NA MWANDISHI MAALUM-ZANZIBAR
Katika
juhudi za kuimarisha ushiriki wa wanawake katika uongozi na kukuza haki za
kidemokrasia, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-
ZNZ) kimetoa mafunzo ya siku mbili kwa Wahamasishaji Jamii (Citizen Brigades) wapatao
60 kwa upande wa Unguja ikiwa ni sehemu ya programu ya kuimarisha uongozi kwa wanawake
(SWIL) wenye lengo la kujenga jamii yenye usawa wa kijinsia kwa kuwawezesha
wanawake kushika nafasi katika ngazi za maamuzi.
Akizungumza
wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano TAMWA ZNZ,
Saphia Ngalapi, ameeleza kuwa watekelezaji wa programu wana imani na wahamasishaji
waliopatiwa mafunzo na kuwa watakuwa mabingwa wa kuhamasisha jamii juu ya haki
za wanawake kushiriki katika uongozi.
"Kupitia
timu hii, tunatarajia mabadiliko katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki ya
demokrasia na uongozi kwa wanawake ili kufikia 50% kwa 50% katika ngazi za
maamuzi, jambo litakalochangia kuleta maendeleo endelevu kwa wote" alisema
Ngalapi.
Afisa
Ufuatiliaji na Tathmini TAMWA ZNZ, Mohamed Khatib, aliwasisitizia wahamasishaji
hao juu ya umuhimu wa kazi yao katika kukuza nafasi za wanawake katika uongozi.
"Tufahamu
kuwa hili jambo la kuelimisha jamii si ajira bali ni kazi ya kujitolea
kuhakikisha matarajio ya wanawake kushika nafasi za uongozi yanafikiwa kwa
kubadilisha mitazamo ya jamii, uchaguzi wa 2025, tunataka tuone wanawake wanashika
nafasi za uongozi kuanzia ngazi za shina hadi Taifa kwani uwezo huo wanao, alifafanua afisa huyo.
Mafunzo
haya yamejumuisha wawakilishi kutoka makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo
viongozi wa dini, watu wenye ulemavu, wanaharakati wa kupinga vitendo vya udhalilishaji
na wanaume wa mabadiliko.
Nae mkufunzi
ni mafunzo hayo ya siku mbili Asha Abdi aliwahimiza wahamasishaji jamii kuwa
mstari wa mbele katika kuhakikisha malengo ya mradi huu yanafikiwa.
Ukhty
Amina Salum ambae ni kiongozi wa dini na mwanaharakati wa siku nyingi ameeleza
shukrani zake kwa kuchaguliwa kuwa sehemu ya wahamasishaji wa jamii.
"Nafurahi kuwa miongoni mwa wahamasishaji wa jamii, dhamana hii nitaibeba
na kuhakikisha jamii inahamasika na kuachana na dhana potofu juu ya uwezo wa
mwanamke na maamrisho ya dini kuhusiana na wanawake kushiriki katika uongozi. alisema
Ukhty Amina.
Nae
Haji Khamis Haji kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja alisisitiza kuwa elimu
aliyoipata itamsaidia kuhamasisha jamii katika mkoa wake kutambua haki zao za kidemokrasia
na kuongeza wanawake katika nafasi za uongozi.
Mafunzo
haya yanaashiria jitihada za TAMWA- ZNZ kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wanawake
Wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba
(PEGAO) Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) kwa mashirikiano
makubwa na Ubalozi wa Norway katika kuwaandaa wanawake wenye nia ya kugombea
nafasi za uongozi kuelekea uchaguzi wa 2025, huku wakilenga kuongeza idadi ya
wanawake katika ngazi za maamuzi visiwani Zanzibar.
Comments
Post a Comment