hayakuwa yakiwatosheleza.
“Wakati mwengine wanafunzi wetu walishindwa hata kujifunza kwa
ufasha, kutokana na kukosa kwa huduma ya maji ya uhakika na leo( jana),
kupatikana kwa kisima hiki kimetimiza ndoto zetu skulini hapa,’’alifafanua.
Aidha Mwalimu huyo alisema kuwa, watatimiza
malengo ya mradi huo, ikiwemo kusaidia upatikanaji wa maji kwa jamii
inayowazunguka.
Kwa upande wake Mwalimu mkuu skuli hiyo Othman
Khamis Amour na Mwenyekiti wa skuli hiyo waliwataka walimu, wanafunzi na jamii
iliyozunguka skuli hiyo, kuithamini na
kuilinda miundombinu hiyo, ili waweze kutumia wao na vizazi vijavyo.
Walisema,
iwapo watafanya uharibifu wa aina yoyote ile, hawatoitendea haki miundombinu hiyo, pamoja na waliotowa msaada
huo, jambo ambalo litakwenda kinyume na malengo yaliyokusudiwa.
“Maji ni
uhai na ndio maana tulikuwa na shida pale ilipofikia hatua ya maji ya ZAWA
hayatoshelezi, sasa basi kisima hichi ni cha kwenu mnapaswa kukienzi,’’walisema.
Akikabidhi
kisima hicho Mkurugenzi wa Shirika la Afrika Direct Aid Association’ upande
wa Zanzibar Mohamed Said Othman, alihimiza kutoa sadaka kwa wenye uwezo, kwani kutawatatulia
changamoto zinazowakabili maskini.
Alifahamisha
kuwa utowaji wa sadaka haumnufaishi mpokeaji pekee, kama wengi wanavyofikiria,
bali hata mtowaji, nae ana malipo yake.
Hata hivyo
aliutaka uongozi wa skuli hiyo, kuandaa mikakati thabiti na endelevu, ili
kuhakikisha kisima hicho kinatoa huduma kama ilivyokusudiwa.
Akisoma
taarifa ya kitaalamu mkandarasi wa ujenzi huo kutoka kampuni ya Takdir Drilling
Patnaship Salum Mbarouk Salum alisema, kisima hicho kina urefu wa mita 70
kwenda chini, ambacho kina uwezo wa kujaza lita 22,000 kwa masaa mawili.
Mradi wa
uchimbaji wa kisima hicho, ambao umegharimu shilingi milioni 35, unakusudia
kuwaondoshea shida ya huduma ya maji safi na salama, wanafunzi, waalimu na
wanajamii wa shehia ya Uweleni wilaya ya Mkoani.
Mwisho.
Comments
Post a Comment