HABIBA
ZARALI, PEMBA@@@@
AFISA Mkuu
wa Mawasiliano na Uchechemuzi kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
Tanzania TAMWA- Zanzibar Sophia Ngalapi, amesema iwapo habari za kupinga udhalilishaji
zitaandikwa na kufanyiwa ufuatiliaji (follow up) zitasaidia kupunguza vitendo
hivyo nchini.
Akizungumza katika mafunzo ya
kuwajengea uwezo waandishi wa habari kisiwani Pemba, juu ya mbinu bora
za kuandika habari za udhalilishaji, alisema habari hizo zimekuwa
zikiandikwa kwa muda mrefu, ingawa imeonekana bado waandishi hawazifanyii
ufuatiliaji.
Alisema kuwa, hali hiyo imebainika
baada ya TAMWA kufanya utafiti kupitia vyombo vya habari, na kugunduwa kuwa
zipo habari za udhalilishaji zilizoripotiwa, lakini hazina ufuatiliaji jambo
ambalo, linarejesha nyuma juhudi za mapambano hayo.
"Utafiti mdogo wa miezi mitatu
uliokusanya vyombo vya habari vya redio, magazeti na mitandao ya kijamii,
lakini changamoto kubwa iliyoonekana, ni habari za udhalilishaji, kutofanyiwa
ufuatiliaji", alisema.
Akitowa mada mkufunzi Iman Due,
aliwahimiza waandishi hao kujituma zaidi na kuandika habari za kuelekeza,
kukosoa na kuibuwa changamoto, kwenye jamii kwa lengo la kuleta maslahi chanya.
Hata hivyo aliwaasa waandishi hao,
kusimamia hoja zenye maslahi ya jamii, hasa ukizingatia kazi yao ni yenye
kuhitaji uthubutu.
"Waandishi andikeni habari
za uchambuzi na wala musiendeshwe na mihemko ya jazba yoyote ile, na hii ndio
itawafanya muweze kuwa weledi,"alisema.
Akitowa mada ya uandishi habari za
uchunguzi mwandishi nguli Ali Mbarouk Omar, aliwataka waandishi kutokuwa na
hofu katika kiripoti habari za uchunguzi, kwani lengo ni kuibua vitu vyenye
kuleta maslahi mapana ya jamii.
Alisema jambo la muhimu, ni kufuata maadili
ya kazi yao inavyowaelekeza, ili dhamira ya kufanya uchunguzi iweze kupatikana.
Mafunzo hayo ya siku tatu kwa
waandishi wa habari kisiwani Pemba, yanaendeshwa na TAMWA kwa kushirikiana na UNESCO.
MWISHO.
|
Comments
Post a Comment