NA NUSRA SHABAN@@@@
WAWANAWAKE katika nafasi za uongozi wanakutana na changamoto mbalimbali zinazohusiana na usalama wao.
Changamoto hizo zimekuwa sehemu ya hali halisi inayowakumba wanawake wengi ambao wanashika madaraka, haswa katika muktadha wa kijamii na kisiasa.
Katika historia ya Zanzibar, wanawake walikuwa na nafasi ndogo katika maeneo ya uongozi lakini hivi sasa walau idadi ya wanawake viongozi imeongezeka tofauti na miaka ya nyuma.
Mfano hai mwaka 2010, Tanzania iliweza kupata wanawake wabunge 23 waliopata nafasi zao kupitia majimbo ya uchaguzi. Ukijumuisha na wale wa viti maalumu, Bunge la Tanzania likafikisha asilimia 29 ya wabunge wanawake -kiwango cha juu kabisa kwa wakati huo.
Kadhalika, 2020 zilifanyika Chaguzi tatu katika ngazi ya Ubunge na Udiwani ambapo katika chaguzi hizo, jumla ya Wabunge wanawake 73 walishinda chaguzi hizo na kuchaguliwa kuwa Wabunge wa Majimbo huku upande wa Madiwani Jumla ya Wanawake 654 wakichaguliwa kuwa Madiwani katika Shehia husika.
Katika jamii za Zanzibar, wanawake wamekuwa wakiongoza katika sekta mbalimbali, lakini mara nyingi hususani wanawake walio katika vyama vya upinzani, wanakutana na kikwazo kikubwa cha usalama.
Changamoto za kiusalama kwa wanawake viongozi ni pamoja na vitisho vya kimwili, vurugu za kijinsia, kutengwa na kudhalilishwa, pamoja na unyanyapaa kutoka kwa jamii na waandishi wa habari.
Kwa sasa, hakuna takwimu rasmi zinazoonesha kuhusu vitisho vinavyowakumba wanawake viongozi kwa Zanzibar, ingawa kesi hizo zimekuwa zikishuhudiwa kutokea.
Kutoekuepo kwa takwimu hizo, inaonesha jinsi mwamko ulivyo mdogo kwa wanawake Zanzibar katika kuripoti changamoto hizo za kiusalama zinazowatokezea
Asiata Said Abubakar Mjumbe wa Baraza kuu kupitia CHADEMA Zanzibar anasema yeye hajawahi kupitia changamoto hiyo tangu aingie kwenye siasa ingawa anasema wamekuwa wakiona wanawake tofauti wanaopitia changamoto hiyo.
Akitoa mfano, alisema, aliwahi kutekwa Katibu Mwenezi wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA) Taifa, Aisha Machano na kupigwa kisha kutupwa katika pori.
Aliendelea kusema kwamba,kwa upande wa mwanamke yoyote aliye kiongozi akiona vitu kama hivyo vinaweza kumtia hofu na kumfanya arudi nyuma na kushindwa kutimiza ndoto zake za Uongozi.
Utafiti wa UN Women (2023), umeonyesha kuwa vitisho kwa wanawake viongozi, kama vile unyanyasaji wa kijinsia na matusi, huathiri afya ya akili yao na kuleta athari kubwa katika ufanisi wa kazi zao.
Wanawake wengi wameeleza kuwa vitisho vinavyoletwa dhidi yao vinachangia kuongezeka kwa wasiwasi, msongo wa mawazo, na hofu ya usalama.
Kwa wanawake wanaoongoza au kushiriki katika siasa, usalama wao umejikita zaidi katika kutokuwa na uhakika wa kulindwa kutokana na vurugu za kisiasa na matendo ya kudhalilisha.
Makala hii imeangazia changamoto za kiusalama kwa wanawake viongozi, na hatua ambazo zinaweza kuchukuliwa ili kuboresha usalama wao na kuwawezesha kuendelea kutimiza malengo yao bila kuogopa chochote.
