NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
UONGOZI wa shehia ya Wawi wilaya ya Chake chake, umewakumbusha wananchi wote wanaotaka kununua ardhi, nyumba na mali nyingine, wasifanye hivyo kwanza, kabla ya kuonana na wasaidizi wa sheria, kwa ajili ya kupata ushauri na msaada wa kisheria.
Sheha wa shehia hiyo Sharifa Waziri Abdalla, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari kufuatia, kuwepo kwa kesi kadhaa za migogoro zinazohusishwa na ununuaji na ardhi na nyumba kimakosa.
Alisema, ndani ya shehia hiyo wapo wasaidizi wa sheria, ambao moja ya kazi zao ambazo ni bila ya malipo, ni kuwapa elimu, ushauri na msaada wa kisheri watu mbali mbali.
Alieleza kuwa, ikiwa wananchi wanataka kuondoa migogoro ya ardhi na mingine, hawanabudi kuwatumia wasaidizi hao wa sheria, ambao hukaa pamoja na kamati ya sheha kwa ajili ya kuepusha migogoro.
‘’Hawa wasaidizi wa sheria tumeletewa na seriali, ili kupunguza migogoro ambayo siyo ya lazima, na wanatoa elimu, ushauri na msaada bila ya malipo,’’alieleza.
Katika hatua nyingine Sheha huyo, alisema wasaidizi wa sheria hapo tu kwa ajili ya kusubiri migogoro na kuitatua, bali wanalojukumu kwa kushirikiana na wananchi pia kuikinga migogoro isitokezee.
‘’Wananchi wasiibue migogoro tu ndio wawatafute wasiaidizi wa sheria, hapana bali kabla haijatokezea wawe nao karibu, kupata ushauri kabla ya kununua au kuuza mali,’’alishauri.
Katibu wa sheha, shehiani humo Sham Haroub Said, alisema ili kuwafahamu kazi zao wasaidizi hao wa sheria, ni wajibu wa wananchi kuhudhuria katika mikutano wanayoiitisha.
‘’Wananchi wamekuwa wazito kuhudhuria kwenye mikutano iliyoitwisha na sheha na wasaidizi wake wa sheria, ndio maana ipo migogoro inatokana na ukosefu wa uwelewa,’’alieleza.
Nae mjumbe wa sheha kijiji cha Mtemani Nassor Said Rashid, alisema migogoro ya ndoa, ardhi, matunzo ya watoto, inaweza kuzuilika ikiwa jamii itashirikiana na wasaidizi wa sheria.
Msaidizi wa sheria shehia za Mgogoni na Wawi Fatma Hilali Salum, alisema wanaendelea kutoa huduma hiyo bila ya malipo, ili kuwasaidia wananchi.
‘’Ni kweli wapo wananchi wanathubutu kunua mfano ardhi nyumba bila ya kujua umiliki halali wa muuzaji na ikiwa yuko peke yake ama laa,’’alieleza.
Alifahamisha kuwa, karibu kila mwezi hupata kesi tatu zinazohusu miogogoro ya iwe mipaka, kuuzwa kwa mtu zaidi ya mmoja, umiliki wa mtu zaidi mmoja, kukosekana kwa hati za umiliki, uhalulishaji au kuuzwa ka eka.
Mkurugenzi wa Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ Mohamed Hassan Abdalla, aliwakumbusha wananchi kuwatumia wasaidizi wa sheria ili kupata ushauri wa kisheria.
Mwananchi Khamis Haji Mohamed, alisema wengi wao walikuwa hawafahamu, juu ya huduma za wasaidizi wa sheria waliomo ndani ya shehia zao.
Khadija Haji Kassim, alisema utoro wa kuhudhuria kwenye mikutano ya shehia, umechangia kwa baadhi yao kukukosa uwelewa wa kuwepo kwa wasaidizi wa sheria.
Maryam Kombo Juma, alisema yeye mara mbili ameshawatumia wasaidizi wa sheria, na kufanikiwa kulipwa deni lake la shilingi 500,000.
‘’Hata juzi nilikuwa na mgogoro wa mipaka na mwenzangu, tulishalisawazisha hilo, kupitia kamati ya sheha iliyokuwa ikioongozwa na wasaidizi wa sheria,’’alieleza.
Akizungumza hivi karibuni kwenye uzinduzi wa kampeni ya Mama Samia ya msaada wa kisheria, Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar Hanifa Ramadhan Said, aliwakumbusba watoa masaada wa kisheria, kuwa makini ili kuepusha kuwa sehemu ya migogoro.
Mkuu wa wilaya ya Mkoani Dk. Hamad Omar Bakar, alisema bado sekta ya sheria, inahitajika mno kwa jamii, ili kuhakikisha waliokata tamaa wanapata haki zao.
Mwisho
Comments
Post a Comment