Na Nafda Hindi, Zanzibar@@@@
JAMII imetakiwa kuwaunga mkono wanawake katika harakati wanazozifanya za kuleta maendeleo ili kufikia malengo waliyojiwekea.
Hayo yalisemwa na muhadhiri wa kiislamu Visiwani Zanzibar, Ukhti Amina Salum Khalfan, wakati akizungumza na baadhi ya wanawake katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kujitokeza kugombea nafasi za Uongozi, mafunzo ambayo yaliandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) huko Tunguu Wilaya ya Kati Unguja.
Amesema wanawake wanahaki ya kushirikishwa katika harakati mbalimbali ikiwemo za kiuchumi, kijamii na kisiasa hivyo ni vyema wanapojitokeza katika maeneo hayo kuungwa mkono na kushirikishwa ipasavyo ili kuweza kufikia ndoto zao na kuleta maendeleo kupitia mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Amesema harakati za Uongozi kwa wanawake hazikuanza sasa na badala yake zilianza toka enzi za Mitume na Mtume Muhammad ( S.A.W) ambapo alikuwa akiwapa elimu ya kujitambua na kuwapa haki zao ili kuona kama kundi hilo ni moja ya makundi muhimu katika jamii.
“Mtume Muhammad (S.A.W) alikuwa akiwaruhusu maswahaba kwenda kujifunza kwa mkewe ambae ni bibi Aisha, (R.A) hali ambayo inadhihirisha wazi kwamba mwanamke hajakatazwa kuwa kiongozi au kufanya kazi,” Ukhti Amina Muhadhir wa Kiislam Visiwani Zanzibar.
Hivyo alitumia fursa hiyo kuiasa jamii kuacha mawazo mgando na badala yake kujitokeza kugombea na fasi mbalimbali ili kuongeza idadi ya viongozi wanawake katika ngazi za maamuzi hatua ambayo itatoa fursa kwa wanawake kueleza changamoto zinazowakabili na kupatiwa ufumbuzi.
Diwani wa wadi ya Kiongoni Makunduchi Zawadi Hamdu Vuai aliwashauri wanawake wenye nia ya kugombea nafasi za Uongozi kujituma na kujiamini pamoja na kuwa karibu na jamii ni njia moja wapo ya kufanikiwa na kufikia malengo.
“Sikutegemea kama ipo siku nitakuwa kiongozi, ila nimesoma kitu, jinsi unavyojitoa kwa watu ndio kilichonisogeza mbele kufikia nafasi ya Uongozi,” Zawadi Hamdu Vuai , Diwani wa Kiungoni Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja.
Mratibu wa Mradi wa kuwainua wanawake katika Uongozi (SWIL) kutoka tamwa Zanzibar Mariam Ame Chum alisema wamekuwa wakitoa mafunzo mara kwa mara ya kuwajengea uwezo wanawake kuwa Viongozi.
”Tunawaasa wanawake waliopatiwa mafunzo hayo kuyatumia na kwenda kuwafundisha wenzao ili kuongeza uelewa kwa jamii na kuweza kuungwa mkono wanawake pale wanaposimama kugombea nafasi za uongozi,” Zawadi Hamdu Vuai Diwani Kiungoni Makunduchi,
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo waliviomba vyama vya siasa na serikali kwa ujumla kufatilia nyenendo za viongozi wa majimbo na endapo wakibaini hawawajibiki katika kuwaletea wananchi maendeleo ni vyema kipindi kinachofata wasichaguliwe.
Hata hivyo waliwataka wanawake wenzao wasirudi nyuma na wasikate tamaa na badala yake wajitokeze kugombea nafasi mbalimbali.
Comments
Post a Comment