NA HAJI NASSOR, PEMBA
MKUU wa mkoa wa kusini Pemba Mattar
Zahor Massoud, amewahakikishia masheha mkoani humo, kuwa watakosa kazi na kisha
kusughulikiwa kisheria, ikiwa watasimama kama mashahidi kuzifanyia sulhu kesi
za udhalilishaji.
Alisema kwa
sasa imekuwa ni mchezo endelevu mkoani humo, kwa baadhi ya masheha kujihusisha
na sulhu kwa kesi za ukatili na udhalilishaji, jambo ambalo amesema sasa
imetosha.
Mkuu huyo
mkoa aliyaeleza hayo, wakati akilighairisha kongamano la kujadili changamoto za matendo ya ukatili na udhalilishaji, lililofanyika hivi karibuni mjiji Chake
chake, lililoandaliwa na Jumuiya ya Tumaini Jipya Pemba TUJIPE.
Alisema kama
kuna sheha ameshachoka kuhudumu kwenye nafasi hiyo, ajaribu kuzitia mkono kesi
hizo, ambazo kwa sasa zimekuwa zikijotokeza siku hadi na kuvizisha juhudi za
serikali na wadau wake.
Alieleza
kuwa, sasa kila sheha lazima ajitenge mbali na kushiriki kwenye jamvi au vikao
vya sulhu, baina ya wazazi wa pande mbili, na akigundulika hatua za kinidhamu
dhidi yake zitachukuliwa.
Hata hivyo
aliwataka masheha hao, wanapobaini uwepo wa matukio kwenye shehia yake
kuwasiliana na yeye moja kwa moja, kabla ya kutoa taarifa kwenye mamlaka
yoyote.
‘’Kama mpaka
leo hii kuna sheha anajifanya ni sehemu ya mahakama kwa kuzikalisha pande mbili
chini, ili sulhu ipatikane baada ya mtoto kudhalilishaji, kwanza hana tena kazi
pili taratibu nyingine zitafuata,’’alieleza.
Katika eneo
jengine Mkuu huyo wa mkoa, amelitaka Jeshi
la Polisi mkoani humo, kuwasweka lupango, wazazi na walezi watakaobainika kuwatorosha
vijana wao, wanaotuhumiwa kufanya makosa ya udhalilishaji.
Alisema wapo
baadhi ya wazazi wamekuwa, wakitengeneza mazingira na kisha kuwatorosha vijana,
wao wakijua kuwa wanatafutwa na Jeshi la Polisi kwa tuhma zinazowabili.
Alilitaka
Jeshi la Polisi mara wabainipo mtuhumiwa kutoroka waanzishe uchunguzi na
wakibaini kuwa wazazi wamehusika, waanze na wao kwa kuwaweka ndani hadi kijana
wao atakaporudi.
‘’Jeshi la
Polisi naliagiza rasmi, ikiwa kuna wazazi na walezi wamekuwa wakibuni mbinu na
kuandaa mikakati ya kuwakimbiza watuhumiwa, msipate shida kamata mama, baba au
mlezi weka ndani hadi mtuhumiwa arudi,’’alieleza.
Katika hatua
nyengine Mkuu huyo wa Mkoa wa kusini Pemba Mattar Zahoro Massoud ameitaka
jamii, kuacha rushwa muhali na kwenda mahakamani kutoa ushahidi, ili watuhumiwa
wapatiwe adhabu.
‘’Hakuna
kesi itakayopatiwa hatia pasi na mashuhuda wa tukio kufika mahakamani kutoa
ushahidi, lakini ikiwa mmezidiwa na rushwa muhali matendo hayo
hayatokoma,’’alifafanua.
Kwa upande
wake Mkuu wa wilaya ya Chake chake Abdalla Rashid Ali, alisema kama hakuna njia
ya kumaliza matendo, kama sio kuyaripoti kwa wakati.
Akizungumza
kwenye kongamano hilo, Mratibu wa TUJIPE Pemba Tatu Abdalla Msellem, alisema
moja ya jambo linalowaumiza kichwa ni wazazi na walezi kukubali sulhu kwa kesi
za udhalilishaji.
‘’Wazazi
wamekua wakali mara tukio linapotokezea, lakini linapoanza kufika mahakamani
huanza dharura za hapa na pale na wakati mwengine hadi kumkana mtuhumiwa,’’alieleza.
Kamanda wa
Polisi mkoa wa kusini Pemba Richard Tadei Mchomvu, aliwataka wazazi kuwa karibu
na watoto wao, ili wanapopata shida kama ya udhalilishaji kupata taarifa
mapema.
Mwisho
Comments
Post a Comment