ZANZIBAR, kama ilivyo baadhi ya nchi za Afrika, nayo ilipitia
changamoto ya kutawaliwa na wageni kadhaa, wakiwemo Wareno, Waarabu na Waingereza.
Utawala wa Waarabu baina ya mwaka 1832 hadi mwaka
1920, kwa wakati huo, Zanzibar ilikuwa ikifanya maamuzi kwa kupitia Majilisi al
Shura.
Ambayo ilitunga sheria kwa kuegemea kwa kiasi kikubwa
mamlaka binafsi ya Sultan, yaani mtawala.
Baadae mkubaliano ya kuilinda Zanzibar, yaliyotiwa
saini kati ya Uingereza na Sultan, Juni 14, mwaka 1890, yalitela mabadikilo ya
kuulinzi chini ya Uingereza.
Historia, iliyowekwa kwenye tovuti la Baraza la
Wawakilishi Zanzibar, inafafanua kuwa, mwaka 1891, serikali ya kikatiba,
ilianzishwa na Jenerali Sir LIoyd Mathews, kama Waziri wa kwanza wa Uingereza Zanzibar.
Safari ya Zanzibar, kujikomboa ilifikia mwaka 1914 na
hasa mwaka 1926, ambapo Amri ya Sheria ya Mabaraza ilipitishwa na kuanzishwa Baraza
la Kiutendaji.
Hayo yanafanyika, hakukua na mzalendo hata mmoja,
ingawa ilikuwa ni kwa ajili ya taifa la Zanzibar, kwa wakati huo, kabla ya
mapinduzi ya mwaka 1964.
Baada ya chaguzi kadhaa kufanyika, kuanzia Januari
1961, Juni 1962 na Julai 1963, hapo chombo kipya cha kutunga sheria Zanzibar, kilianzishwa
kwa katiba ya kwanza na kuanzishwa.
Ingawa Katiba hiyo, haikudumu, maana Muasisi wa
mapinduzi Abeid Amani Karume na wenzake, walifanya mapinduzi kwa kuuondoa
utawala wa kidhalimu, pale Januari, 12 mwaka 1964.
KABLA YA TAAANGAZO LA ELIMU BURE
Alishatangaaza pale, Septemba 23 mwaka 1964, Rais wa kwanza
wa Zanzibar Abeid Amani Karume, kuwa elimu ya Zanzibar, itatolewa bure.
Maana, watoto wa kizanzibari, wakiwemo wenye ulemavu,
kabla ya mapinduzi walibaguliwa na kukoseshwa haki yao ya elimu, na waliokuwa
wakiipata walilazimika kuigharamia.
Mwandawa Haji Kassim (71) wa Mtambile, anasema
hakukua na mtoto wa mkulima, na hasa mwenye ulemavu, kabla ya mapinduzi aliyepata
elimu.
‘’Wewe wendauliza watoto wenye ulemavu, wale waliokua
na viungo kamili, hawakupewa elimu na mkoloni, je ambae anaulemavu,’’anahoji.
Kassim Mohamed Haji (67) wa Chake chake, anasema haki
ya kupata elimu, halikuzingatiwa na Sultan wala Mreno, walihofia kutawaliwa.
Anaeleza, hata skuli kwa upande wa Pemba, ilianzia
eneo la Jambangome miaka 300 iliyopita, lakini wakisomeshana wenyewe.
Fatma Haji Said (68) mwenye ulemavu mkaazi wa Mkoani,
anasema hakuwahi kuingia darasani kupata elimu, kwani wazazi wake walikuwa ni
watumwa, kwa waarabu.
‘’Hakukua na mtoto aliyepata elimu, kabla ya mapinduzi
na ikitokezea anaishia darasa la pili tu,’’anasema.
Kwa wakati huo, historia inaonesha miji iliyokuwa na
wahindi kama Kengeja na Jambangome, wenyewe walijianzishia skuli, kwa ajili ya watoto
wao tu.
‘’Kwa mfano maeneo ya wahindi kama Jambagone, Pujini
Mkamandume na Mkumbuu ‘Kambaluu’ walikimbilia Zanzibar, kwa kuogopa vita nchini
kwao,’’inafafanua.
Kabla ya mapinduzi ya Zanzibar, hakukua na wizara ya Elimu,
wala taasisi iliyokuwa ikishughulikia elimu, jambo lililowakosesha elimu watoto
wenye ulemavu.
BAADA YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR MWAKA
Ndani ya mwaka huu wa 2025/2026 ambapo Zanzibar inatimiza
miaka 62, wapo wanafunzi wenye ulemavu 1,048 wakiwa wanaendelea na masomo.
Kwa mujibu wa taarifa ya takwimu za elimu za mwaka 2025,
zilizopo kwenye tovuti ya wizara ya Elimu na Mafunzo ya Elimu Zanzibar, inasema
Pemba pekee wapo wanafunzi 5, 416.
Ni wastani wa kila mkoa wa mmoja wa Pemba, kuwa na wanafunzi
wenye ulemavu 2,708 sawa na wanafunzi 1,354 ukiwaganya kwa wilaya nne za
kisiwani humo, wakifaidi tunda la elimu.