Wanawake viongozi Zanzibar wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa katika safari yao ya kuleta mabadiliko.
Changamoto hizo zinaathiri kwa kiasi kikubwa utendaji wao na ndoto zao za kubadili jamii. Bi. Hidaya Yussuph Ali, ambaye ni Katibu wa Ngome ya Wanawake ACT Wazalendo Mkoa wa Kati, anasema:
“Katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2020, nilikumbana na hali ngumu. Wakati wa kurudi nyumbani nilifuatiliwa na watu wasiojulikana hadi nikalazimika kutembea na gari lisilowasha taa majira ya usiku kwa sababu ya usalama.”
Simulizi nyengine ni ya Mtumwa Faiz, mwanachama wa ADC, anasimulia changamoto za kiusalama alizokutana nazo mwaka 2020.
“Binafsi nimekutana na vitisho vya kutishiwa kutiwa ndani kwa kosa la kuulizia juu ya wakala wangu. Lakini bado nilisimama imara kwa sababu najua kazi yangu ni muhimu kwa jamii.”
Changamoto hizo za kiusalama zinahitaji suluhisho la haraka. Vyombo vya usalama vimekuwa na jukumu muhimu katika kulinda wanawake viongozi, kama anavyosema Inspekta Sadiki Ali Sultan ,Mkaguzi msaidizi wa Polisi.
“Jamii ina jukumu kubwa katika kulinda wanawake viongozi. Ushirikiano wa pamoja na uhamasishaji ni nyenzo muhimu za kuondoa changamoto hizi na kuunda mazingira salama kwa kila mmoja.”
Kwa kweli, kulinda wanawake viongozi kunahitaji ushirikiano wa pamoja kati ya vyombo vya usalama na jamii.
Bila uangalizi wa pamoja, wanawake wataendelea kuwa wahanga wa vitisho na unyanyasaji.
Hali ya vitisho dhidi ya wanawake viongozi sio ya Zanzibar pekee. Ripoti ya Umoja wa Mataifa (2016) inasema kuwa asilimia 82 ya wanawake wabunge waliripoti kukumbana na aina fulani ya unyanyasaji wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na vitisho vya kifo, vurugu, na unyanyasaji wa kingono.
Hali hii inadhihirisha kuwa unyanyasaji dhidi ya wanawake wanasiasa ni tatizo linaloendelea.
Shirika la Kimataifa la Wanawake Wanasiasa (IPU) pia linathibitisha kuwa wanawake wanasiasa hukumbana na vitisho vya kutekwa, kufungwa, au hata kuuawa.
Serikali ya Zanzibar inajitahidi kuboresha hali hii kupitia Dira ya 2050 na Mpango wa Maendeleo ya Zanzibar, ambao unalenga kufikia uwiano wa kijinsia wa 50/50 katika nafasi za uongozi.
Ingawa kuna maendeleo katika suala hilo, changamoto zinazowakabili wanawake wanaotaka kushiriki katika uongozi ni kubwa. Ukatili wa kijinsia na vitisho, hasa wakati wa uchaguzi, vinawafanya wanawake wengi kushindwa kufikia malengo yao.
Changamoto za kiusalama kwa wanawake viongozi ni tatizo linalohitaji hatua za haraka. Jamii inapaswa kushirikiana kuhamasisha, kuelimisha, na kulinda viongozi hawa ili waweze kutimiza ndoto zao za kuleta mabadiliko.
Ili kuendelea kufikia malengo ya uwiano wa kijinsia, lazima tuzingatie umuhimu wa usalama wa wanawake na kutoa msaada wa kutosha ili kuhakikisha mazingira salama kwao.
Kwa kumalizia, makala hii ni jukumu la kila mmoja kuunga mkono na kusaidia wanawake katika safari yao ya kuleta mabadiliko. Haki yao ya kuongoza katika mazingira salama ni muhimu kwa maendeleo ya jamii.
MWISHO
Comments
Post a Comment