NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
TIMU ya Wawi star, inayoshiriki ligi
daraja la kwanza kanda ya Pemba, imeendelea kutimiza dhamira yake ya kupanda
ligi kuu ya Zanzibar msimu ujao, baada ya tena jana, kuvuna alama tatu muhimu,
mbele ya wenyeji timu ya El-Legado FC, baada ya kuikalisha chini kwa bao 1-0.
Katika mchezo huo, uliokuwa wa kusisimua na kuhudhuriwa
na watamazaji wengi kutoka mitaa ya Finya, ulichezwa majira ya saa 10:00 jioni,
ndani ya dimba la FF Finya.
Timu zote ziliuanza mchezo kwa kasi, huku kila
mmoja akijaribu kumsoma mwenzake, na kukijitokeza mashambulizi ya
kushtukiziana, kwa kila mara na kwa zamu.
Wageni Wawi star, walianza kuwaamsha wenyeji wao,
mnamo dakika ya 15, baada ya kupeleka shangwe zito langoni mwao, kisha shuti la
Suleiman Seif Madeo, likatoka nje.
E-legado kuona hivyo, nao mipango yao ilikaa sawa
mnamo dakika 25, baada ya kulianzisha kwa kasi, kutoka upande wa mashariki mwa
uwanja, kisha pasi nzuri ya kumalizia ikamfikia Ali Issa Mzinga, ingawa shuti lake
lilipaa juu.
Kasi ya mchezo ilionekana kuongezeka, hasa mnamo
dakika ya 38, baada Wawi star kugongeana gongeana vyema, jambo lililoanzia kwa
Az-har Mbarouk Seif kisha kumpa pasi Hassan Is-mail Yombo, ingawa shuti lake,
lililiwa na kipa Said Massoud Ali.
Wawi star, waliamka tena dakika 44, na huku tayari
washabiki wakiwa wameshanyanyuka juu, kushangilia bao la kwanza, baada ya Rafii
Haida Ramadhan, kuwapita walinzi wote, ingawa fataki aliloliachia lilikosa
dira.
Na hapo dakika 45 za awali wanaume hao 22,
wakazimaliza kukiwa hakuna timu iliyocheka, na kuzipa nafasi dakika 45 nyingine
kuanza kwa kasi kwa kila upande.
Hamu ya kusakala alama tatu za ugenini kwa Wawi star,
ilipata mbolea, mnano dakika ya 81, baada ya shuti la Ali Maliki alilolipiga
umbali wa mita 20 kutuwa, ndani ya vyavu.
Mwamuzi wa mchezo huo, alizimaliza dakika 90 kwa
Wawi star, kuondoka na ushindi wa bao 1-0, na kuwaacha wenyeji wa uwanja huo,
kubakia kulaumiana.
Na katika mchezo mwingine wa ligi hiyo, klabu ya Super
Falcon na Yosso Boys, wakagawana alama moja moja, baada ya kuchapana bao 1-1,
mchezo uliochezwa uwanja wa Mtega Wawi.
Mwisho
Comments
Post a Comment