NA HAJI NASSOR, PEMBA
BIBI Maryam Bakar Issa miaka 60,
mkaazi wa shehia ya Ukunjwi, ni mmoja kati ya walengwa 14,280 wanaopokea fedha
za mpango wa kunusuru kaya maskini, kutoka TASAF Pemba.
Mpango huo,
kwake ulianza kumfikia miaka minane iliyopita, akipokea kati ya shilingi 30,000
hadi shilingi 44,000 kila baada ya miezi miwili, hutegemeana na kukidhi masharti.
Mpango huo
ulikuwa na maana sana kwake, kwa vile mwaka 2013 kabla ya kuingia kwenye ruzuku,
alifiliwa na mume wake na kumuachia watoto wawili wadogo, walioanza kumtegemea.
Kilomo cha
muhogo, mpunga, migomba na kazi ya uvuvi wa chaza, ndio aliyokuwa kazi yake alikuwa
akiitegemea kwa wakati huo kuendesha familia yake.
Maisha
yalikuwa mazito, hasa pale anapokwenda pwani na kukosa chaza, vipando bado
vichanga na dukani ana deni, na watoto wanahitaji walau mlo mmoja.
“Uwanawake
wangu ulikuwa ni pale nnapokwenda pwani na kurudi na chaza, ili niziweke pamoja
kwenye njiti za makuti kwa ajili ya biashara, ili nipate unga wa sembe na
nyingine kuzifanya kitoweleo cha siku,’’anasema.
Wakati akiwa
anavuna muhogo au ndizi, ndio kipindi alichokuwa na uhakika wa mlo wa siku na
watoto wake mayatima, ingawa huwa ni kipindi kifupi.
Anasema
kipindi cha jua, hutumia miale yake inayopenya kwa juu ya paa la nyumba yake,
kufanya shughuli zake kutokana na makuti kuoza.
“Lakini hata
usiku kama mwezi unang’aa, sikuwa nahitaji taa, kutokana na miale yake kuingia
mwangu bila ya kizuizi, achia mbali mvua haina hodi,’’anasimulia.
Maisha ya kubahatisha,
yaliyozaa dhiki, shida, na uchungu, wakati mwengine, yalipelekea watoto wake
kusimamishwa masomo, kuanzia madrassa hadi skuli kwa wakati huo.
Hakuwa na
tamaa kuwa, iko siku ataishi maisha ya furaha kama wengine, achia mbali kuishi
kwenye nyumba ya kisasa yenye huduma za lazima.
BAADA YA KUFIKIWA NA MPANGO WA TASAF
Kwa mara ya
kwanza, alipopokea taarifa kutoka kwa Sheha wake wa Ukunjwi, juu ya kuatakiwa
kuorodhesha majina ya watoto wake, aliona ni pumbazo la viongozi.
“Nilipofuatwa
na Sheha kuwa natakiwa kuandikisha majini ya watoto wangu na kisha nilipwe,
nilikuwa na hakika jambo hilo haliwezekani,’’anasimulia.
Maana,
anaona kwenye akili yake, ili mtu alipwe kwanza atanguliwe na kufanyakazi,
ambapo wakati huo yeye akiwa ameshaanza kupungua nguvu.
Siku ya
kujazishwa fomu, anasema ilifika na kisha kusbiria mwisho wa mwezi, ambapo
aliahidiwa kulipwa na siku ilipofika, alikuwa mtu wa pili.
“Malipo ya
mwanzo nilipotakiwa kwenda kusaini, hata msuwaki na kunawa uso nilisahau siku
hiyo, maana ilikuwa roho na moyo wangu haukubali kuwa TASAF, inilipe kabla ya
kufanyakazi,’’anahadithia.
Bibi Maryam
ambae kwa sasa anatimiza miaka 60, anasema fedha hizo za mwanzo, alinunua
mchele na samaki mnene na kula na watoto wake mapema.
Anakiri kuwa,
fedha alizopewa alielezwa madhumuni yake, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha watoto
wanakwenda skuli kwa wakati, ununuzi wa vifaa husika.
