IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
WADAU wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar
(ZSSF) Pemba wamependekeza, kubakia umri wa kustaafu kwa watumishi kati ya miaka
55 ya hiari mpaka 60, na sio miaka 60 kwa 65, kwani wananchi wengi wanapofikia
umri huo wanakabiliwa na maradhi mbalimbali, ikiwemo shinikizo la damu,
kisukari na ugonjwa wa moyo ambayo humsababishia kushindwa kufanya kazi vizuri.
Walisema
kuwa, rasimu hiyo ya Sheria isiangalie tu watu wachache ambao wana muonekano mzuri
wa kiafya na wenye nguvu katika kipindi cha umri huo, na kuliacha kundi kubwa
ambalo linapofikia umri wa miaka 60 linakabiliwa na maradhi mbalimbali,
yanayowafanya washindwe kuwajibika ipasavyo katika utekelezaji majukumu yao ya kazi
kwenye Ofisi.
Walitoa
mapendekezo hayo wakati walipokuwa kwenye mkutano wa kukusanya maoni juu ya
Mswaada wa Marekebisho ya Sheria ya Mfuko ya Hifadhi ya Jamii Zanzibar,
uliofanyika Ukumbi wa Tibirinzi Chake chake Pemba, wadau hao walipendekeza
kuachwa umri ule ule wa kustaafu wa miaka 60 kwa mtumishi.
"Bora tu Sheria hii ibakishwe kama ilivyo,
kwani mwanachama akiongezewa miaka 65 hatomudu tena kufanya kazi zake kama
mwanzo kutokana na maradhi pamoja na uzee," alisema mdau kutoka Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Amali Abeda Ali Seif.
Kwa
upande wake mdau Asha Mussa Omar kutoka Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi
Zanzibar alisema kuwa, ni bora muda wa kustaafu uwe wa miaka 60 kama ilivyo Sheria
kwani, wengi husubiri pesa zao ili wapate kwenda Hija, hivyo utakapoongezwa
umri wa kustaafu watakosa nguzo muhimu kwao kwa sababu watakuwa hawana nguvu
tena ya kwenda kufanya ibada hiyo, ambayo ina masharti yake maalumu.
Alisema
kuwa, Msaada huo utawasaidia kwa kiasi kikubwa kufahamu, kukuza ustawi wa
kijamii na kiuchumi kwa wa wanachama, kuweka akiba ya muda mrefu na muda mfupi
kwa mahitaji yao ya baadae.
“Msaada
huu ni muhimu sana, lakini kuna baadhi ya vifungu vinapaswa kuwekwa sawa, pia
tunapendekeza kikokotoo cha wastaafu wenye kima cha chini cha mshahara
kizidishwe, ili na wao wae na hali nzuri kimaisha,” alisema.
Nae
mdau Omar Seif Hamad kutoka Shirikisho la Wafanyakazi alipendekeza kuwa, mafao
ya uzazi pia yawekwe kwa wanaume, kwani watumishi wengi wake zao hawafanyi
kazi, hivyo wanakosa haki yao hiyo.
Mdau Ali
Suleiman Othman kutoka Chama cha Wafanyakazi alisema kuwa, rasimu ya Sheria ni
nzuri na imeangalia vigenzo mbalimbali vya Tanzania bara na East Afrika, ambapo
wamefanya kazi nzuri katika kubuni, hivyo amewashukuru wataalumu hao kwa
kuifanya kazi kubwa.
“Kuhusiana
na kipengele cha daktari, amependekeza kuwepo tafsiri rasmi ya daktari kwani
hapo haijafafanuliwa, kwa sababu kwenye mifumo ya kiafya hakuna ‘daktari
maalumu’ hivyo inaweza kuja kuleta shida hapo baadae, naomba tuiweke
sawa,” alisema mdau huyo.
Mapema
akifungua mkutano huo Mkurugenzi wa ZSSF Pemba Msabah Masoud Msabah aliwataka
wadau hao kutoa maoni yenye kujenga, ili kupata Sheria nzuri itakayowanufaisha
wadau wote wa mfuko huo.
Akiwasilisha
rasimu hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Sheria kutoka ZSSF Ramadhan Juma Suleiman
alisema kuwa, lengo na madhumuni ya kuwaita wadau ni kukusanya maoni ya wadau,
ili kupata Sheria nzuri itakayowaongoza na kumgusa kila mtu, ili anufaike na
mfuko huo.
“Rasimu
ya awali iliandaliwa na ZSSF baada ya maoni yenu wadau tukakaa na Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu kuwekwa sawa na sasa tumeirudisha kwenu tena hivyo tunaomba
mutoe maoni yenu yenye kujenga zaidi ili kuboresha,” alisema Mkurugenzi huyo.
MWISHO.
Comments
Post a Comment