IMEANDIKWA
NA HAJI NASSOR, PEMBA
MAHAKAMA
ya Mkoa Wete imeanza kusikiliza ushahidi wa kesi ya daktari Is-hak Hadid Rashid
anaedaiwa kumbaka mtoto wa miaka 16.
Shahidi namba moja ambae ni baba mzazi wa mtoto huyo alidai
mahakamani hapo kuwa, Aprili 21 mwaka 2022 majira ya saa 10:00 jioni wakati
anarudi kwenye pirika zake za kazi aliambiwa na mke wake kuwa, mtoto wao
hajarudi skuli mpaka muda huo.
Alidai kuwa, hakufanya wasiwasi sana kwani aliamini kuwa
itakuwa yuko kwa shoga zake baadae alikwenda bondeni na aliporudi saa 11 jioni
aliambiwa bado mtoto huyo hajarudi.
“Nilikwenda kwa shoga zake kumuulizia, lakini hawakuwa na
taarifa zozote, ndipo nikarudi nyumbani kushauriana na mke wangu na tukaamua
kwenda kutoa taarifa kituo cha Polisi Madungu’, alidai baba huyo.
Mama wa mtoto huyo alidai mwanawe ni mwanafunzi wa kidato cha
nne, ambapo alikwenda skuli majira ya saa 4:00 asubuhi kwa vile ilikuwa ni
mwezi wa Ramadhani, ingawa ilifika muda wa kurudi skuli hajafika nyumbani,
ndipo walipoanza kumtafuta na baada ya kutofanikiwa kumpata walikwenda kituo
cha Polisi kutoa taarifa.
“Kwa kipindi chote alichoondoka mtoto wake alikuwa hapatikani
kwenye simu yake mpaka pale alitaka mwenyewe kunipigia simu Aprili 25 mwaka huu
na kuniambia kuwa yupo Kangagani ambapo
nyumbani aliondoka tangu Aprili 21 mwaka huu”, alidai mama huyo.
Alidai kuwa, baada ya kupigiwa simu na mwanawe huyo alimtaka
arudi nyumbani kwao ingawa alifikia kwa mjomba wake na ndipo alipokenda
kumchukua na kumpeleka Polisi.
Mara baada ya mtuhumiwa kupanda kizimbani akisubiri taratibu
za mahakama, wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka Juma
Mussa Omar alipodai kuwa, shauri hilo lipo kwa ajili ya kusikilizwa mashahidi.
“Tunao mashahidi watatu ambae ni baba wa mtoto, mama, na mtoto
mwenyewe, hivyo muhehismiwa hakimu tuko tayari kusikiliza mashahidi wetu”,
alidai wakili huyo.
Baada ya kusikilizwa ushahidi wa baba na mama, mtoto anaedaiwa
kufanyiwa kitendo hicho, katika ushahidi wake alikana kubakwa na daktari huyo
na ndipo wakili huyo alipoiomba mahakama iliahirishe shauri hilo hadi tarehe
nyengine.
“Muheshimiwa hakimu, ushahidi anaoutoa mtoto huyu hapa
mahakamani ni wa uongo kwa sababu kituo cha Polisi alitoa maelezo na leo
anayakana haya na kutoa mengine”, alidai DPP huyo.
Hakimu wa mahakama hiyo Ali Abdul-rahman Ali alikubaliana na
ombi la upande wa mashitaka na kusema kuwa kesi hiyo itarudi tena Juni 22 mwaka
huu kwa ajili ya kusikilizwa mashahidi.
Ilidaiwa
kuwa, baina ya Aprili 21, mwaka huu mtuhumiwa huyo alimtorosha mtoto huyo
kutoka nyumbani kwao Gombani wilaya ya Chake Chake na kumpeleka nyumbani kwake
anakoishi Kangagani wilaya ya Wete, ambapo usiku wake alianza kumbaka na
kuendelea kumfanyia kitendo hicho kwa siku tatu tofauti.
Kufanya
hivyo ni kosa, kinyume na kifungu cha 113 (1) (a) cha sheria ya Adhabu nambari
6 ya mwaka 2018, sheria ya Zanzibar.
Kosa
la pili kwa mtuhumiwa huyo, baada ya kumtorosha mtoto huyo, siku hiyo hiyo
majira ya saa 3:00 usiku alimbaka, ambapo ni kinyume na kifungu cha 108 (1),
(2), (e) na 109 (1) cha sheria ya Adhabu nambari 6 ya mwaka 2018.
Kosa
la tatu, ambalo lilitokea Aprili 22 mwaka huu na la nne ambalo lilitokea Aprili
23, mwaka huu pia, alilitenda kwa nyakati tofauti za usiku, ambapo alidaiwa
kumbaka mtoto huyo.
Kufanya
hivyo, ni kinyume na kifungu cha 108 (1), (2), (e) na 109 (1) cha sheria ya
Adhabu nambari 6 ya mwaka 2018, sheria ya Zanzibar.
MWISHO.
Comments
Post a Comment