Kuanzia hapo
na mwezi mwengine, Bi Maryam anasema aliamini kuwa sasa, anataka kunusuriwa na
umaskini, na elimu ya kuzifanyia shughuli nyingine fedha hizo, ili zizae.
Ilipofika
mwaka 2018, anasema huku akiwa anaweka fedha hizo nusu kwenye hisa na watoto
wake wakiongezeka umri, alimuita mtoto wake, mwenye miaka 18, kumpa wazo la
kununua mtumbwi.
!!!!!...naam
siku ikafika, bi Maryam ambae ni mlengwa wa kaya maskini, shehia ya Ukunjwi
wilaya ya Wete, kununua mtumbwi kwa shilingi 300,000.
Wapi alikuwa
akizitunza fedha hizo na muda gani, nilumuuliza na kusema kuwa, alikuwa
akiziweka ndani mwake hadi kutimia kiwango cha ununuzi wa mtumbwi.
Aliacha
kununua boda boda wala kuanzisha biashara, akisema kazi ya Ukunjwi ambayo ni
rahisi ya yenye kipato cha haraka, ni uvuvi.
Anasema,
sasa anaishi kwenye maisha ya furaha na kusahau yale madhila na machungu ya
miaka karibu 50, aliyokuwa nayo.
“Mtoto wangu
ndie anenivisha, kunilisha asubuhi na jioni na wakati mwengine hunipa fedha
hadi kufiki shilingi 100,000 na huku bado naendelea kupokea kutoka
TASAF,’’anasema.
Sasa bi Maryam,
anasema haikimbii tena michango ya familia iwe ya harusi, ungonjwa au kufiliwa,
maana wakati wowote akiba ya shilingi 100,000 hadi shilingi 300,000 kwake sio
jambo kubwa.
Jee bibi
Mrayam ni mvuvi wa mtumbwi, nilipomuuliza alisema alishaacha kuvua chaza kwa
miguu miaka minne iliyopita, ingawa alimpa mtoto wake Abdi Abdalla Khamis.
MTOTO WA MLENGWA: ABDI ABDALLA KHAMIS
Yeye shuguli
ya uvuvi, alianza mara tu baada ya kumaliza masomo yake darasa la 12, miaka
miwili iliyopita, na kisha alipoamua kutaka kufungu ndoa, alitumia gharama
wastani wa shilingi milioni 1, zilizotokana na mtumbwi huo.
Abdi,
anasema ubunifu wa mama yake kuweka fedha hadi kufikia shilingi 300,000 na
kumnunulia mtumbwi, ndio unaompa uhakika wa kuendesha familia yake, na mama
yake kwa ujumla.
“Mtumbwi
ulizaa mahari yangu ya ndoa ya kwanza, na hadi nilipoa tena mke wa pili
shilingi 700,000 zilitoka kwenye mtumbwi ulionunuliwa na mama,’’anasema.
Kwa mwezi
mmoja, huwa anakwenda baharini siku 15, kutokana na mabadiliko ya bahari, na hujiingizia
kati ya shilingi 50,000 hadi 70,000 ingawa inategemea na bahari ilivyoamka.
Ndio maana,
Abdi sasa kwa mwezi mmoja hujipatia kati ya shilingi 750,000 wastani wa
shilingi 50,000 kwa siku 15 za mwezi, anazokwenda baharini.
Hapo utaona
mvuvi huyo mwenye asili ya fedha za TASAF za shilingi 40,000 za mpango wa
kunusuru kaya maskini, kwa mwaka anajipatia shilingi milioni 9,000,000.
Kwa sasa
tayari, ameshanunu matofali 1000, kwa thamani ya shilingi milioni 1, akiweka
malengo ya kujenga nyumba yao ya familia yenye vyumba vinne, kama lengo la mama
yake lilivyo.
Miaka miwili
ijayo, anatarajia amalize ujenzi wa nyumba hiyo, na kisha anampango wa kununua
boda boda, kwa ajili ya kuongeza pato lake zaidi.
‘’Unajua
fedha za TASAF ambazo mama anendelea kupata zimefika pahala ndipo, maana awali
aliponikabdhi mtumbwi niliona kama vile sio sahihi, lakini sasa matunda
yapo,’’anasema.
