NA ZUHURA JUMA, PEMBA
WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kusoma na kuzielewa sheria zote, ili kufanya kazi ya habari kwa ufanisi na bila vikwazo.
Akifungua mafunzo ya siku moja kuhusu sheria ya habari, Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Khatib Juma Mjaja alisema, kujua na kuzielewa sheria za habari ni muhimu sana kwa wanahabari kwani wanazitumia katika kazi zao za kila siku.
Alisema kuwa, sera, kanuni, sheria na maadili ndio yanayojenga ustawi wa habari, hivyo kuna haja kwa waandishi kuwa na juhudi ya kuzisoma sheria kila siku ili kufanya kazi zao kwa ufanisi na kuepuka vikwazo.
"Waandishi wa habari ni wadau wakubwa ambao wanaifanyia kazi sheria, hivyo ni lazima tuzisome na tuzijue vizuri ili kutusaidia katika kazi zetu za kihabari" alisema Mjaja.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Kajubi Mukajanga alisema, waandishi wa habari wasipozielewa sheria, mchakato wa kupitisha sheria utakuwa kwenye mikono ya wanasheria na wanasiasa tu, hivyo wao watakuwa hawana nafasi.
"Ni matumaini yetu kwamba baada ya mafunzo haya mtakuwa wabobezi wa kuijua sheria na mtachukua juhudi ya kuelimisha kwenye vyombo vyenu", alisema Katibu huyo.
Nae Afisa Mdhamini Wizara ya Habari, Vijana, Sanaa na Michezo Pemba Mfamau Lali Mfamau aliwaomba waandishi wa habari kuwa makini wanapopewa mafunzo, kwani yanawajenga zaidi katika kufanya kazi zao za kila siku.
"Naliomba Baraza la Habari Tanzania liwasaidie waandishi wa habari nyezo za kufanyia kazi, kwani wengi wao wanashindwa kumiliki na wana uwezo mkubwa katika masuala ya habari", alisema.
Afisa Mdhamini MCT Zanzibar Shifaa Said Hassan alifahamisha kuwa, kada ya habari ndio inayoleta maendeo katika nchi yeyote duniani, hivyo aliwataka waandishi wa habari kuzidisha mashirikiano katika kukuza na kuendeleza tasnia hiyo.
Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo Afisa huyo alisema, kuna madhila mengi yanayowakumba wanahabari ingawa wengine wanashindwa kuripoti, ambapo aliwataka waripoti MCT kwa ajili ya kurikodiwa kwenye kanzidata.
Akiwasilisha mada ya Uhuru wa maoni mwanasheria Mpale Mpoki alisema ili nchi ipate maendeleo, kuwepo kwa demokrasia na Utawala Bora lazima watu watoe waliyonayo, kwani hujenga ustawi bora wa maisha.
"Haki ya kupata habari ni miongoni mwa haki muhimu za binadamu na ana kila sababu ya kupata habari, hivyo waandishi muhakikishe habari zenu zinawafikia wananchi na wapate kutoa maoni yao", alifahamisha mwanasheria huyo.
Mafunzo hayo ya siku moja ya sheria ya habari, yalifanyika katika Ukumbi wa Samael Gombani Chake Chake.
MWISHO.
Comments
Post a Comment