NA HAJI NASSOR, PEMBA
WASAIDIZI wa sheria tarajali kisiwani Pemba, wameelezwa
kuwa, moja ya jambo linalowaondoa kwenye usaidizi wa sheria, ni kujiingiza
kwenye siasa za wazi wazi.
Hayo yameelezwa na
Afisa sheria kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar, Ali Haji
kwenye mafunzo yanayoendelea ya siku 15, yanayofanyika Chakechake.
Alisema kila mtu
kikatiba yuko huru kuamini dini na hata imani ya chama cha siasa akipendacho,
ingawa kwa wasaidizi wa sheria, lazima wajiwekee mipaka.
'’Ni haki ya
kikatiba kushiriki katika masuala ya siasa na hasa kuchagua na kuchaguliwa,
ingawa kwenu wasaidizi wa sheria muwe makini na ushabiki wa kupindukia,’'alieleza.
Kwa upande wake
Naibu Mkuu wa skuli ya sheria Zanzibar kitengo cha taaluma, Msemo Mavare alisema
suala la kuthibitisha jambo mahakamani, lina njia zake kadhaa.
Alisema mfano ni
kukiri jambo ‘confession’ pasi na kutenzwa nguvu, kuahidiwa jambo, sambamba
na njia ya kuwa na mashahidi.
Hivyo amewashauri
wasaidizi hao wa sheria tarajali, kuisoma kwa kina sheria ya ushahidi, ili
kuwasidia wananchi wanaowafikia kutaka msaada na ushauri wa kisheria.
"Sheria hii
ya ushahidi ni kubwa, lakini hamna budi kuipitia na kuisoma vile vifungu muhimu,
kikiwemo cha nani shahidi, aina ya ushahidi pamoja na njia za kutoa
ushahidi," alisema.
Akiwasilisha mada
ya njia za unasihi kwa wahanga wa matukio ya udhalilishaji, Afisa Idara ya
ustawi wa jamii Pemba Fatma Abdalla, alisema ni eneo linalohitaji ujuzi wa hali
ya juu.
Alifahamisha kuwa,
shurti moja wapo kwa mtoa ushauri nasihi ni kumjua kwa kina mteja wake, aina ya
udhalilishaji aliyofanyiwa na athari.
"Huwezi kuwa
mshauri nasihi mzuri, ikiwa hawezi kujenga masuali yanayoweza kukupa taarifa,
pamoja na ujuzi wa uchaguzi wa lugha,"alifahamisha.
Mapema wakili wa
serikali Seif Mohamed Khamis, aliwataka washiriki hao, kuhakikisha wanaielewa
katiba hasa vile vipengele muhimu zaidi.
‘’Kwa mfano
Katiba ya Zanzibar yam waka 1984, kuanzia kifungu cha 11 hadi cha 25
kinachoeleezea haki za binadamu, muhakikisha mnavipitia mara kwa
mara,’’alishauri.
Baadhi wa
washiriki, walisema elimu hiyo ni nzuri ingawa changamoto iliyobakia ni jamii
kubadili mtazamo kuwa hilo ni jukumu la serikali pekee.
Mshiriki Juma
Seif kutoka jimbo la Chonga, Wahida Kombo Khamis wa jimbo la Chake chake na
Fatma Hamad Faki wa jimbo la Wingwi wameahidi kuifikisha elimu hiyo kwa jamii.
mwisho |
Comments
Post a Comment