NA MWANDISHI MAALUM, ZANZIBAR
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mhe. Wakili Dunford George Mpelumbe, amewahakikishia wanachi wa Zanzibar jinsi ya Tume hiyo ilivyojipanga vyema katika kupokea, kuchunguza na kutatua kwa wakati na usawa, malalamiko yote ya ukiukwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora yanayofikishwa katika ofisi za Tume hiyo zilizopo Zanzibar.
Mhe. Mpelumbe ameyasema hayo leo
tarehe 11 Novemba, 2026, alipozungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali
katika Ofisi za Tume zilizopo Mombasa, Mkoa wa Mjini mMagharibi.
Akitaja majukumu ya Tume kwa
waandishi hao Mwenyekiti Mpelumbe aliwaeleza waandishi hao kwamba Tume mbali ya
majukumu mengi iliyonayo, inatoa Elimu kwa Umma, kusimamia mikataba ya
kimataifa kwa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mikataba yote ya kikanda na
kimataifa inayohusu haki za binadamu ambayo Tanzania imeridhia.
Pia alieleza namna ya Tume
inavyoendelea na kushughulikia malalamiko ya wananchi yanayofikishwa katika
ofisi za Tume hiyo kwa maeneo mbalimbali ya nchi huku akionesha baadhi ya
matawi ambako Tume hiyo inafanyakazi ikiwemo Makao makuu Dodoma, Ofisi ya
Zanzibar, matawi ya Pemba, Mwanza, Dar es Salaam, Tabora na mikoa mengine nchini.
Aidha, Mhe. Mpelumbe ameendelea
kuisihi jamii na wadau wa haki za binadamu kuendeleza ushirikiano wa pamoja
uliopo baina yao na Tumw sambamba na kuendeleza kujenga utamaduni wa kuheshimu
haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini.
Akizungumza katika Mkutano huo,
Makamu Mwenyekiti, Mhe. Omar Ali Omar wakati akiibu swali la waandishi kuhusu mkakati
mpya wa Tume wa kutosubiri malalamiko ofisini pekee, amefafanua mwelekeo mpya
wa utendaji kazi za Tume kama ulivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema Tume itaendeleza
utamaduni wake wa kushughulikia kwa wakti changamoto na malalamiko yote wanayoyapokea.
“Tume hatutakuwa watu wa kukaa
maofisini na kusubiri wananchi waje, badala yake tumejipanga kikamilifu
kuchukua hatua za haraka na za makusudi kutambua, kuchunguza, na kushughulikia
changamoto zote za haki za binadamu na utawala bora mara zinapojitokeza katika
jamii," amesisitiza Mhe. Omar.
Hata hiyo, Makamu Omar ametoa
wito kwa wananchi na jamii kwa ujumla vikiwemo vyombo vya habari, kuacha woga
na kuwa huru kuifikia Tume kwani ndio chombo chao kikuu cha utetezi wa misingi
ya haki na utu.
Huu ni mkutano wa kwanza na
vyombo vya habari kwa Zanzibar, tangu uongozi huu ulipoteuliwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuapishwa hivi
karibuni.
MWISHO





Comments
Post a Comment