SHEHA
Sheha wa
shehia ya Ukunjwi Mkongwe Kassande Khamis, anasema, walengwa kama bibi Maryam
kwenye shehia yake wapo zaidi ya 10.
Hao
wamejiongeza na wamekuwa mfano wa kuukimbia umaskini, kwa kule kujiajiri
wenyewe, kama ilivyo azma ya TASAF, kupitia mpango huo.
Shehia ya
Ukunjwi yenye wakaazi 3,429 ingawa waliomo kwenye mpango huo walikuwa 239 na kwa
sasa wanaondelea ni 215 baada ya wengine kufariki.
Vipo vikundi
12 vilivyoundwa na walengwa wa kaya maskini, ikihusishwa wananchi 240, ambao
fedha zao wameamua kuzikukuza.
“Kwa hakika
TASAF shehiani mwangu, inaendelea kuacha alama, maana sasa wapo wananchi
wanaojenga nyumba za kudumu, walioanzisha miradi ya kimaendeleo kama ufugaji,
mtumbwi na kilimo,’’anasema.
Anajivunia
mlengwa kama bibi Maryam licha ya umri wake, lakini amebuni mradi wa mtumbwi,
ambao sasa unamsaidia kimaisha.
TASAF
Mratibu wa
TASAF Pemba Mussa Said, anasema wapo walengwa 14,280 kwa Pemba ambao
wanaendelea kupata fedha za kunusuriwa na umaskini.
Walengwa hao
wapo kwenye shehia 78 ikiwemo ya Ukunjwi, Tumbe Mashariki, Mgogoni, Kiwani,
Ndagoni, Makangale ambapo tayari
shilingi bilioni 14. 4 zimeshwafikia.
Mtu kama bi Maryam
ndio hasa ametimiza yale, malengo ya TASAF, ya kumtoa mwananchi katika unyonge wa
kipato na chakula na kumleta kwenye taa.
“TASAF inaorodhesha
ya zaidi ya walengwa 50,000 kutoka wastani wa walengwa 15 kila shehia, kati ya
shehia 78, ambao wamenzisha miradi ya kujikwamua.
“Mtu kama bi
Fatma wa Tumbe anaemiliki nyumba, Amina wa Mgogoni na mwenzake Mfake wenye
mifugo, hatuna shaka, hawawezi kurudi tena kwenye umaskini wa kipato, wanafikia
50,000 kwa Pemba yote,’’anaeleza.
Mratibu
Mussa anabainisha kuwa, kwa mwaka 2014/2015 walengwa hao wa kunusuru kaya
maskini, waliibua miradi ya kijamii 41, idadi iliongozeka mwaka uliofuata kwa
kufikia miradi 84.
Mwaka 2017/2018
walijukuta na miradi mengine ya kijamii 21, inayuhusisha upandaji miti kama
vile Makangale, uazishwaji wa vitalu na ujenzi wa matuta ya kinga maji ya
bahari Ndagoni, Kiwani, Micheweni na Tumbe.
Achia mbali
idadi ya watu 50,000 waliojiwekeza wenyewe, vipo vikundi 942 vikizaa walengwa
12,000 vilivyoanzishwa, kuanzia mwaka 2014 hadi 2019, ingawa vilivyosajiliwa ni
700.
WANANCHI WA UKUNJWI
Imani Haji
Khamis, anasema bibi Maryam ameona mbali kwa kule kumnunulia mtoto wake
mtumbwi, kwa ajili ya kuendeleza sekta ya uvuvi.
Omar Hassan
Shaibu anasema, moja ya shughuli adhimu ya shehia ya Ukunjwi ni bahari, hivyo
wazo la bi Maryam kutumia fedha zake katika eneo hilo, hazikupotea.
Kazija Idd
Abdi anasema, bi Maryam hakuamua kuingia kwenye ushirika wowote, na tulidhani
anaweza kupotea njia kwenye kujikwamua na umaskini, lakini ni tofauti.
Mtoto wake
ameshaanza ujenzi kupitia mtumbwi, ameshaoa pia lakini anaendesha maisha yake
kwa uzuri, maana anavua peke yake anachokipata hagawani na mwengine.
Mwisho
Comments
Post a Comment