Idadi hii ya wanafunzi, ambayo kabla ya mapinduzi
haikuwepo, ni tunda jipya la elimu mjumuisho kwa kuwaingiza, kwenye wanafunzi mchanganyiko.
Maana kwa idadi hiyo ya wanafunzi 5,416 ni sawa na kwamba,
wameunda madarasa 120, yenye wastani wa wanafunzi 45 kila darasa, kama sera ya
elimu inavyoekeza.
Sera inasisitiza, kwa upande wa skuli isizidi
wanafunzi kati ya 400 hadi 450, ambapo kwa idadi hiyo ya wanafunzi, wanaweza
kutengeneza skuli 12 zenye kima cha wanafunzi hao.
Waziri wa Elimu na Mafunzo la Amali Zanzibar, Lela Mohamed
Mussa, akiwasilisha hutuba ya bajeti ya mwaka 2025/2026, ukumbi wa Baraza la
Wawakilishi, anasema juhudi za kuwaingiza madarasani wanafunzi ni kubwa.
Anasema, lengo lao ni kuondosha ubaguzi katika sekta
zote, ikiwemo elimu, hasa kwa kuwepo kwa sera ya elimu Mjumuisho.
‘’Ni wazi kuwa, kabla ya mapinduzu hakukua na idadi
ya mtoto hata mmoja, mwenye ulemavu aliyepata haki ya elimu, leo wapo zaidi ya
10,000 kwa Unguja na Pemba,’’anafafanua.
Katibu Mkuu wizara hiyo Khamis Abdalla Said, akaeleza
kuwa, baada ya kujikomboa, sasa zipo
skuli maalum zinazoitwa mjumuisho, zikiwa na miundombinu kwa wanafunzi wote.
Kwa Pemba ipo Pujini, iliyopewa jina la ‘Hemed’ ambayo
ilifunguliwa miaka mitano iliyopita, na sasa wanafunzi wenye ulemavu na wingine
wakiendelea kujisomea.
TAKWIMU
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, katika
kasaha lake la takwimu la mwaka 2025, iliyowekwa kwenye tovuti yake, imezidi
kufafanua kuwa, kwa Pemba wapo wanafunzi 5,416 wenye ulemavu wa aina mbali
mbali, huku elimu ya awali wakisajiliwa 744, wakiwemo skuli za serikali 566 na
binafsi 178.
Ngazi ya elimu ya Msingi wapo wanafunzi 2,584 ambapo
wanaosoma skuli za serikali, wakiwa 2,468 na wale wa skuli binafsi 116.
Elimu ya sekondari, kuanzia kidato cha kwanza hadi
cha nne, waliopo serikali ni wanafunzi 14,22 wakati kwa skuli binafsi ni 50, na
kutengeneza takwimu ya 1,472.
Wilaya za Micheweni na Mkoani, kwa elimu ya awali, ndizo
zilizoongoza kwa wanafunzi 159 kila moja, huku wilaya za Wete na Chake chake,
zikiwa na 124.
Kwa elimu msingi wilaya ya Mkoani, imebeba wanafunzi
797, ikifuatiwa na Wete 619, wakati Chake chake na Micheweni, zikiwa na wanafunzi
sawa ya 526.
Taarifa hiyo inafafanua kuwa, wilaya ya Wete inaowanafunzi
wenye ulemavu 429, Chake chake 428, Mkoani 353 na Micheweni 212 wanaopata haki
yao ya elimu ngazi ya sekondari.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu ‘NBS’ kwenye taarifa yake
iliyokwa Januari 17, mwaka huu juu ya hali ya ulemavu, imeripoti wanafunzi 2, 225,
671 wenye ulemavu wakipata haki yao ya elimu Tanzania.
Ambapo kati hao, milioni 1,119, 694 wako elimu ya
msingi na 107, 759 wakiendelea na masomo yao ngazi ya sekondari kwa Tanzania
bara pekee.
WANAFUNZI WENYE ULEMAVU WANASEMAJE
Issa Haji Muhsin wa Mwambe, anaesoma darasa la nne, anasema
sera ya elimu mjumuisho, imekuja kuwakomboa.
Aisha Tunu Makame wa skuli ya Michakaini anasema kama
sio uwepo wa sera hiyo, leo yeye na wenzake wasingekuwa wanapata haki yao ya elimu.
Fatma Hija Kassim mwenye ulemavu wa uziwi wa skuli ya
sekondari ya Mchanga mdogo, anasema malengo yake ya baadae ni kuwa daktari.
‘’Leo najivunia nna vifaa vya kusomea na kuongezea
suati, nasema heko sera ya elimu mjumuisho,’’anasifia.
WAZAZI
Mzazi wake Hija Kassim Hija, ansema sasa watoto wao,
wanaendelea kutimiza ndoto zao, kama ilivyokuwa azma ya serikali.
Maryam Hassan Said wa Pandani, anasema sasa mtoto
wake mwenye ulemavu wa viungo, ni daktari wa watoto Arusha, na amekuwa msaada
mkubwa wa familia.
‘’Ukitaja faida ya sera ya elimu mjumuisho kwangu, ni
mfano wa mtoto wangu, leo amekuwa ndio simba wa familia,’’anasema.
WADAU WA ELIMU
Tatu Abddalla Msellem wa Ole, anasema idadi ya watoto
5,416, kwamba wako madarasani wakipata elimu, tena wakiwa na ulemvu ni jambo la
kujivunia.
Ofisa Mdhamini wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba,
Mohamed Nassor Salim, anasema wizara itandelea kuwawekea mazingira wezeshi, kwa
wanafunzi wenye ulemavu.
Hidaya Mjaka Ali mwenye ulemavu wa viungo mkaazi wa
Vitongoji, anasema sera ya elimu kwa wote, imekua na mafanikio kwa kundi la watoto
wenye ulemavu.
Khadija Haji ni anaesoma fani ya ualimu wa viziwi,
chuo cha Ualimu Nkurumah, anasema anatamani kuona kundi la wanafunzi wenye ulemvu
wananufaika na elimu.
Mkuu wa chuo hicho, Ame Haji Vuai anasema, wanazo
fani zaidi ya nne, zikiwalenga watoto wenye ulemavu, ambapo sasa wanafundisha
waalimu.
‘’Chuo cha ualimu Nkurumah, kimeibuka tena kwa mfumo
mpya, wa kuwafundisha wanaosomea ualimu kwa ajili ya wabafunzi wenye ulemavu,’’anasema.
MIKATABA
Sera ya Elimu ya
Zanzibar, ya mwaka 2006 inawazingatia watu wenye ulemavu, wakiwemo wenye
ulemavu wa uziwi, kupitia misingi ya elimu jumuishi na utoaji wa haki sawa ya
elimu.
Ibara ya 4.6 inasiistiza
kuwachanganywa wanafunzi wasio na ulemavu, ili kusoma kwa pamoja na kuanzishwa
kwa mtaala wa elimu mjumuisho, katika mafunzo ya amali.
Mpango wa Maendeleo II uliyopita wa wizara ya
Elimu, unasema, elimu jumuishi inayotolewa katika ngazi ya darasa inaeleweka
kujumuisha, mifumo mizuri ya kugundua na kufuatilia mapema wanafunzi wenye
ulemavu.
Sheria ya watu wenye ulemavu
Zanzibar Na. 8 ya mwaka 2022, kifungu cha 28 (1), kinatoa haki ya elimu bora na
kuzuia ubaguzi wa aina yoyote, kutokana na ulemavu.
Mpango wa Maendeleo
2025 hadi 2030, serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, nao imedhamiria kuimarisha
mifumo ya utambuzi wa mapema wa ulemavu na kuimarisha miundombinu ya elimu.
Aambap sera ya elimu
na mafunzo ya Ufundi ya Tanzania ya
mwaka 2014, toleo la mwaka 2023, limelenga fursa za usawa, katika utoaji wa elimu
na mafunzo, bila ya ubaguzi wowote.
Mkataba wa kimataifa
wa haki za watu wenye ulemavu wa mwaka 2006, Ibara ya 24, inatambua haki za watu
hao, kupata elimu, tena bila ya
ubaguzi.
Katiba ya Zanzibar ya
mwaka 1984, kifungu cha 12 (1) kinasiistiza kuwa, binaadamu wote huzaliwa
huru, na wote ni sawa kila mtu, anastahili heshima ya kutambuliwa na
kuthaminiwa utu wake.
Kifungu cha 13 (1) kinaenda
mbali zaidi, kwa ufafanuzi kuwa, watu wote ni sawa mbele ya sheria, na
wanayohaki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya
sheria.
‘’Hakuna sheria
itakayokuwa na kifungu chochote ambacho ni cha ubaguzi wa moja kwa moja au kwa
taathira yake,’’ ikafafanua.
Azimio la ulimwengu la
haki za binaadamu toleo la kuadhimisha miaka 60 mwaka 1948 hadi 2008, katika ibara
ya 26, inaelekeza ‘kila mtu ana haki ya kupata elimu na itolewe bure, hasa
ile madarasa ya awali na iwe wazi kwa wote’.
Wakati akizindua
Baraza la wawakilishi la 1l Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, anasema katika
kutambua umuhimu wa sekta ya elimu, serikali itaimarisha na itaipa kipaumbele.
‘’Katika kipindi hichi
tutaimarisha sekta ya elimu katika kuwawekea mazingira rafiki na vifaa vya
kujifunzia na kufundisha, kulingana na mahitaji ya wanafunzi,’’alifafanua.
Afisa Programu
na Mawasiliano wa Chama cha Waandishi wa Habari wanawake Tanzania (TAMWA -
Zanzibar), Khairat Ali Haji alipokuwa akiwajengea uwezo waandishi wa habari, alisema
wananafasi katika kubadilisha mitazamo hasi, kuhusu haki za watu wenye ulemavu.
Ndio maana, akasema upo mradi mjumuishi wa kuwawezesha
watu wenye ulemavu, kupitia vikundi vya ushirika, kusudi wajiwezeshe ili watoto
wao wasome.
Mwisho




Comments
Post a Comment